Mwanzo 40:1-15
Mwanzo 40:1-15 NEN
Baada ya muda, mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri, wakamkosea bwana wao, mfalme wa Misri. Farao akawakasirikia hawa maafisa wake wawili, mnyweshaji mkuu na mwokaji mkuu, akawaweka chini ya ulinzi katika nyumba ya mkuu wa kikosi cha ulinzi katika gereza lile lile alimofungwa Yosefu. Mkuu wa kikosi cha ulinzi akawakabidhi kwa Yosefu, naye akawahudumia. Walipokuwa wamekaa chini ya ulinzi kwa muda, kila mmoja wa hao wawili waliokuwa wamewekwa gerezani, yaani mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri, waliota ndoto usiku mmoja, na kila ndoto ilikuwa na maana yake tofauti. Yosefu alipowajia asubuhi yake, akawaona kwamba walikuwa na huzuni. Ndipo Yosefu akawauliza maafisa hao wa Farao waliokuwa chini ya ulinzi pamoja naye nyumbani mwa bwana wake, akasema, “Mbona nyuso zenu zimejaa huzuni leo?” Wakamjibu, “Sisi sote tuliota ndoto, lakini hapakuwa na mtu yeyote wa kuzifasiri.” Ndipo Yosefu akawaambia, “Je, kufasiri ndoto si kazi ya Mungu? Niambieni ndoto zenu.” Basi mkuu wa wanyweshaji akamweleza Yosefu ndoto yake. Akamwambia, “Katika ndoto yangu niliona mzabibu mbele yangu, nao mzabibu ulikuwa na matawi matatu. Mara tu ulipoanza kuchipua, maua yalichanua na vishada vyake vikawa zabibu zilizoiva. Kikombe cha Farao kilikuwa mkononi mwangu, nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe cha Farao, na nikaweka kikombe mkononi mwake.” Yosefu akamwambia, “Hii ndiyo maana yake: Matawi matatu ni siku tatu. Katika siku hizi tatu, Farao atakutoa gerezani na kukuweka tena kwenye nafasi yako, nawe utaweka kikombe cha Farao mikononi mwake, kama vile ulivyokuwa unafanya ulipokuwa mnyweshaji wake. Lakini wakati mambo yatakapokuwia mazuri, unikumbuke, unifanyie wema, useme mema juu yangu kwa Farao ili niondoke huku gerezani. Kwa maana nilichukuliwa kwa nguvu kutoka nchi ya Waebrania, na hata hapa nilipo sikufanya lolote linalostahili niwekwe gerezani.”