Mwanzo 40:1-15
Mwanzo 40:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa, baada ya mambo hayo, mnyweshaji wa mfalme wa Misri, na mwokaji wake, wakamkosea bwana wao, mfalme wa Misri. Farao akawaghadhibikia maofisa wake wawili, mkuu wa wanyweshaji na mkuu wa waokaji. Akawatia katika ulinzi nyumbani mwa mkuu wa askari, humo gerezani, mahali alipofungwa Yusufu. Mkuu wa askari akamwekea Yusufu watu hao, naye akawahudumia, nao wakakaa siku kadhaa katika kifungo. Wakaota ndoto wote wawili, kila mtu ndoto yake usiku mmoja, kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake, mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri waliofungwa gerezani. Yusufu akawajia asubuhi, akawaona wamefadhaika. Akawauliza hao maofisa wa Farao, waliokuwa pamoja naye katika kifungo, nyumbani mwa bwana wake, akisema, Mbona nyuso zenu zimekunjamana leo? Wakamwambia, Tumeota ndoto wala hapana awezaye kuifasiri. Yusufu akawaambia, Nawaomba mniambie, kufasiri si ni kazi ya Mungu? Mnyweshaji mkuu akamhadithia Yusufu ndoto yake; akamwambia, Katika ndoto yangu nimeota, uko mzabibu mbele yangu. Na katika mzabibu mlikuwa na matawi matatu, nao ulikuwa kana kwamba unamea, unachanua maua, vishada vyake vikatoa zabibu zilizoiva. Na kikombe cha Farao kilikuwa mkononi mwangu, nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe cha Farao, nikampa Farao kikombe mkononi mwake. Yusufu akamwambia, Tafsiri yake ndiyo hii. Matawi matatu ni siku tatu. Baada ya siku tatu Farao atakiinua kichwa chako, atakurudisha katika kazi yako; nawe utampa Farao kikombe mkononi mwake, kama desturi ya kwanza, ulipokuwa mnyweshaji wake. Ila unikumbuke mimi, utakapopata mema, ukanifanyie fadhili, nakuomba, ukanitaje kwa Farao, na kunitoa katika nyumba hii. Kwa sababu hakika niliibwa kutoka nchi ya Waebrania, wala hapa sikutenda jambo lolote hata wanitie gerezani.
Mwanzo 40:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa, baada ya mambo hayo, mnyweshaji wa mfalme wa Misri, na mwokaji wake, wakamkosa bwana wao, mfalme wa Misri. Farao akawaghadhibikia maakida wake wawili, mkuu wa wanyweshaji na mkuu wa waokaji. Akawatia katika lindo nyumbani mwa mkuu wa askari, humo gerezani, mahali alipofungwa Yusufu. Mkuu wa askari akamwekea Yusufu watu hao, naye akawahudumu, nao wakakaa siku kadha wa kadha katika kifungo. Wakaota ndoto wote wawili, kila mtu ndoto yake usiku mmoja, kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake, mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri waliofungwa gerezani. Yusufu akawajia asubuhi, akawaona wamefadhaika. Akawauliza hao maakida wa Farao, waliokuwa pamoja naye katika kifungo, nyumbani mwa bwana wake, akisema, Mbona nyuso zenu zimekunjamana leo? Wakamwambia, Tumeota ndoto wala hapana awezaye kuifasiri. Yusufu akawaambia, Kufasiri si kazi ya Mungu? Tafadhalini mniambie. Mnyweshaji mkuu akamhadithia Yusufu ndoto yake; akamwambia, Katika ndoto yangu nimeota, uko mzabibu mbele yangu. Na katika mzabibu mlikuwa na matawi matatu, nao ulikuwa kana unamea, unachanua maua, vishada vyake vikatoa zabibu zilizoiva. Na kikombe cha Farao kilikuwa mkononi mwangu, nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe cha Farao, nikampa Farao kikombe mkononi mwake. Yusufu akamwambia, Tafsiri yake ndiyo hii. Matawi matatu ni siku tatu. Baada ya siku tatu Farao atakiinua kichwa chako, atakurudisha katika kazi yako; nawe utampa Farao kikombe mkononi mwake, kama desturi ya kwanza, ulipokuwa mnyweshaji wake. Ila unikumbuke mimi, utakapopata mema, ukanifanyie fadhili, nakuomba, ukanitaje kwa Farao, na kunitoa katika nyumba hii. Kwa sababu hakika naliibiwa kutoka nchi ya Waebrania, wala hapa sikutenda neno lo lote hata wanitie gerezani.
