Ezekieli 21:18-32
Ezekieli 21:18-32 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, weka alama njia mbili ambazo upanga wa mfalme wa Babeli utapitia, njia hizo zikianzia katika nchi hiyo hiyo. Weka kibao pale ambapo njia zinagawanyika kuelekea mjini. Weka alama njia moja kwa ajili ya upanga upate kuja dhidi ya Raba ya Waamoni na nyingine upate kuja dhidi ya Yuda na Yerusalemu iliyozungushiwa ngome. Kwa kuwa mfalme wa Babeli sasa amesimama katika njia panda, katika makutano ya njia mbili, akipiga ramli: anapiga kura kwa kutumia mishale, anataka shauri kwa sanamu zake, anachunguza maini ya wanyama. Upande wake wa kuume inakuja kura ya Yerusalemu, ambapo ataweka vyombo vya kuvunjia boma, ili kuamrisha mauaji, kupiga ukelele wa vita, kuweka vyombo vya kuvunjia boma kwenye malango, kuweka jeshi kuzunguka na kufanya uzingiraji. Itakuwa kama kupiga ramli kwa uongo kwa wale watu ambao wameapa kumtii yeye. Lakini mfalme wa Babeli atawakumbusha juu ya uovu wao na kuwachukua mateka. “Kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: ‘Kwa sababu enyi watu mmekumbusha uovu wenu kwa kuasi waziwazi, mkidhihirisha dhambi zenu katika yale yote mfanyayo, kwa kuwa mmefanya jambo hili, mtachukuliwa mateka. “ ‘Ee mtawala kafiri na mwovu wa Israeli, ambaye siku yako imewadia, ambaye wakati wako wa adhabu umefikia kilele chake, hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Vua kilemba, ondoa taji. Kwa kuwa mambo hayatakuwa kama yalivyokuwa. Aliye mnyonge atakwezwa na aliyekwezwa atashushwa. Mahame! Mahame! Nitaufanya mji kuwa mahame! Hautajengwa upya mpaka aje yule ambaye ndiye mwenye haki nao; yeye ndiye nitakayempa.’ “Nawe, mwanadamu, tabiri na useme, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo kuhusu Waamoni na matukano yao. “ ‘Upanga, upanga, umefutwa kwa ajili ya kuua, umesuguliwa ili kuangamiza na unametameta kama umeme wa radi! Wakati wakitoa maono ya uongo kwa ajili yako, wanapobashiri uongo kwa ajili yako, wanakuweka wewe kwenye shingo za watu wapotovu, wale walio waovu, wale ambao siku yao imewadia, wakati wa adhabu yao ya mwisho. Urudishe upanga kwenye ala yake! Katika mahali ulipoumbiwa, katika nchi ya baba zako, huko nitakuhukumu. Nitamwaga ghadhabu yangu juu yako na kupuliza moto wa hasira yangu dhidi yako; nitakutia mikononi mwa watu wakatili, watu stadi katika kuangamiza. Mtakuwa kuni za kuwashia moto, damu yenu itamwagwa katika nchi yenu, wala hamtakumbukwa tena; kwa maana Mimi BWANA nimesema.’ ”
Ezekieli 21:18-32 Biblia Habari Njema (BHN)
Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Chora njia mbili ambapo utapitia upanga wa mfalme wa Babuloni. Njia zote mbili zianzie katika nchi moja. Mwanzoni mwa kila njia utaweka alama ya kuonesha upande mji uliko. Utachora njia upanga utakapopitia kwenda kuufikilia mji wa Raba wa Waamoni, na njia nyingine inayoelekea mji wenye ngome wa Yerusalemu nchini Yuda. Mfalme wa Babuloni anasimama mwanzoni mwa hizo njia mbili, kwenye njia panda, apate kupiga bao. Anatikisa mishale, anaviuliza shauri vinyago vya miungu yake na kuchunguza maini ya mnyama. Mshale unaodokezea ‘Yerusalemu’ umeangukia mkono wake wa kulia. Anaweka zana za kubomolea, anaamuru mauaji na kelele za vita zifanywe, zana za kubomolea malango zimewekwa, maboma na minara ya kuuzingira mji vimewekwa. Lakini watu wa Yerusalemu wataudhania kuwa ni utabiri wa uongo kwa sababu wamekula kiapo rasmi. Hata hivyo unabii huu utawakumbusha uovu wao na kusababishwa kukamatwa kwao. Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wote wataweza kuziona dhambi zenu. Kila mtu atajua jinsi mlivyo na hatia. Kila kitendo mnachotenda kinaonesha dhambi zenu. Nyinyi mmehukumiwa adhabu nami nitawatia mikononi mwa maadui zenu. “Nawe mtawala wa Israeli wewe ni mpotovu kabisa. Siku yako imefika, naam, siku ya adhabu yako ya mwisho. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nakuambia hivi: Vua kilemba chako na taji yako kwani mambo hayatabaki kama yalivyokuwa. Walio chini watakwezwa, walio juu watashushwa! Uharibifu! Uharibifu! Hamna chochote katika mji huu nitakachosaza. Lakini kabla ya hayo atakuja yule ambaye nimempa mamlaka ya kuuadhibu, ambaye mimi nitampa mji huo. “Ewe mtu, tabiri kuhusu Waamoni na maneno yao ya dhihaka kwa Waisraeli: Waambie kuwa nasema: Upanga, upanga! Upanga umenyoshwa kuua, umenolewa uangamize, umengarishwa ungae kama umeme. Wakati nyinyi mmetulia katika maono yenu madanganyifu na utabiri wenu wa uongo, upanga utakuwa tayari kukata shingo za waasi na waovu. Siku imewadia ambapo maovu yenu yataadhibiwa. “Sasa rudisha upanga alani mwake! Nitawahukumu mahali palepale mlipoumbwa, katika nchi mlipozaliwa. Nitawamwagia ghadhabu yangu. Moto wa ghadhabu yangu nitaupuliza juu yenu. Nitawatia mikononi mwa watu wakatili, watu hodari wa kuangamiza. Mtakuwa kuni motoni, damu yenu itamwagika katika nchi. Mtu hatawakumbuka tena. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Ezekieli 21:18-32 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Neno la BWANA likanijia tena, kusema, Tena, mwanadamu, ujiwekee njia mbili, upanga wa mfalme wa Babeli upate kuja; hizo mbili zitatoka katika nchi moja; ukaandike mahali, upaandike penye kichwa cha njia iendayo mjini. Utachora njia, ili upanga upate kufikia Raba wa wana wa Amoni, na kufikia Yuda katika Yerusalemu, wenye maboma. Maana mfalme wa Babeli alisimama penye njia panda, penye kichwa cha njia hizo mbili, ili atumie uganga; aliitikisa mishale huku na huko, akaziuliza terafi, akayatazama maini. Katika mkono wake wa kulia alikuwa na kura ya Yerusalemu, kuviweka vyombo vya kubomolea, kufumbua kinywa katika machinjo, kuiinua sauti kwa kupiga kelele sana, kuweka vyombo vya kubomolea juu ya malango, kufanya maboma, na kujenga ngome. Jambo hili litakuwa kwao kama uganga wa ubatili, mbele ya macho yao waliowaapia viapo lakini ataufanya uovu ukumbukwe, ili kwamba wakamatwe. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa mmeufanya uovu wenu ukumbukwe, kwa maana makosa yenu yamefunuliwa, hata dhambi zenu zikaonekana kwa matendo yenu; kwa sababu mmekumbukwa, mtakamatwa kwa mkono. Na wewe, Ewe mtu mwovu, uliyetiwa jeraha kiasi cha kukuua, mkuu wa Israeli, ambaye siku yako imekuja, katika wakati wa uovu wa mwisho; Bwana MUNGU asema hivi; Kiondoe kilemba, livue taji; haya hayatakuwa tena kama yalivyo; kikweze kilicho chini, kakishushe kilichoinuka. Nitakipindua, nitakipindua, nitakipindua; hiki nacho hakitakuwa tena, hata atakapokuja yeye ambaye ni haki yake; nami nitampa. Nawe, mwanadamu, tabiri useme, Bwana MUNGU asema hivi, kuhusu wana wa Amoni, na kuhusu aibu yao; Nena, Upanga; upanga umefutwa; umeng'arishwa, ili kuua, ili kuufanya uue sana, upate kuwa kama umeme; wakati wanapokupa maono ya udanganyifu, wakati wanapokuagulia uongo, wanakuweka juu ya shingo zao wachukizao, na waovu, ambao siku yao imekuja, katika wakati wa adhabu ya mwisho. Uurudishe alani mwake. Mahali pale ulipoumbwa, katika nchi uliyozaliwa; nitakuhukumu wewe. Nami nitamwaga ghadhabu yangu juu yako; nitakupulizia moto wa hasira yangu; nami nitakutia katika mikono ya watu walio kama hayawani, wajuao sana kuangamiza. Utakuwa kuni za kutiwa motoni; damu yako itamwagika katikati ya nchi; hutakumbukwa tena; maana mimi, BWANA, nimenena neno hili.
Ezekieli 21:18-32 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Neno la BWANA likanijia tena, kusema, Tena, mwanadamu, ujiwekee njia mbili, upanga wa mfalme wa Babeli upate kuja; hizo mbili zitatoka katika nchi moja; ukaandike mahali, upaandike penye kichwa cha njia iendayo mjini. Utaagiza njia, upanga upate kufikilia Raba wa wana wa Amoni, na kufikilia Yuda katika Yerusalemu, wenye maboma. Maana mfalme wa Babeli alisimama penye njia panda, penye kichwa cha njia hizo mbili, ili atumie uganga; aliitikisa mishale huko na huko, akaziuliza terafi, akayatazama maini. Katika mkono wake wa kuume alikuwa na kura ya Yerusalemu, kuviweka vyombo vya kubomolea, kufumbua kinywa katika machinjo, kuiinua sauti kwa kupiga kelele sana, kuweka vyombo vya kubomolea juu ya malango, kufanya maboma, na kujenga ngome. Jambo hili litakuwa kwao kama uganga wa ubatili, mbele ya macho yao waliowaapia viapo lakini ataufanya uovu ukumbukwe, ili kwamba wakamatwe. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa mmeufanya uovu wenu ukumbukwe, kwa maana makosa yenu yamefunuliwa, hata dhambi zenu zikaonekana kwa matendo yenu; kwa sababu mmekumbukwa, mtakamatwa kwa mkono. Na wewe, Ewe mtu mwovu, uliyetiwa jeraha kiasi cha kukuua, mkuu wa Israeli, ambaye siku yako imekuja, katika wakati wa uovu wa mwisho; Bwana MUNGU asema hivi; Kiondoe kilemba, ivue taji; haya hayatakuwa tena kama yalivyo; kikweze kilicho chini, kakishushe kilichoinuka. Nitakipindua, nitakipindua, nitakipindua; hiki nacho hakitakuwa tena, hata atakapokuja yeye ambaye ni haki yake; nami nitampa. Nawe, mwanadamu, tabiri useme, Bwana MUNGU asema hivi, katika habari za wana wa Amoni, na katika habari za aibu yao; Nena, Upanga; upanga umefutwa; umesuguliwa, ili kuua, ili kuufanya uue sana, upate kuwa kama umeme; wakati wakuoneapo ubatili, wakati wakufanyiao uganga wa uongo, ili kukuweka juu ya shingo zao waliotiwa jeraha kiasi cha kuwaua, ambao siku yao imekuja, katika wakati wa uovu wa mwisho. Uurudishe alani mwake. Mahali pale ulipoumbwa, katika nchi uliyozaliwa; nitakuhukumu wewe. Nami nitamwaga ghadhabu yangu juu yako; nitakupulizia moto wa hasira yangu; nami nitakutia katika mikono ya watu walio kama hayawani, wajuao sana kuangamiza. Utakuwa kuni za kutiwa motoni; damu yako itakuwa katikati ya nchi; hutakumbukwa tena; maana mimi, BWANA, nimenena neno hili.