Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezra 1:1-11

Ezra 1:1-11 SRUV

Ikawa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, ili kwamba neno la BWANA alilolisema kwa kinywa cha Yeremia lipate kutimizwa, BWANA akaamsha roho yake Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata akapiga mbiu katika ufalme wake wote, akaiandika pia, akisema, Koreshi, mfalme wa Uajemi asema hivi; BWANA, Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote za dunia; naye ameniagiza nimjengee nyumba katika Yerusalemu, ulioko Yuda. Basi kila mtu katika ninyi nyote mlio watu wake, BWANA, Mungu wake, na awe pamoja naye, na akwee mpaka Yerusalemu, ulioko Yuda, akaijenge nyumba ya BWANA, Mungu wa Israeli, (yeye ndiye Mungu), iliyoko Yerusalemu. Na mtu yeyote aliyesalia mahali popote akaapo kama mgeni, na asaidiwe na watu wa mahali pake, kwa fedha, na dhahabu, na mali, na wanyama, zaidi ya vitu vitolewavyo kwa hiari ya mtu, kwa ajili ya nyumba ya Mungu, iliyoko Yerusalemu. Ndipo wakaondoka wakuu wa koo za mababa, wa Yuda na Benyamini, na makuhani, na Walawi, naam, watu wote ambao Mungu ameamsha roho zao kukwea, ili kuijenga nyumba ya BWANA, iliyoko Yerusalemu. Na watu wote waliokaa karibu nao pande zote wakawatia nguvu mikono yao, kwa vyombo vya fedha, kwa dhahabu, kwa mali, na kwa wanyama, na vitu vya thamani, zaidi ya vile vilivyotolewa kwa hiari ya mtu. Tena Koreshi, mfalme, alivitoa vyombo vya nyumba ya BWANA, alivyokuwa amevileta Nebukadneza toka Yerusalemu, na kuvitia katika nyumba ya miungu yake. Naam, vyombo vile ndivyo alivyovitoa Koreshi, mfalme wa Uajemi, kwa mkono wa Mithredathi, mtunza hazina; naye akavihesabu mbele ya Sheshbaza, mkuu wa Yuda. Na hii ndiyo hesabu yake; sinia za dhahabu thelathini, sinia za fedha elfu moja, visu ishirini na tisa; mabakuli ya dhahabu thelathini, mabakuli ya fedha ya namna ya pili mia nne na kumi, na vyombo vingine elfu moja. Vyombo vyote vya dhahabu na vya fedha vilikuwa jumla yake elfu tano na mia nne. Hivyo vyote Sheshbaza akakwea navyo, hapo walipokwea wale wa uhamisho kutoka Babeli mpaka Yerusalemu.

Soma Ezra 1

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha