Mwanzo 40:1-15
Mwanzo 40:1-15 SRUV
Ikawa, baada ya mambo hayo, mnyweshaji wa mfalme wa Misri, na mwokaji wake, wakamkosea bwana wao, mfalme wa Misri. Farao akawaghadhibikia maofisa wake wawili, mkuu wa wanyweshaji na mkuu wa waokaji. Akawatia katika ulinzi nyumbani mwa mkuu wa askari, humo gerezani, mahali alipofungwa Yusufu. Mkuu wa askari akamwekea Yusufu watu hao, naye akawahudumia, nao wakakaa siku kadhaa katika kifungo. Wakaota ndoto wote wawili, kila mtu ndoto yake usiku mmoja, kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake, mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri waliofungwa gerezani. Yusufu akawajia asubuhi, akawaona wamefadhaika. Akawauliza hao maofisa wa Farao, waliokuwa pamoja naye katika kifungo, nyumbani mwa bwana wake, akisema, Mbona nyuso zenu zimekunjamana leo? Wakamwambia, Tumeota ndoto wala hapana awezaye kuifasiri. Yusufu akawaambia, Nawaomba mniambie, kufasiri si ni kazi ya Mungu? Mnyweshaji mkuu akamhadithia Yusufu ndoto yake; akamwambia, Katika ndoto yangu nimeota, uko mzabibu mbele yangu. Na katika mzabibu mlikuwa na matawi matatu, nao ulikuwa kana kwamba unamea, unachanua maua, vishada vyake vikatoa zabibu zilizoiva. Na kikombe cha Farao kilikuwa mkononi mwangu, nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe cha Farao, nikampa Farao kikombe mkononi mwake. Yusufu akamwambia, Tafsiri yake ndiyo hii. Matawi matatu ni siku tatu. Baada ya siku tatu Farao atakiinua kichwa chako, atakurudisha katika kazi yako; nawe utampa Farao kikombe mkononi mwake, kama desturi ya kwanza, ulipokuwa mnyweshaji wake. Ila unikumbuke mimi, utakapopata mema, ukanifanyie fadhili, nakuomba, ukanitaje kwa Farao, na kunitoa katika nyumba hii. Kwa sababu hakika niliibwa kutoka nchi ya Waebrania, wala hapa sikutenda jambo lolote hata wanitie gerezani.