Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 41:9-36

Mwanzo 41:9-36 NEN

Ndipo mnyweshaji mkuu alipomwambia Farao, “Leo nimekumbushwa kuhusu kosa langu. Wakati fulani Farao aliwakasirikia watumishi wake, akanifunga mimi na mwokaji mkuu katika nyumba ya mkuu wa ulinzi. Kila mmoja wetu aliota ndoto katika usiku mmoja na kila ndoto ilikuwa na maana yake tofauti. Basi kijana wa Kiebrania aliyekuwa pamoja nasi huko, alikuwa mtumishi wa mkuu wa kikosi cha ulinzi. Tulimweleza ndoto zetu, naye akatufasiria, akitupa kila mtu tafsiri ya ndoto yake. Nayo mambo yakawa sawa kabisa na jinsi alivyotufasiria ndoto zetu: Mimi nilirudishwa kazini mwangu na huyo mtu mwingine akaangikwa.” Basi, Farao akatuma Yosefu aitwe, naye akatolewa kifungoni haraka. Baada ya kunyoa na kubadilisha nguo zake akaenda mbele ya Farao. Farao akamwambia Yosefu, “Nimeota ndoto, wala hakuna mtu hata mmoja anayeweza kuifasiri. Lakini nimesikia ikisemwa kwa habari yako kwamba unapoelezwa ndoto waweza kuifasiri.” Yosefu akamjibu Farao, “Siwezi kuifasiri, lakini Mungu atampa Farao jibu analolihitaji.” Kisha Farao akamwambia Yosefu, “Katika ndoto yangu nilikuwa nimesimama ukingoni mwa Mto Naili, nikawaona ngʼombe saba, wazuri na wanono, wakijitokeza kutoka mtoni wakaja kujilisha kwenye matete. Baada ya hao, ngʼombe wengine saba wadhaifu wakatokea, wabaya sana na waliokonda. Kamwe sikuwahi kuona ngʼombe wabaya jinsi hiyo katika nchi yote ya Misri. Hao ngʼombe waliokonda na wabaya sana wakawala wale ngʼombe saba walionona waliojitokeza kwanza. Lakini hata baada ya kuwala, hakuna mtu ambaye angeweza kusema kwamba wamekula, bado walionekana wabaya kama mwanzoni. Kisha nikaamka kutoka usingizini. “Pia katika ndoto zangu niliona masuke saba ya nafaka, yamejaa na mazuri, yanakua katika bua moja. Baada ya hayo masuke mengine saba yakachipua, yaliyonyauka, membamba na yamekaushwa na upepo wa mashariki. Yale masuke membamba ya nafaka yakayameza yale masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka. Nimewaeleza waaguzi, wala hakuna yeyote aliyeweza kunifasiria.” Ndipo Yosefu akamwambia Farao, “Ndoto za Farao ni ndoto iyo hiyo moja. Mungu amemfunulia Farao jambo analokusudia kufanya karibuni. Ngʼombe saba wazuri ni miaka saba, nayo masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka ni miaka saba, ni ndoto iyo hiyo moja. Ngʼombe saba waliokonda na wabaya wale waliojitokeza baadaye ni miaka saba, vivyo hivyo masuke saba ya ngano yaliyodhoofika na kukaushwa na upepo wa mashariki, ni miaka saba ya njaa. “Ni kama vile nilivyomwambia Farao: Mungu amemwonyesha Farao jambo analokusudia kufanya karibuni. Miaka saba ya neema inakuja katika nchi yote ya Misri, lakini itafuata miaka saba ya njaa. Ndipo neema yote ya Misri itasahaulika na njaa itaikumba nchi. “Neema iliyokuwa katika nchi haitakumbukwa, kwa sababu njaa itakayofuata itakuwa kali mno. Sababu ya ndoto kumjia Farao kwa namna mbili ni kwamba jambo hilo Mungu ameshaamua kwa hakika, naye Mungu atalifanya karibuni. “Basi sasa Farao na atafute mtu mwenye akili na hekima ili amweke kuwa msimamizi wa nchi ya Misri. Farao na aweke wenye amri nchini kote wakusanye sehemu ya tano ya mavuno ya Misri katika miaka hii saba ya neema. Wakusanye chakula chote katika miaka hii saba ya neema inayokuja na kuhifadhi nafaka chini ya mamlaka ya Farao, iwe akiba ya chakula katika miji. Chakula hiki kitakuwa akiba ya tahadhari kwa ajili ya nchi, ili kitumike katika ile miaka saba ya njaa itakayokuja Misri, ili nchi isiharibiwe na njaa.”