Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 45:16-28

Mwanzo 45:16-28 NEN

Habari zilipofika kwenye jumba la Farao kwamba ndugu zake Yosefu wamefika, Farao na maafisa wake wote wakafurahi. Farao akamwambia Yosefu, “Waambie ndugu zako, ‘Fanyeni hivi: Pakieni wanyama wenu mrudi mpaka nchi ya Kanaani, mkamlete baba yenu na jamaa zenu kwangu. Nitawapa sehemu nzuri sana ya nchi ya Misri nanyi mtafurahia unono wa nchi.’ “Mnaagizwa pia kuwaambia, ‘Fanyeni hivi: Chukueni magari ya kukokotwa kutoka Misri, kwa ajili ya watoto wenu na wake zenu, mkamchukue baba yenu mje. Msijali kamwe kuhusu mali zenu, kwa sababu mema yote ya Misri yatakuwa yenu.’ ” Hivyo wana wa Israeli wakafanya hivyo. Yosefu akawapa magari ya kukokotwa, kama Farao alivyoagiza, pia akawapa mahitaji kwa ajili ya safari yao. Kila mmoja mavazi mapya, lakini Benyamini akampa shekeli 300 za fedha, na jozi tano za nguo. Hivi ndivyo vitu alivyotuma kwa baba yake: punda kumi waliochukua vitu vizuri vya Misri, punda wake kumi waliobeba nafaka, mikate na mahitaji mengine ya safari. Akaagana na ndugu zake walipokuwa wakiondoka, akawaambia, “Msigombane njiani!” Basi wakatoka Misri na kufika kwa baba yao Yakobo katika nchi ya Kanaani. Wakamwambia baba yao, “Yosefu angali hai! Ukweli ni kwamba yeye ndiye mtawala wa Misri yote.” Yakobo akapigwa na bumbuazi; hakuwasadiki. Lakini walipokwisha kumweleza kila kitu ambacho Yosefu alikuwa amewaambia, na alipoona magari ya kukokotwa Yosefu aliyokuwa amempelekea ya kumchukua aende Misri, roho ya baba yao Yakobo ikahuishwa. Ndipo Israeli akasema, “Nimesadiki! Mwanangu Yosefu bado yu hai. Nitakwenda nikamwone kabla sijafa.”