Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 34:1-16

Ezekieli 34:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)

Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Toa unabii dhidi ya wachungaji wa Israeli. Waambie hao wachungaji kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ole wenu nyinyi wachungaji wa Israeli, mnaojilisha nyinyi wenyewe tu! Je, haiwapasi wachungaji kuwalisha kondoo? Mnakunywa maziwa, mnavaa mavazi ya manyoya yao na kondoo wanono mnawachinja na kuwala. Lakini hamwalishi hao kondoo. Walio dhaifu hamkuwapatia nguvu, wagonjwa hamkuwaponya, waliojeruhiwa hamkuwafungia dawa, waliotangatanga hamkuwarudisha na waliopotea hamkuwatafuta. Lakini mmetumia mabavu na ukatili kuwatawala. Basi, kwa kuwa hao kondoo hawakuwa na mchungaji walitawanywa, wakawa mawindo ya wanyama wakali. Naam, kondoo wangu walitawanywa, wakatangatanga milimani na vilimani. Kondoo walisambazwa duniani kote, na hapakuwa na mtu aliyejali juu yao wala kuwatafuta. “Basi, sikieni vizuri neno langu mimi Mwenyezi-Mungu, enyi wachungaji: Kama niishivyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, naapa kwamba: Nimechoka kuwaona kondoo wangu wamekuwa mawindo ya wanyama wakali kwa vile hapakuwa na mchungaji; wachungaji wangu hawakuwatafuta kondoo wangu, bali wamejilisha wao wenyewe badala ya kuwalisha kondoo wangu. Basi, nyinyi wachungaji, sikieni neno langu mimi Mwenyezi-Mungu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitapambana nanyi, enyi wachungaji. Nitawaondolea madaraka ya kuchunga kondoo wangu, wala sitakubali muwachunge tena. Hamtakuwa tena na nafasi ya kujinufaisha wenyewe. Nitawaokoa kondoo wangu makuchani mwenu, ili wasiwe chakula chenu tena. “Basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi mwenyewe nitawatafuta kondoo wangu na kuwatunza. Kama mchungaji anavyowatafuta kondoo wake waliotawanyika, ndivyo nitakavyowatafuta kondoo wangu. Nitawarudisha kutoka kila mahali walipotawanyika siku yenye mawingu na giza nene. Nitawatoa kutoka kwa watu wa mataifa. Nitawakusanya kutoka nchi za mbali na kuwaleta katika nchi yao wenyewe. Nitawachunga juu ya milima ya Israeli, kando ya vijito na katika sehemu zote za nchi zinazokaliwa na watu. Nitawapa malisho mazuri kwenye milima mirefu ya Israeli ambako yako malisho yao. Watapumzika huko kwenye mbuga za malisho mazuri; naam, watapata malisho mazuri juu ya milima ya Israeli. Mimi mwenyewe nitakuwa mchungaji wa kondoo wangu. Mimi mwenyewe nitawapumzisha. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Kondoo waliopotea nitawatafuta na waliotangatanga nitawarudisha nyumbani. Waliojeruhiwa nitawatibu, na wale walio dhaifu nitawapa nguvu. Kondoo wanono na wenye nguvu nitawaangamiza. Mimi nitawachunga kondoo kama itakiwavyo.

