Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 41:9-36

Mwanzo 41:9-36 SRUV

Basi mkuu wa wanyweshaji akamwambia Farao akisema, Nayakumbuka makosa yangu leo. Farao aliwakasirikia watumishi wake, akanitia nifungwe nyumbani mwa mkuu wa askari walinzi, mimi na mkuu wa waokaji. Tukaota ndoto usiku mmoja, mimi na yeye; kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake tukaota. Na huko pamoja nasi palikuwa na kijana; Mwebrania, mtumishi wa mkuu wa askari, tukamhadithia, naye akatufasiria ndoto zetu; akamfasiria kila mtu kama ilivyokuwa ndoto yake. Ikawa, kama vile alivyotufasiria ndivyo ilivyotokea; mimi nilirudishwa katika kazi yangu, na yeye alitundikwa. Ndipo Farao akatuma watu kumwita Yusufu, wakamleta upesi kutoka gerezani. Akanyoa, akabadili nguo zake, na kuingia kwa Farao. Farao akamwambia Yusufu, Nimeota ndoto, wala hakuna awezaye kunifasiria; nami nimesikia habari zako, ya kwamba, usikiapo ndoto, waweza kuifasiri. Yusufu akamjibu Farao, akisema, Si mimi; Mungu atampa Farao majibu ya amani. Farao akamwambia Yusufu, Katika ndoto yangu nilikuwa nimesimama ukingoni mwa mto; na tazama, ng'ombe saba wanatoka mtoni, wanono, wazuri, wakajilisha nyasini. Kisha, tazama, ng'ombe saba wengine wakapanda baada yao, dhaifu, wabaya sana, wamekonda; katika nchi yote ya Misri sijaona kama hao kwa udhaifu. Na hao ng'ombe waliokonda, wabaya, wakawala wale ng'ombe saba wa kwanza, wale wanono. Na walipowala haikutambulikana ya kwamba wamewala, bali wakaonekana wabaya kama kwanza. Basi nikaamka. Kisha nikaona katika ndoto yangu, na tazama, masuke saba yanatokeza katika bua moja, mema, yamejaa. Na tazama, masuke saba membamba, dhaifu, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao. Na hayo masuke dhaifu yakameza yale masuke saba mema. Nami nikawaambia hao waganga, wala hakuna aliyeweza kunionesha maana yake. Yusufu akamwambia Farao, Ndoto ya Farao ni moja; Mungu amemwonesha Farao atakayoyafanya hivi karibuni. Wale ng'ombe saba wema ni miaka saba; na yale masuke saba mema ni miaka saba. Ndoto ni moja. Na wale ng'ombe saba, dhaifu, wabaya, waliopanda baada yao, ni miaka saba; na yale masuke saba matupu yaliyokaushwa na upepo wa mashariki, yatakuwa miaka saba ya njaa. Ndivyo nilivyomwambia Farao, ya kwamba Mungu amemwonesha Farao atakayoyafanya hivi karibu. Tazama, miaka saba ya shibe inakuja, katika nchi yote ya Misri. Kisha kutakuja miaka saba ya njaa baada yake; na shibe ile yote itasahauliwa katika nchi ya Misri, na njaa itaiharibu nchi. Wala shibe ile haitajulikana katika nchi kwa sababu ya njaa inayokuja baadaye, maana itakuwa kali sana. Na ndoto ya Farao kwa vile ilivyokuja mara mbili, ni kwa sababu neno hilo Mungu amelithibitisha, na Mungu atalitimiza upesi. Basi, Farao na ajitafutie mtu wa akili na hekima amweke juu ya nchi ya Misri. Farao na afanye hivi, tena akaweke wasimamizi juu ya nchi, na kutwaa sehemu ya tano katika nchi ya Misri, katika miaka hii saba ya kushiba. Na wakusanye chakula chote cha miaka hii myema ijayo, wakaweke akiba ya nafaka mkononi mwa Farao wakakilinde kuwa chakula katika miji. Na hicho chakula kitakuwa akiba ya nchi kwa ajili ya miaka hiyo saba ya njaa, itakayokuwa katika nchi ya Misri, nchi isiharibike kwa njaa.

Soma Mwanzo 41