Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 36:16-28

Ezekieli 36:16-28 SRUV

Tena, neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, nyumba ya Israeli walipokaa katika nchi yao wenyewe, waliitia uchafu kwa njia yao na kwa matendo yao. Njia yao mbele zangu ilikuwa kama uchafu wa mwanamke wakati wa kutengwa kwake. Kwa hiyo nilimwaga hasira yangu juu yao, kwa ajili ya damu waliyoimwaga juu ya nchi, na kwa sababu wameitia uchafu kwa vinyago vyao. Nikawatawanya katika mataifa, wakatapanyika katika nchi nyingi; kwa kadiri ya njia yao, na kwa kadiri ya matendo yao, niliwahukumu. Nao walipoyafikia mataifa yale waliyoyaendea, walilitia unajisi jina langu takatifu; kwa kuwa watu waliwanena, wakisema, Watu hawa ni watu wa BWANA, nao wametoka katika nchi yake. Lakini, niliwahurumia kwa ajili ya jina langu takatifu, ambalo nyumba ya Israeli walikuwa wamelitia unajisi katika mataifa walikoenda. Kwa hiyo; waambieni nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi, sitendi hili kwa ajili yenu, Ee nyumba ya Israeli, bali kwa ajili ya jina langu takatifu, mlilolitia unajisi katika mataifa mlikoenda. Nami nitalitakasa jina langu kuu, lililotiwa unajisi katika mataifa, mlilolitia unajisi kati yao; nao mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, asema Bwana MUNGU, nitakapotakaswa kati yenu mbele ya macho yao. Maana nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote, na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe. Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni kutoka kwa uchafu wenu wote, na kutoka kwa vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda. Nanyi mtakaa katika nchi ile niliyowapa baba zenu, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Ezekieli 36:16-28