Ezekieli 34:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, toa unabii juu ya wachungaji wa Israeli, toa unabii, uwaambie, naam, hao wachungaji, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wachungaji wa Israeli, wanaojilisha wenyewe; je! Haiwapasi wachungaji kuwalisha kondoo? Mnawala walionona, mnajivika manyoya, mnawachinja walionona; lakini hamwalishi kondoo. Wagonjwa hamkuwatia nguvu, wala hamkuwaponya wenye maradhi, wala hamkuwafunga waliovunjika, wala hamkuwarudisha waliofukuzwa, wala hamkuwatafuta waliopotea; bali kwa nguvu na kwa ukali mmewatawala. Nao wakatawanyika, kwa sababu hapakuwa na mchungaji; wakawa chakula cha wanyamamwitu, wakatawanyika. Kondoo wangu walitangatanga katika milima yote, na juu ya kila kilima kirefu; naam, kondoo wangu walitawanyika juu ya uso wote wa dunia; wala hapakuwa na mtu aliyewaulizia, wala kuwatafuta. Basi, enyi wachungaji, lisikieni neno la BWANA; Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, kwa sababu kondoo wangu walikuwa mateka, kondoo wangu wakawa chakula cha wanyamamwitu wote, kwa sababu hapakuwa na mchungaji, wala wachungaji wangu hawakutafuta kondoo wangu, bali wachungaji walijilisha wenyewe wala hawakuwalisha kondoo wangu; kwa sababu hiyo, enyi wachungaji, lisikieni neno la BWANA; Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu ya wachungaji; nami nitawataka kondoo wangu mikononi mwao, nami nitawaachisha hiyo kazi ya kuwalisha kondoo; nao wachungaji hawatajilisha wenyewe tena; nami nitawaokoa kondoo wangu vinywani mwao, wasiwe tena chakula chao. Maana, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi mwenyewe, naam, mimi, nitawatafuta kondoo wangu, na kuwatunza. Kama vile mchungaji atafutavyo kondoo wake, siku ile anapokuwa kati ya kondoo wake waliotawanyika; ndivyo nitakavyowatafuta kondoo wangu; nami nitawaokoa katika mahali pote walipotawanyika, katika siku ya mawingu na giza. Nami nitawatoa katika watu wa mataifa, na kuwakusanya katika nchi zote, nami nitawarudisha katika nchi yao wenyewe; nami nitawalisha juu ya milima ya Israeli, kando ya mifereji ya maji; na katika mahali pote pa nchi panapokaliwa na watu. Nami nitawalisha malisho mema, pa juu ya milima ya mahali palipoinuka pa Israeli litakuwa zizi lao; huko watalala katika zizi jema; nao watakula malisho mema, juu ya milima ya Israeli. Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo wangu, nami nitawalaza, asema Bwana MUNGU. Nami nitawatafuta waliopotea, nitawarudisha waliotangatanga, nitawatibu waliojeruhiwa, nitawatia nguvu wagonjwa; nao wanono na wenye nguvu nitawaharibu; nitawalisha hukumu.

Ezekieli 34:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, toa unabii juu ya wachungaji wa Israeli, toa unabii, uwaambie, naam, hao wachungaji, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wachungaji wa Israeli, wanaojilisha wenyewe; je! Haiwapasi wachungaji kuwalisha kondoo? Mnawala walionona, mnajivika manyoya, mnawachinja walionona; lakini hamwalishi kondoo. Wagonjwa hamkuwatia nguvu, wala hamkuwaponya wenye maradhi, wala hamkuwafunga waliovunjika, wala hamkuwarudisha waliofukuzwa, wala hamkuwatafuta waliopotea; bali kwa nguvu na kwa ukali mmewatawala. Nao wakatawanyika, kwa sababu hapakuwa na mchungaji; wakawa chakula cha wanyama-mwitu, wakatawanyika. Kondoo zangu walitanga-tanga katika milima yote, na juu ya kila kilima kirefu; naam, kondoo zangu walitawanyika juu ya uso wote wa dunia; wala hapakuwa na mtu aliyewaulizia, wala kuwatafuta. Basi, enyi wachungaji, lisikieni neno la BWANA; Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, kwa sababu kondoo zangu walikuwa mateka, kondoo zangu wakawa chakula cha wanyama-mwitu wote, kwa sababu hapakuwa na mchungaji, wala wachungaji wangu hawakutafuta kondoo zangu, bali wachungaji walijilisha wenyewe wala hawakuwalisha kondoo zangu; kwa sababu hiyo, enyi wachungaji, lisikieni neno la BWANA; Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu ya wachungaji; nami nitawataka kondoo zangu mikononi mwao, nami nitawaachisha hiyo kazi ya kuwalisha kondoo; nao wachungaji hawatajilisha wenyewe tena; nami nitawaokoa kondoo zangu vinywani mwao, wasiwe tena chakula chao. Maana, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi mwenyewe, naam, mimi, nitawatafuta kondoo zangu, na kuwaulizia. Kama vile mchungaji atafutavyo kondoo zake, siku ile anapokuwa kati ya kondoo zake waliotawanyika; ndivyo nitakavyowatafuta kondoo zangu; nami nitawaokoa katika mahali pote walipotawanyika, katika siku ya mawingu na giza. Nami nitawatoa katika watu wa mataifa, na kuwakusanya katika nchi zote, nami nitawarudisha katika nchi yao wenyewe; nami nitawalisha juu ya milima ya Israeli, kando ya mifereji ya maji; na katika mahali pote pa nchi panapokaliwa na watu. Nami nitawalisha malisho mema, pa juu ya milima ya mahali palipoinuka pa Israeli litakuwa zizi lao; huko watalala katika zizi jema; nao watakula malisho mema, juu ya milima ya Israeli. Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo zangu, nami nitawalaza, asema Bwana MUNGU. Nami nitawatafuta waliopotea, nitawarudisha waliofukuzwa, nitawafunga waliovunjika, nitawatia nguvu wagonjwa; nao wanono na wenye nguvu nitawaharibu; nitawalisha hukumu.