Mwanzo 40:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati fulani baada ya mambo hayo, maofisa wawili wa mfalme wa Misri walimkosea mfalme. Maofisa hao walikuwa mtunza vinywaji mkuu na mwoka mikate mkuu wa mfalme. Farao aliwakasirikia hao maofisa wake wawili, akawafungia ndani ya ngome ya mkuu wa kikosi cha ulinzi, katika gereza, mahali alipofungwa Yosefu. Mkuu wa kikosi cha ulinzi akamteua Yosefu awatumikie. Nao wakawa kifungoni kwa muda fulani. Basi, usiku mmoja, yule mtunza vinywaji mkuu na yule mwoka mikate mkuu wa mfalme wa Misri, waliota ndoto humo gerezani, kila mmoja na ndoto yake tofauti. Yosefu alipokwenda kwao asubuhi na kuwaona, wote wawili walikuwa wenye wasiwasi. Basi, Yosefu akawauliza maofisa hao wa Farao waliokuwa kifungoni pamoja naye nyumbani mwa bwana wake, “Mbona leo mna nyuso za huzuni?” Wakamjibu, “Tuna huzuni kwa kuwa tumeota ndoto na hakuna awezaye kututafsiria ndoto zetu.” Yosefu akawaambia, “Je, kutafsiri ndoto si kazi ya Mungu? Basi, niambieni ndoto zenu.” Mtunza vinywaji mkuu wa mfalme akamsimulia Yosefu ndoto yake, akisema, “Katika ndoto yangu niliona mzabibu mbele yangu, nao ulikuwa na matawi matatu. Mara tu ulipoanza kuchipua majani, maua yake yalichanua na vishada vyake vikawa zabibu mbivu. Mkononi mwangu nilikuwa na kikombe cha Farao, basi, nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe hicho, nikampa Farao.” Yosefu akamwambia huyo mtumishi, “Tafsiri ya ndoto yako ni hii: Yale matawi matatu ni siku tatu. Baada ya siku tatu Farao atakunyanyua kutoka gerezani na kukurudisha tena katika cheo chako. Utaweza tena kumpa Farao kikombe mkononi kama ulivyokuwa unafanya hapo awali. Lakini tafadhali usinisahau wakati mambo yatakapokwendea vema; unifanyie fadhili na kunitaja mbele ya Farao, nipate kutoka humu gerezani. Maana mimi nilitoroshwa kutoka nchi ya Waebrania, na hapa Misri sijafanya chochote kinachostahili nitiwe gerezani.”
Mwanzo 40:1-15 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Baada ya muda, mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri, wakamkosea bwana wao, mfalme wa Misri. Farao akawakasirikia hawa maafisa wake wawili, mnyweshaji mkuu na mwokaji mkuu, akawaweka chini ya ulinzi katika nyumba ya mkuu wa kikosi cha ulinzi katika gereza lile lile alimofungwa Yosefu. Mkuu wa kikosi cha ulinzi akawakabidhi kwa Yosefu, naye akawahudumia. Walipokuwa wamekaa chini ya ulinzi kwa muda, kila mmoja wa hao wawili waliokuwa wamewekwa gerezani, yaani mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri, waliota ndoto usiku mmoja, na kila ndoto ilikuwa na maana yake tofauti. Yosefu alipowajia asubuhi yake, akawaona kwamba walikuwa na huzuni. Ndipo Yosefu akawauliza maafisa hao wa Farao waliokuwa chini ya ulinzi pamoja naye nyumbani mwa bwana wake, akasema, “Mbona nyuso zenu zimejaa huzuni leo?” Wakamjibu, “Sisi sote tuliota ndoto, lakini hapakuwa na mtu yeyote wa kuzifasiri.” Ndipo Yosefu akawaambia, “Je, kufasiri ndoto si kazi ya Mungu? Niambieni ndoto zenu.” Basi mkuu wa wanyweshaji akamweleza Yosefu ndoto yake. Akamwambia, “Katika ndoto yangu niliona mzabibu mbele yangu, nao mzabibu ulikuwa na matawi matatu. Mara tu ulipoanza kuchipua, maua yalichanua na vishada vyake vikawa zabibu zilizoiva. Kikombe cha Farao kilikuwa mkononi mwangu, nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe cha Farao, na nikaweka kikombe mkononi mwake.” Yosefu akamwambia, “Hii ndiyo maana yake: Matawi matatu ni siku tatu. Katika siku hizi tatu, Farao atakutoa gerezani na kukuweka tena kwenye nafasi yako, nawe utaweka kikombe cha Farao mikononi mwake, kama vile ulivyokuwa unafanya ulipokuwa mnyweshaji wake. Lakini wakati mambo yatakapokuwia mazuri, unikumbuke, unifanyie wema, useme mema juu yangu kwa Farao ili niondoke huku gerezani. Kwa maana nilichukuliwa kwa nguvu kutoka nchi ya Waebrania, na hata hapa nilipo sikufanya lolote linalostahili niwekwe gerezani.”