Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 34:1-16

Ezekieli 34:1-16 SRUV

Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, toa unabii juu ya wachungaji wa Israeli, toa unabii, uwaambie, naam, hao wachungaji, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wachungaji wa Israeli, wanaojilisha wenyewe; je! Haiwapasi wachungaji kuwalisha kondoo? Mnawala walionona, mnajivika manyoya, mnawachinja walionona; lakini hamwalishi kondoo. Wagonjwa hamkuwatia nguvu, wala hamkuwaponya wenye maradhi, wala hamkuwafunga waliovunjika, wala hamkuwarudisha waliofukuzwa, wala hamkuwatafuta waliopotea; bali kwa nguvu na kwa ukali mmewatawala. Nao wakatawanyika, kwa sababu hapakuwa na mchungaji; wakawa chakula cha wanyamamwitu, wakatawanyika. Kondoo wangu walitangatanga katika milima yote, na juu ya kila kilima kirefu; naam, kondoo wangu walitawanyika juu ya uso wote wa dunia; wala hapakuwa na mtu aliyewaulizia, wala kuwatafuta. Basi, enyi wachungaji, lisikieni neno la BWANA; Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, kwa sababu kondoo wangu walikuwa mateka, kondoo wangu wakawa chakula cha wanyamamwitu wote, kwa sababu hapakuwa na mchungaji, wala wachungaji wangu hawakutafuta kondoo wangu, bali wachungaji walijilisha wenyewe wala hawakuwalisha kondoo wangu; kwa sababu hiyo, enyi wachungaji, lisikieni neno la BWANA; Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu ya wachungaji; nami nitawataka kondoo wangu mikononi mwao, nami nitawaachisha hiyo kazi ya kuwalisha kondoo; nao wachungaji hawatajilisha wenyewe tena; nami nitawaokoa kondoo wangu vinywani mwao, wasiwe tena chakula chao. Maana, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi mwenyewe, naam, mimi, nitawatafuta kondoo wangu, na kuwatunza. Kama vile mchungaji atafutavyo kondoo wake, siku ile anapokuwa kati ya kondoo wake waliotawanyika; ndivyo nitakavyowatafuta kondoo wangu; nami nitawaokoa katika mahali pote walipotawanyika, katika siku ya mawingu na giza. Nami nitawatoa katika watu wa mataifa, na kuwakusanya katika nchi zote, nami nitawarudisha katika nchi yao wenyewe; nami nitawalisha juu ya milima ya Israeli, kando ya mifereji ya maji; na katika mahali pote pa nchi panapokaliwa na watu. Nami nitawalisha malisho mema, pa juu ya milima ya mahali palipoinuka pa Israeli litakuwa zizi lao; huko watalala katika zizi jema; nao watakula malisho mema, juu ya milima ya Israeli. Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo wangu, nami nitawalaza, asema Bwana MUNGU. Nami nitawatafuta waliopotea, nitawarudisha waliotangatanga, nitawatibu waliojeruhiwa, nitawatia nguvu wagonjwa; nao wanono na wenye nguvu nitawaharibu; nitawalisha hukumu.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Ezekieli 34:1-16

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha