Ezekieli 21:18-32
Ezekieli 21:18-32 SRUV
Neno la BWANA likanijia tena, kusema, Tena, mwanadamu, ujiwekee njia mbili, upanga wa mfalme wa Babeli upate kuja; hizo mbili zitatoka katika nchi moja; ukaandike mahali, upaandike penye kichwa cha njia iendayo mjini. Utachora njia, ili upanga upate kufikia Raba wa wana wa Amoni, na kufikia Yuda katika Yerusalemu, wenye maboma. Maana mfalme wa Babeli alisimama penye njia panda, penye kichwa cha njia hizo mbili, ili atumie uganga; aliitikisa mishale huku na huko, akaziuliza terafi, akayatazama maini. Katika mkono wake wa kulia alikuwa na kura ya Yerusalemu, kuviweka vyombo vya kubomolea, kufumbua kinywa katika machinjo, kuiinua sauti kwa kupiga kelele sana, kuweka vyombo vya kubomolea juu ya malango, kufanya maboma, na kujenga ngome. Jambo hili litakuwa kwao kama uganga wa ubatili, mbele ya macho yao waliowaapia viapo lakini ataufanya uovu ukumbukwe, ili kwamba wakamatwe. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa mmeufanya uovu wenu ukumbukwe, kwa maana makosa yenu yamefunuliwa, hata dhambi zenu zikaonekana kwa matendo yenu; kwa sababu mmekumbukwa, mtakamatwa kwa mkono. Na wewe, Ewe mtu mwovu, uliyetiwa jeraha kiasi cha kukuua, mkuu wa Israeli, ambaye siku yako imekuja, katika wakati wa uovu wa mwisho; Bwana MUNGU asema hivi; Kiondoe kilemba, livue taji; haya hayatakuwa tena kama yalivyo; kikweze kilicho chini, kakishushe kilichoinuka. Nitakipindua, nitakipindua, nitakipindua; hiki nacho hakitakuwa tena, hata atakapokuja yeye ambaye ni haki yake; nami nitampa. Nawe, mwanadamu, tabiri useme, Bwana MUNGU asema hivi, kuhusu wana wa Amoni, na kuhusu aibu yao; Nena, Upanga; upanga umefutwa; umeng'arishwa, ili kuua, ili kuufanya uue sana, upate kuwa kama umeme; wakati wanapokupa maono ya udanganyifu, wakati wanapokuagulia uongo, wanakuweka juu ya shingo zao wachukizao, na waovu, ambao siku yao imekuja, katika wakati wa adhabu ya mwisho. Uurudishe alani mwake. Mahali pale ulipoumbwa, katika nchi uliyozaliwa; nitakuhukumu wewe. Nami nitamwaga ghadhabu yangu juu yako; nitakupulizia moto wa hasira yangu; nami nitakutia katika mikono ya watu walio kama hayawani, wajuao sana kuangamiza. Utakuwa kuni za kutiwa motoni; damu yako itamwagika katikati ya nchi; hutakumbukwa tena; maana mimi, BWANA, nimenena neno hili.