Mwanzo 32:1-21
Mwanzo 32:1-21 SRUV
Yakobo akashika njia yake na malaika wa Mungu wakakutana naye. Naye Yakobo alipowaona, alisema, Hili ni jeshi la Mungu. Akapaita mahali pale, Mahanaimu. Basi, Yakobo akapeleka wajumbe mbele yake kwenda kwa Esau nduguye mpaka nchi ya Seiri katika nyika ya Edomu. Akawaagiza akisema, Mwambieni hivi bwana wangu, Esau, Hivi ndivyo asemavyo mtumwa wako, Yakobo; Nimekaa ugenini kwa Labani, na kukawia huko hata sasa, nami nina ng'ombe, na punda, na kondoo, na watumwa, na vijakazi; nami nimepeleka watu nimpashe bwana wangu habari, nipate neema machoni pako. Wale wajumbe wakarudi kwa Yakobo wakisema, Tulifika kwa ndugu yako, Esau, naye anakuja kukulaki, na watu mia nne pamoja naye. Ndipo Yakobo akaogopa sana, na kufadhaika sana, akawagawanya watu waliokuwa pamoja naye, na kondoo, na ng'ombe, na ngamia, wawe makundi mawili. Akasema, Akija Esau kwa kundi la kwanza, akalipiga, kundi litakalosalia litaokoka. Yakobo akasema, Ee Mungu wa baba yangu Abrahamu, na Mungu wa baba yangu Isaka, BWANA, uliyeniambia, Rudi uende mpaka nchi yako, na kwa jamaa zako, nami nitakutendea mema; mimi sistahili hata kidogo hizo rehema zote na kweli yote uliyomfanyia mtumwa wako; maana nilivuka mto huo wa Yordani na fimbo yangu tu, na sasa nimekuwa makundi mawili. Uniokoe sasa kutoka kwa mkono wa ndugu yangu, mkono wa Esau, maana mimi ninamwogopa, asije akaniua, na kina mama pamoja na watoto. Nawe ulisema, Hakika nitakutendea mema, nami nitafanya uzao wako uwe kama mchanga wa bahari, usiohesabika kwa kuwa mwingi. Akakaa huko usiku ule. Kisha akatwaa baadhi ya vitu alivyokuwa navyo, kuwa zawadi kwa Esau, nduguye; mbuzi majike mia mbili, mbuzi dume ishirini, kondoo majike mia mbili, na kondoo dume ishirini; ngamia wanyonyeshao thelathini pamoja na wana wao, ng'ombe majike arubaini na mafahali kumi; punda wake ishirini na wana wao kumi. Akawatia mkononi mwa watumwa wake, kila kundi peke yake. Naye akawaambia watumwa wake, Vukeni mbele yangu, mkaache nafasi kati ya kundi na kundi. Akamwagiza yule wa kwanza akasema, Esau, ndugu yangu, akikukuta, na kukuuliza, akisema, Wewe ni wa nani? Unakwenda wapi? Tena ni wa nani hawa walio mbele yako? Basi, useme, Ni wa mtumwa wako, Yakobo, ni zawadi, aliyompelekea bwana wangu, Esau. Na tazama, yeye mwenyewe yuko nyuma yetu. Akamwagiza tena wa pili, na wa tatu, wote waliofuata makundi, akisema, Hivi ndivyo mtakavyomwambia Esau, akiwakuta. Tena semeni, Tazama, mtumwa wako, Yakobo, yuko nyuma yetu. Maana alisema, Nitamsuluhisha kwa zawadi inayonitangulia, baadaye nitamwona uso wake; huenda atanikubali uso wangu. Basi ile zawadi ikavuka mbele yake, naye mwenyewe akakaa usiku ule kambini.