Ezekieli 34:1-16 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, tabiri juu ya wachungaji wa Israeli, tabiri na uwaambie: ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Ole wa wachungaji wa Israeli ambao hujitunza wenyewe tu! Je, haiwapasi wachungaji kutunza kundi la kondoo? Mnakula mafuta ya wanyama, mnavaa mavazi ya sufu na kuchinja kondoo walionona, lakini hamlitunzi kundi. Hamkuwatia nguvu walio dhaifu wala hamkuwaganga wenye maradhi wala kuwafunga waliojeruhiwa. Hamkuwarudisha waliotangatanga wala kuwatafuta wale waliopotea. Badala yake mmewatawala kwa ukali na kwa ukatili. Hivyo walitawanyika kwa sababu hapakuwepo mchungaji, nao walipotawanyika, wakawa chakula cha wanyama wa mwitu wote. Kondoo wangu walitawanyika, wakatangatanga kwenye milima yote na kwenye kila kilima kirefu. Kondoo wangu walitawanyika juu ya uso wa dunia yote bila kuwa na yeyote wa kuwaulizia wala wa kuwatafuta. “ ‘Kwa hiyo, ninyi wachungaji, lisikieni neno la BWANA: Kwa hakika kama niishivyo, asema BWANA Mwenyezi, kwa sababu kondoo zangu wamekosa mchungaji na hivyo wametekwa nyara na kuwa chakula cha wanyama wote wa mwituni na kwa sababu wachungaji wangu, hawakuwatafuta kondoo zangu, bali wachungaji wamejitunza wenyewe, nao hawakuwalisha kondoo zangu, kwa hiyo enyi wachungaji, sikieni neno la BWANA: Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Mimi ni kinyume na wachungaji nami nitawadai kondoo zangu mikononi mwao. Nitawafukuza kutoka kwenye kuchunga kundi langu, ili wachungaji wasiendelee kujitunza wenyewe. Nitaokoa kondoo zangu kutoka kwenye vinywa vyao, nao kondoo hawatakuwa tena chakula chao. “ ‘Kwa kuwa hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Mimi mwenyewe nitawaulizia kondoo wangu na kuwatafuta. Kama vile mchungaji atafutavyo kundi lake lililotawanyika wakati akiwa pamoja nalo, hivyo ndivyo nitakavyowatafuta kondoo wangu. Nitawaokoa kutoka mahali pote walipokuwa wametawanyikia katika siku ya mawingu na giza nene. Nitawatoa katika mataifa na kuwakusanya kutoka nchi mbalimbali, nami nitawaleta katika nchi yao wenyewe. Nitawalisha kwenye milima ya Israeli, katika mabonde na mahali pote panapokalika katika nchi. Nitawachunga kwenye malisho mazuri na miinuko ya mlima wa Israeli patakuwa mahali pao pa malisho. Huko watajipumzisha kwa amani katika nchi ya malisho mazuri, nao watajilisha huko katika malisho tele katika milima ya Israeli. Mimi mwenyewe nitawachunga kondoo zangu na kuwafanya wapumzike, asema BWANA Mwenyezi. Nitawaulizia kondoo waliopotea na kuwaleta waliotangatanga. Nitawafunga waliojeruhiwa na kuwatia nguvu walio dhaifu lakini wale waliojikinai na wenye nguvu nitawaangamiza. Nitalichunga kundi kwa haki.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha