Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 36

36
Baraka kwa Israeli
1Na wewe, mwanadamu, itabirie milima ya Israeli, useme, Enyi milima ya Israeli, lisikieni neno la BWANA. 2#Kum 32:13; Zab 78:69; Isa 58:14; Hab 3:19 Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu adui amesema juu yenu, Aha! Na, Mahali pa juu pa zamani pamekuwa petu tupamiliki; 3basi tabiri useme, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu, naam, kwa sababu wamewafanya ninyi kuwa ukiwa, na kuwameza pande zote, mpate kuwa milki kwa mabaki ya mataifa, nanyi mmesemwa kwa midomo yao waongeao, na kwa masingizio ya watu; 4#Zab 79:4 kwa sababu hiyo, enyi milima ya Israeli, lisikieni neno la Bwana MUNGU; Bwana MUNGU aiambia hivi hiyo milima na vilima, mito ya maji na mabonde, mahali palipoharibika na kuwa ukiwa, na miji iliyoachwa na watu, ambayo imekuwa mateka, na kuzomewa na mabaki ya mataifa, walio karibu pande zote; 5#Kum 4:24; Isa 66:15,16; Eze 38:19; 35:10; Zek 1:15 basi Bwana MUNGU asema hivi; Hakika kwa moto wa wivu wangu nimenena juu ya mabaki ya mataifa, na juu ya Edomu yote, waliojiandalia nchi yangu kuwa milki yao, kwa furaha ya mioyo yao yote, kwa ujeuri wa roho zao, wakatwaa nchi yangu kuwa milki yao, kwa sababu ya malisho yake, ili kuipora; 6#Zab 123:3,4; Eze 34:29 basi katika kutabiri habari za nchi ya Israeli, uiambie milima na vilima, mifereji ya maji na mabonde, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nimenena katika wivu wangu na hasira yangu, kwa sababu mmetukanwa na mataifa; 7#Eze 20:5 basi Bwana MUNGU asema hivi; Nimeinua mkono wangu, kusema, Hakika, mataifa walio karibu nanyi pande zote, nao watatukanwa. 8Lakini ninyi, enyi milima ya Israeli, mtachipuza matawi yenu na kuwapa watu wangu Israeli matunda yenu; maana wako karibu kuja. 9#Hos 2:21-23; Hag 2:19 Maana, tazama, mimi nasimama upande wenu, nami nitawaelekea, nanyi mtalimwa na kupandwa mbegu; 10#Isa 58:12; 61:4; Amo 9:14 nami nitaongeza watu juu yenu, nyumba yote ya Israeli, naam, yote pia; nayo miji itakaliwa na watu, na mahali palipoharibika patajengwa. 11#Yer 31:27; 33:12; Eze 35:9; Hos 2:20; Yoe 3:17; 1 Yoh 5:20 Nami nitaongeza juu yenu mwanadamu na mnyama, nao watazidi na kuzaa; nami nitawakalisha watu ndani yenu, kwa kadiri ya hali yenu ya kwanza, nami nitawatendea mema kuliko mema ya mianzo yenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA. 12#Oba 1:17; Yer 15:7 Naam, nitaleta watu watembee juu yenu, naam, watu wangu Israeli; nao watakumiliki, nawe utakuwa urithi wao, wala hutawaua watoto wao tena tangu leo. 13#Hes 13:32 Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa watu hukuambia, wewe nchi u mwenye kula watu, nawe umekuwa mwenye kuua watu wa taifa lako; 14basi hutakula watu tena, wala hatuna watoto wa taifa lako tena, asema Bwana MUNGU; 15#Isa 60:14; Eze 34:29; Sef 3:19,20 wala sitakuacha usikie matusi ya wasioamini, wala hutaaibishwa na watu tena; wala hutalikwaza taifa lako tena, asema Bwana MUNGU.
Israeli kufanywa upya
16Tena, neno la BWANA likanijia, kusema, 17#Yer 2:7; Law 15:19 Mwanadamu, nyumba ya Israeli walipokaa katika nchi yao wenyewe, waliitia uchafu kwa njia yao na kwa matendo yao. Njia yao mbele zangu ilikuwa kama uchafu wa mwanamke wakati wa kutengwa kwake. 18#Eze 16:36 Kwa hiyo nilimwaga hasira yangu juu yao, kwa ajili ya damu waliyoimwaga juu ya nchi, na kwa sababu wameitia uchafu kwa vinyago vyao. 19#Eze 22:15; 7:3 Nikawatawanya katika mataifa, wakatapanyika katika nchi nyingi; kwa kadiri ya njia yao, na kwa kadiri ya matendo yao, niliwahukumu. 20#Isa 52:5; Rum 2:24 Nao walipoyafikia mataifa yale waliyoyaendea, walilitia unajisi jina langu takatifu; kwa kuwa watu waliwanena, wakisema, Watu hawa ni watu wa BWANA, nao wametoka katika nchi yake. 21#Eze 20:9 Lakini, niliwahurumia kwa ajili ya jina langu takatifu, ambalo nyumba ya Israeli walikuwa wamelitia unajisi katika mataifa walikoenda. 22#Kum 9:5; Zab 106:8 Kwa hiyo; waambieni nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi, sitendi hili kwa ajili yenu, Ee nyumba ya Israeli, bali kwa ajili ya jina langu takatifu, mlilolitia unajisi katika mataifa mlikoenda. 23#Eze 20:41 Nami nitalitakasa jina langu kuu, lililotiwa unajisi katika mataifa, mlilolitia unajisi kati yao; nao mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, asema Bwana MUNGU, nitakapotakaswa kati yenu mbele ya macho yao. 24#Eze 34:13 Maana nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote, na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe. 25#Hes 19:13; Isa 52:15; Yer 33:8; 1 Yoh 1:7 Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni kutoka kwa uchafu wenu wote, na kutoka kwa vinyago vyenu vyote. 26#Zab 51:10; Yn 3:3-5; 2 Kor 3:18; Eze 11:19-20 Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. 27#Eze 37:14; Isa 44:3; Rum 8:4,9; Gal 5:5; Efe 1:13 Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda. 28#Eze 28:25; Yer 30:22 Nanyi mtakaa katika nchi ile niliyowapa baba zenu, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu. 29#Mt 1:21; Zab 105:16 Nami nitawaokoeni kutoka kwa uchafu wenu wote; nitaiamuru ngano iongezeke, wala sitawaletea njaa tena. 30#Eze 34:27 Nami nitazidisha matunda ya miti, na mazao ya mashamba, msipate tena kutukanwa na mataifa kwa sababu ya njaa. 31#Eze 6:9; Law 26:39 Ndipo mtazikumbuka njia zenu mbaya, na matendo yenu yasiyokuwa mema, nanyi mtajichukia nafsi zenu kwa macho yenu, kwa sababu ya maovu yenu na machukizo yenu. 32#Kum 9:5; Dan 9:19 Ijulikane kwenu ya kuwa silitendi neno hili kwa ajili yenu, asema Bwana MUNGU; tahayarikeni, na kufadhaika, kwa sababu ya njia zenu, Enyi nyumba ya Israeli. 33#Rum 8:30-32 Bwana MUNGU asema hivi; Siku ile nitakapowatakaseni kutoka kwa maovu yenu yote, nitaifanya miji ikaliwe na watu, na palipobomolewa pajengwe tena. 34#Yer 25:9 Nchi iliyokuwa ukiwa italimwa, ijapokuwa ilikuwa ukiwa mbele ya macho ya watu wote waliopita. 35#Isa 51:3; Mwa 2:8-9 Nao watasema, Nchi hii, iliyokuwa ukiwa, imekuwa kama bustani ya Adeni; nayo miji iliyokuwa mahame, na ukiwa, na magofu, sasa ina maboma, inakaliwa na watu. 36#Zab 58:11; Eze 17:24; 22:14 Ndipo mataifa, waliobaki karibu yenu pande zote, watajua ya kuwa mimi, BWANA, nimejenga mahali palipoharibika, nami nimepanda mbegu katika nchi iliyokuwa ukiwa; mimi, BWANA, nimesema hayo; tena nitayatenda.
37 # Zab 102:17; Isa 45:11,19; Yer 29:11-13; Eze 14:3; Zek 13:9; Mt 7:7,8; Flp 4:6; Yak 4:3 Bwana MUNGU asema hivi, Tena kwa ajili ya jambo hili nitaulizwa na nyumba ya Israeli, ili niwatendee; nami nitawaongeza kwa watu kama kundi la kondoo. 38Kama kundi lililo tayari kutolewa sadaka, kama kundi la Yerusalemu katika sikukuu zake zilizoamriwa; ndivyo itakavyojazwa watu, miji ile iliyokuwa maganjo; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.

Iliyochaguliwa sasa

Ezekieli 36: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha