Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 45:16-28

Mwanzo 45:16-28 SRUV

Habari ikasikika nyumbani mwa Farao kusema, Ndugu zake Yusufu wamekuja. Ikawa vema machoni pa Farao, na machoni pa watumishi wake. Farao akamwambia Yusufu, Uwaambie ndugu zako, Fanyeni hivi; wabebesheni mizigo wanyama wenu, mwondoke mwende nchi ya Kanaani; kisha mkamtwae baba yenu, na watu wa nyumbani mwenu, mkanijie; nami nitawapa mema ya nchi ya Misri, nanyi mtakula unono wa nchi. Nawe umeamriwa; fanyeni hivi, mjitwalie magari katika nchi ya Misri kwa watoto wenu wadogo na wake zenu, mkamchukue baba yenu mje. Wala msivisumbukie vyombo vyenu, maana mema ya nchi yote ya Misri ni yenu. Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli. Yusufu akawapa magari kama Farao alivyoamuru, akawapa na chakula cha njiani. Akawapa kila mtu nguo za kubadili; lakini Benyamini, alimpa fedha mia tatu na mavazi matano ya kubadili. Na baba yake akampelekea vifuatavyo: punda kumi waliochukua mema ya Misri, na punda majike kumi waliochukua nafaka, na mikate, na chakula cha njiani kwa babaye. Akaagana na ndugu zake, wakaenda zao; naye akawaambia, Msigombane njiani. Wakatoka Misri, wakafika nchi ya Kanaani kwa Yakobo, baba yao. Wakampasha habari, wakisema, Yusufu angali hai; naye ndiye mtawala katika nchi yote ya Misri. Moyo wake ukazimia, kwa sababu hakuwasadiki. Wakamwambia maneno yote ya Yusufu, aliyowaambia; na alipoona magari aliyotuma Yusufu, ili kumchukua, roho ya Yakobo baba yao ikafufuka. Israeli akasema, Yatosha! Yusufu mwanangu angali hai; nitakwenda, nionane naye kabla sijafa.

Soma Mwanzo 45