Mwanzo 32:1-21
Mwanzo 32:1-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Yakobo aliendelea na safari yake. Basi, malaika wa Mungu wakakutana naye. Yakobo alipowaona, akasema, “Hili ni jeshi la Mungu!” Kwa hiyo akapaita mahali hapo Mahanaimu. Yakobo aliwatuma wajumbe wamtangulie kwenda kwa nduguye Esau, huko Seiri, katika nchi ya Edomu. Aliwapa maagizo haya, “Mtamwambia bwana wangu Esau hivi: Mtumishi wako Yakobo asema hivi, ‘Nimekaa ugenini kwa Labani mpaka sasa. Nina ng'ombe, punda, makundi ya kondoo na watumishi wa kiume na wa kike. Ninakutumia ujumbe huu, bwana wangu, ili nipate fadhili mbele yako.’” Hao wajumbe walikwenda, kisha wakarudi na kumwambia Yakobo, “Tumefika kwa ndugu yako Esau, naye yuko njiani kuja kukulaki, akiwa na watu 400.” Basi, Yakobo akaogopa sana na kufadhaika. Akawagawa katika makundi mawili watu waliokuwa pamoja naye, kondoo, mifugo mingine na ngamia, akifikiri, “Kama Esau akija na kuliangamiza kundi moja, basi, kundi litakalosalia litaponyoka.” Kisha Yakobo akamwomba Mungu akisema, “Ee Mungu wa babu yangu Abrahamu, Mungu wa baba yangu Isaka! Ewe Mwenyezi-Mungu uliyeniambia nirudi katika nchi yangu kwa jamaa yangu, ukaniahidi kunitendea mema, sistahili hata kidogo fadhili ulizonipa kwa uaminifu mimi mtumishi wako. Nilipovuka mto Yordani, sikuwa na kitu ila fimbo; lakini sasa ninayo makundi haya mawili. Nakuomba uniokoe sasa kutoka kwa ndugu yangu Esau, maana nina hofu kuwa atatushambulia na kutuua sote, akina mama pamoja na watoto. Wewe uliniahidi kunitendea mema na kuwafanya wazawa wangu wawe wengi kama mchanga wa bahari ambao hauhesabiki kwa wingi wake.” Basi, Yakobo akalala hapo usiku huo. Kisha akatenga sehemu ya mali yake, iwe zawadi kwa ndugu yake Esau: Mbuzi majike 200 na mabeberu 20, kondoo majike 200 na madume 20, ngamia 30 wanyonyeshao pamoja na ndama wao, ng'ombe majike 40 na mafahali kumi, na punda majike 20 na madume kumi. Akawakabidhi watumishi wake, kila mmoja kundi lake, akawaambia, “Nitangulieni mkiacha nafasi kati ya kundi na kundi katika msafara wenu.” Akamwagiza yule aliyetangulia, “Ndugu yangu Esau atakapokutana nawe na kukuuliza, ‘Wewe ni mtumishi wa nani? Unakwenda wapi? Na wanyama hawa ni wa nani?’ Wewe utamjibu, ‘Hii ni mali ya mtumishi wako Yakobo, nayo ni zawadi yako wewe bwana wangu Esau. Tena Yakobo mwenyewe yuko nyuma anafuata.’” Akatoa agizo hilohilo kwa mtumishi wa kundi la pili na la tatu na wengine wote, akisema, “Mtamwambia Esau maneno hayohayo mtakapokutana naye. Zaidi ya yote, mtamwambia, ‘Mtumishi wako Yakobo yuko nyuma, anafuata.’” Yakobo alifanya hivyo akifikiri, “Pengine nitamtuliza kwa zawadi hizi ninazomtangulizia, na baadaye naweza kuonana naye ana kwa ana; huenda atanipokea.” Basi, akatanguliza zawadi zake, lakini yeye mwenyewe akalala kambini usiku huo.
Mwanzo 32:1-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yakobo akashika njia yake na malaika wa Mungu wakakutana naye. Naye Yakobo alipowaona, alisema, Hili ni jeshi la Mungu. Akapaita mahali pale, Mahanaimu. Basi, Yakobo akapeleka wajumbe mbele yake kwenda kwa Esau nduguye mpaka nchi ya Seiri katika nyika ya Edomu. Akawaagiza akisema, Mwambieni hivi bwana wangu, Esau, Hivi ndivyo asemavyo mtumwa wako, Yakobo; Nimekaa ugenini kwa Labani, na kukawia huko hata sasa, nami nina ng'ombe, na punda, na kondoo, na watumwa, na vijakazi; nami nimepeleka watu nimpashe bwana wangu habari, nipate neema machoni pako. Wale wajumbe wakarudi kwa Yakobo wakisema, Tulifika kwa ndugu yako, Esau, naye anakuja kukulaki, na watu mia nne pamoja naye. Ndipo Yakobo akaogopa sana, na kufadhaika sana, akawagawanya watu waliokuwa pamoja naye, na kondoo, na ng'ombe, na ngamia, wawe makundi mawili. Akasema, Akija Esau kwa kundi la kwanza, akalipiga, kundi litakalosalia litaokoka. Yakobo akasema, Ee Mungu wa baba yangu Abrahamu, na Mungu wa baba yangu Isaka, BWANA, uliyeniambia, Rudi uende mpaka nchi yako, na kwa jamaa zako, nami nitakutendea mema; mimi sistahili hata kidogo hizo rehema zote na kweli yote uliyomfanyia mtumwa wako; maana nilivuka mto huo wa Yordani na fimbo yangu tu, na sasa nimekuwa makundi mawili. Uniokoe sasa kutoka kwa mkono wa ndugu yangu, mkono wa Esau, maana mimi ninamwogopa, asije akaniua, na kina mama pamoja na watoto. Nawe ulisema, Hakika nitakutendea mema, nami nitafanya uzao wako uwe kama mchanga wa bahari, usiohesabika kwa kuwa mwingi. Akakaa huko usiku ule. Kisha akatwaa baadhi ya vitu alivyokuwa navyo, kuwa zawadi kwa Esau, nduguye; mbuzi majike mia mbili, mbuzi dume ishirini, kondoo majike mia mbili, na kondoo dume ishirini; ngamia wanyonyeshao thelathini pamoja na wana wao, ng'ombe majike arubaini na mafahali kumi; punda wake ishirini na wana wao kumi. Akawatia mkononi mwa watumwa wake, kila kundi peke yake. Naye akawaambia watumwa wake, Vukeni mbele yangu, mkaache nafasi kati ya kundi na kundi. Akamwagiza yule wa kwanza akasema, Esau, ndugu yangu, akikukuta, na kukuuliza, akisema, Wewe ni wa nani? Unakwenda wapi? Tena ni wa nani hawa walio mbele yako? Basi, useme, Ni wa mtumwa wako, Yakobo, ni zawadi, aliyompelekea bwana wangu, Esau. Na tazama, yeye mwenyewe yuko nyuma yetu. Akamwagiza tena wa pili, na wa tatu, wote waliofuata makundi, akisema, Hivi ndivyo mtakavyomwambia Esau, akiwakuta. Tena semeni, Tazama, mtumwa wako, Yakobo, yuko nyuma yetu. Maana alisema, Nitamsuluhisha kwa zawadi inayonitangulia, baadaye nitamwona uso wake; huenda atanikubali uso wangu. Basi ile zawadi ikavuka mbele yake, naye mwenyewe akakaa usiku ule kambini.
Mwanzo 32:1-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yakobo akashika njia yake na malaika wa Mungu wakakutana naye. Naye Yakobo alipowaona, alisema, Hili ni jeshi la Mungu. Akapaita mahali pale, Mahanaimu. Basi, Yakobo akapeleka wajumbe mbele yake kwenda kwa Esau nduguye mpaka nchi ya Seiri katika nyika ya Edomu. Akawaagiza akisema, Mwambieni hivi bwana wangu, Esau, Hivi ndivyo asemavyo mtumwa wako, Yakobo; Nimekaa ugenini kwa Labani, na kukawia huko hata sasa, nami nina ng’ombe, na punda, na kondoo, na watumwa, na vijakazi; nami nimepeleka watu nimpashe bwana wangu habari, nipate neema machoni pako. Wale wajumbe wakarudi kwa Yakobo wakisema, Tulifika kwa ndugu yako, Esau, naye anakuja kukulaki, na watu mia nne pamoja naye. Ndipo Yakobo akaogopa sana, na kufadhaika sana, akawagawanya watu waliopo pamoja naye, na kondoo, na ng’ombe, na ngamia, wawe matuo mawili. Akasema, Akija Esau kwa kundi la kwanza, akalipiga, kundi litakalosalia litaokoka. Yakobo akasema, Ee Mungu wa baba yangu Ibrahimu, na Mungu wa baba yangu Isaka, BWANA, uliyeniambia, Rudi uende mpaka nchi yako, na kwa jamaa zako, nami nitakutendea mema; mimi sistahili hata kidogo hizo rehema zote na kweli yote uliyomfanyia mtumwa wako; maana nalivuka mto huo wa Yordani na fimbo yangu tu, na sasa nimekuwa matuo mawili. Uniokoe sasa na mkono wa ndugu yangu, mkono wa Esau, maana mimi namwogopa, asije akanipiga, na mama pamoja na wana. Nawe ulisema, Hakika nitakutendea mema, nami nitafanya uzao wako uwe kama mchanga wa bahari, usiohesabika kwa kuwa mwingi. Akakaa huko usiku ule. Kisha akatwaa baadhi ya vitu alivyokuwa navyo, kuwa zawadi kwa Esau, nduguye; mbuzi wake mia mbili, na mbuzi waume ishirini, kondoo wake mia mbili, na kondoo waume ishirini; ngamia wanyonyeshao thelathini pamoja na wana wao, ng’ombe wake arobaini na mafahali kumi; punda wake ishirini na wana wao kumi. Akawatia mkononi mwa watumwa wake, kila kundi peke yake. Naye akawaambia watumwa wake, Vukeni mbele yangu, mkaache nafasi kati ya kundi na kundi. Akamwagiza yule wa kwanza akasema, Esau, ndugu yangu, akikukuta, na kukuuliza, akisema, Wewe u wa nani? Unakwenda wapi? Tena ni wa nani hawa walio mbele yako? Basi, useme, Ni wa mtumwa wako, Yakobo, ni zawadi, aliyompelekea bwana wangu, Esau. Na tazama, yeye mwenyewe yuko nyuma yetu. Akamwagiza tena wa pili, na wa tatu, wote waliofuata makundi, akisema, Hivi ndivyo mtakavyomwambia Esau, akiwakuta. Tena semeni, Tazama, mtumwa wako, Yakobo, yuko nyuma yetu. Maana alisema, Nitamsuluhisha kwa zawadi inayonitangulia, baadaye nitamwona uso wake; huenda atanikubali uso wangu. Basi ile zawadi ikavuka mbele yake, naye mwenyewe akakaa usiku ule kambini.
