Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 22:2-18

Mwanzo 22:2-18 SRUV

Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia. Abrahamu akaondoka alfajiri, akatandika punda wake, akachukua vijana wawili pamoja naye, na Isaka mwanawe, akachanja kuni kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka, akaenda mpaka mahali alipoambiwa na Mungu. Siku ya tatu Abrahamu akainua macho yake, akapaona mahali pakiwa bado ni mbali. Abrahamu akawaambia vijana wake, Kaeni ninyi hapa pamoja na punda, na mimi na kijana tutakwenda kule, tukaabudu, na kuwarudia tena. Basi Abrahamu akazitwaa kuni za hiyo sadaka, akamtwika Isaka mwanawe; akatwaa moto na kisu mkononi mwake, wakaenda wote wawili pamoja. Isaka akasema na Abrahamu baba yake, akinena, Babangu! Naye akasema, Mimi hapa, mwanangu. Akasema, Tazama! Moto upo, na kuni zipo, lakini yuko wapi mwana-kondoo kwa sadaka ya kuteketezwa? Abrahamu akasema, Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka, mwanangu. Basi wakaendelea wote wawili pamoja. Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Abrahamu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni. Abrahamu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe. Ndipo malaika wa BWANA akamwita kutoka mbinguni, akasema, Abrahamu! Abrahamu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, kwa kuwa hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee. Abrahamu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo dume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Abrahamu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe. Abrahamu akapaita mahali hapo Yehova-yire, kama watu wasemavyo hata leo, Katika mlima wa BWANA itapatikana. Malaika wa BWANA akamwita Abrahamu mara ya pili kutoka mbinguni akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki lango la adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.

Soma Mwanzo 22

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mwanzo 22:2-18