Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezra 1:1-11

Ezra 1:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

Mnamo mwaka wa kwanza wa utawala wa Koreshi, mfalme wa Persia, ili neno la Mwenyezi-Mungu alilolinena kwa njia ya nabii Yeremia litimie, Mwenyezi-Mungu alimfanya Koreshi, mfalme wa Persia, atangaze amri ifuatayo katika ufalme wake na kuiweka katika maandishi: “Hivi ndivyo anavyosema Koreshi mfalme wa Persia: Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu, amenipatia falme zote za ulimwenguni na ameniagiza nimjengee nyumba Yerusalemu, huko Yuda. Basi sasa, kila mtu katika nyinyi nyote mlio watu wake, Mungu wake awe naye na aende Yerusalemu huko Yuda, na kuijenga upya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, Mungu anayeabudiwa huko Yerusalemu. Kila mmoja aliyebaki hai uhamishoni akitaka kurudi, jirani zake na wamsaidie kwa kumpa fedha, dhahabu, mali na wanyama, pamoja na matoleo ya hiari kwa ajili ya nyumba ya Mungu huko Yerusalemu.” Basi, wakaondoka viongozi wa koo za makabila ya Yuda na Benyamini, makuhani na Walawi, na kila mtu ambaye Mungu alimpa moyo wa kwenda kujenga upya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, iliyoko Yerusalemu. Majirani waliwasaidia watu hao kwa kuwapa vyombo vya fedha, dhahabu, mali, wanyama na vitu vingine vya thamani, mbali na vile vilivyotolewa kwa hiari. Mfalme Koreshi aliwarudishia vyombo ambavyo mfalme Nebukadneza alikuwa amevichukua kutoka katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kuviweka katika nyumba ya miungu yake. Alimkabidhi Mithredathi, mtunza hazina, vyombo hivyo, naye akamhesabia Sheshbaza, mtawala wa Yuda. Ifuatayo ndiyo hesabu yake: Bakuli 30 za dhahabu; bakuli 1,000 za fedha; vyetezo 29; bakuli ndogo za dhahabu 30; bakuli ndogo za fedha 410; vyombo vinginevyo 1,000. Vyombo vyote vya dhahabu na fedha, pamoja na vitu vinginevyo vilikuwa jumla yake 5,400. Vyote hivi, Sheshbaza alivichukua hadi Yerusalemu wakati yeye pamoja na watu wengine alipotolewa uhamishoni Babuloni kwenda Yerusalemu.

Shirikisha
Soma Ezra 1

Ezra 1:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, ili kwamba neno la BWANA alilolisema kwa kinywa cha Yeremia lipate kutimizwa, BWANA akaamsha roho yake Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata akapiga mbiu katika ufalme wake wote, akaiandika pia, akisema, Koreshi, mfalme wa Uajemi asema hivi; BWANA, Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote za dunia; naye ameniagiza nimjengee nyumba katika Yerusalemu, ulioko Yuda. Basi kila mtu katika ninyi nyote mlio watu wake, BWANA, Mungu wake, na awe pamoja naye, na akwee mpaka Yerusalemu, ulioko Yuda, akaijenge nyumba ya BWANA, Mungu wa Israeli, (yeye ndiye Mungu), iliyoko Yerusalemu. Na mtu yeyote aliyesalia mahali popote akaapo kama mgeni, na asaidiwe na watu wa mahali pake, kwa fedha, na dhahabu, na mali, na wanyama, zaidi ya vitu vitolewavyo kwa hiari ya mtu, kwa ajili ya nyumba ya Mungu, iliyoko Yerusalemu. Ndipo wakaondoka wakuu wa koo za mababa, wa Yuda na Benyamini, na makuhani, na Walawi, naam, watu wote ambao Mungu ameamsha roho zao kukwea, ili kuijenga nyumba ya BWANA, iliyoko Yerusalemu. Na watu wote waliokaa karibu nao pande zote wakawatia nguvu mikono yao, kwa vyombo vya fedha, kwa dhahabu, kwa mali, na kwa wanyama, na vitu vya thamani, zaidi ya vile vilivyotolewa kwa hiari ya mtu. Tena Koreshi, mfalme, alivitoa vyombo vya nyumba ya BWANA, alivyokuwa amevileta Nebukadneza toka Yerusalemu, na kuvitia katika nyumba ya miungu yake. Naam, vyombo vile ndivyo alivyovitoa Koreshi, mfalme wa Uajemi, kwa mkono wa Mithredathi, mtunza hazina; naye akavihesabu mbele ya Sheshbaza, mkuu wa Yuda. Na hii ndiyo hesabu yake; sinia za dhahabu thelathini, sinia za fedha elfu moja, visu ishirini na tisa; mabakuli ya dhahabu thelathini, mabakuli ya fedha ya namna ya pili mia nne na kumi, na vyombo vingine elfu moja. Vyombo vyote vya dhahabu na vya fedha vilikuwa jumla yake elfu tano na mia nne. Hivyo vyote Sheshbaza akakwea navyo, hapo walipokwea wale wa uhamisho kutoka Babeli mpaka Yerusalemu.

Shirikisha
Soma Ezra 1

Ezra 1:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, ili kwamba neno la BWANA alilolisema kwa kinywa cha Yeremia lipate kutimizwa, BWANA akamwamsha roho yake Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata akapiga mbiu katika ufalme wake wote, akaiandika pia, akisema, Koreshi, mfalme wa Uajemi asema hivi; BWANA, Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote za dunia; naye ameniagiza nimjengee nyumba katika Yerusalemu, ulioko Yuda. Basi kila mtu katika ninyi nyote mlio watu wake, BWANA, Mungu wake, na awe pamoja naye, na akwee mpaka Yerusalemu, ulioko Yuda, akaijenge nyumba ya BWANA, Mungu wa Israeli, (yeye ndiye Mungu), iliyoko Yerusalemu. Na mtu awaye yote aliyesalia mahali po pote akaapo hali ya ugeni, na asaidiwe na watu wa mahali pake, kwa fedha, na dhahabu, na mali, na wanyama, zaidi ya vitu vitolewavyo kwa hiari ya mtu, kwa ajili ya nyumba ya Mungu, iliyoko Yerusalemu. Ndipo wakaondoka wakuu wa mbari za mababa, wa Yuda na Benyamini, na makuhani, na Walawi, naam, watu wote ambao Mungu amewaamsha roho zao kukwea, ili kuijenga nyumba ya BWANA, iliyoko Yerusalemu. Na watu wote waliokaa karibu nao pande zote wakawatia nguvu mikono yao, kwa vyombo vya fedha, kwa dhahabu, kwa mali, na kwa wanyama, na vitu vya thamani, zaidi ya vile vilivyotolewa kwa hiari ya mtu. Tena Koreshi, mfalme, alivitoa vyombo vya nyumba ya BWANA, alivyokuwa amevileta Nebukadreza toka Yerusalemu, na kuvitia katika nyumba ya miungu yake. Naam, vyombo vile ndivyo alivyovitoa Koreshi, mfalme wa Uajemi, kwa mkono wa Mithredathi, mtunza hazina; naye akavihesabu mbele ya Sheshbaza, mkuu wa Yuda. Na hii ndiyo hesabu yake; sinia za dhahabu thelathini, sinia za fedha elfu, visu ishirini na kenda; mabakuli ya dhahabu thelathini, mabakuli ya fedha ya namna ya pili mia nne na kumi, na vyombo vingine elfu. Vyombo vyote vya dhahabu na vya fedha vilikuwa jumla yake elfu tano na mia nne. Hivyo vyote Sheshbaza akakwea navyo, hapo walipokwea wale wa uhamisho kutoka Babeli mpaka Yerusalemu.

Shirikisha
Soma Ezra 1

Ezra 1:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Koreshi mfalme wa Uajemi, ili kulitimiza neno la BWANA lililosemwa na nabii Yeremia, BWANA aliusukuma moyo wa Koreshi mfalme wa Uajemi kutangaza katika himaya yake yote kwa maandishi: “Hili ndilo asemalo Koreshi mfalme wa Uajemi: “ ‘BWANA, Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote duniani, na ameniagiza kumjengea Hekalu huko Yerusalemu katika Yuda. Yeyote wa watu wake miongoni mwenu, Mungu wake na awe pamoja naye, wacha apande kwenda Yerusalemu katika Yuda na kujenga Hekalu la BWANA, Mungu wa Israeli, Mungu aliyeko huko Yerusalemu. Nao watu wa mahali popote wale walionusurika wanapoishi sasa, watu hao wampe fedha na dhahabu, pamoja na vifaa na mifugo, mbali na sadaka za hiari kwa ajili ya Hekalu la Mungu huko Yerusalemu.’ ” Kisha viongozi wa jamaa ya Yuda na Benyamini na makuhani na Walawi kila mmoja ambaye moyo wake ulisukumwa na Mungu, akajiandaa kupanda ili kuijenga nyumba ya BWANA huko Yerusalemu. Majirani zao wote wakawasaidia vyombo vya fedha na dhahabu, pamoja na vifaa na mifugo, pia na zawadi za thamani, pamoja na sadaka zote za hiari. Zaidi ya hayo, Mfalme Koreshi akavitoa vyombo vilivyokuwa mali ya Hekalu la BWANA, ambavyo Nebukadneza alikuwa amevichukua kutoka Yerusalemu na kuviweka katika hekalu la mungu wake. Koreshi mfalme wa Uajemi akavitoa kwa mkono wa Mithredathi mtunza hazina, aliyevihesabu mbele ya Sheshbaza mkuu wa Yuda. Hii ilikuwa ndio orodha ya vifaa: masinia ya dhahabu yalikuwa 30 masinia ya fedha yalikuwa 1,000 vyetezo vya fedha vilikuwa 29 mabakuli ya dhahabu yalikuwa 30 mabakuli ya fedha yanayofanana yalikuwa 410 vifaa vingine vilikuwa 1,000. Kwa ujumla, kulikuwa na vyombo 5,400 vya dhahabu na vya fedha. Sheshbaza akavileta hivi vyote wakati watu walipotoka uhamishoni Babeli kwenda Yerusalemu.

Shirikisha
Soma Ezra 1