Mwanzo 32:1-21 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Yakobo pia akaondoka akaenda zake, nao malaika wa Mungu wakakutana naye. Yakobo alipowaona, akasema, “Hii ni kambi ya Mungu!” Kwa hiyo akapaita mahali pale Mahanaimu. Yakobo akatuma wajumbe kumtangulia kwa Esau ndugu yake huko Seiri, katika nchi ya Edomu. Akawaagiza, akisema: “Hili ndilo mtakalomwambia bwana wangu Esau: ‘Mtumishi wako Yakobo anasema: nimekuwa nikiishi pamoja na Labani na nimekuwa huko hadi sasa. Ninao ng’ombe na punda, kondoo na mbuzi, watumishi wa kiume na wa kike. Sasa ninatuma ujumbe huu kwa bwana wangu, ili nipate kibali machoni pako.’ ” Wajumbe waliporudi kwa Yakobo, wakamwambia, “Tulienda kuonana na ndugu yako Esau, naye sasa anakuja kukulaki akifuatana na wanaume mia nne.” Kwa hofu kuu na huzuni, Yakobo akagawanya watu aliokuwa nao katika makundi mawili; pia akagawanya makundi ya kondoo na mbuzi, na vilevile ng’ombe na ngamia. Yakobo alifikiri, “Kama Esau akija na kushambulia kundi moja, kundi lililobaki litanusurika.” Ndipo Yakobo akaomba, “Ee Mungu wa baba yangu Ibrahimu, Mungu wa baba yangu Isaka, Ee Mwenyezi Mungu, ndiwe uliniambia, ‘Rudi katika nchi yako na jamaa yako, nami nitakufanya ustawi.’ Sistahili fadhili na uaminifu wako wote ulionitendea mimi, mtumishi wako. Nilikuwa na fimbo tu mkononi mwangu nilipovuka mto huu wa Yordani, lakini sasa nimekuwa makundi mawili. Nakuomba uniokoe kutoka kwa mkono wa ndugu yangu Esau, kwa maana ninaogopa kuwa atakuja kunishambulia, pia kina mama pamoja na watoto wao. Lakini umeshasema, ‘Hakika nitakufanya ustawi na kuufanya uzao wako kuwa mwingi kama mchanga wa baharini ambao hauwezi kuhesabika!’ ” Akalala pale usiku ule. Miongoni mwa vitu alivyokuwa navyo, akachagua zawadi kwa ajili ya Esau ndugu yake: beberu ishirini na mbuzi jike mia mbili, kondoo dume ishirini na kondoo jike mia mbili, ngamia jike thelathini pamoja na ndama zao, ng’ombe arobaini na mafahali kumi, punda jike ishirini, na punda wa kiume kumi. Akaviweka chini ya uangalizi wa watumishi wake, kila kundi peke yake, na kuwaambia, “Nitangulieni na kuacha nafasi kati ya makundi.” Akamwagiza yule aliyetangulia hivi, “Ndugu yangu Esau atakapokutana nawe na kukuuliza, ‘Wewe ni wa nani? Unaenda wapi? Wanyama hawa wote mbele yako ni mali ya nani?’ utamjibu hivi, ‘Ni mali ya mtumishi wako Yakobo. Ni zawadi iliyotumwa kwa bwana wangu Esau, naye anakuja nyuma yetu.’ ” Akamwagiza pia yule mtumishi wa kundi la pili, na wa kundi la tatu, na kila mtumishi wa yale mengine yaliyofuata, hivi: “Mtamwambia Esau maneno hayo hayo mtakapokutana naye. Hakikisheni mmesema, ‘Mtumishi wako Yakobo anakuja nyuma yetu.’ ” Kwa kuwa alifikiri, “Nitaweza kumtuliza kwa zawadi hizi ninazotanguliza; hatimaye nitakapomwona, huenda atanikubali.” Kwa hiyo zawadi za Yakobo zilitangulia mbele yake, lakini yeye mwenyewe alilala kambini usiku ule.