Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 14:1-11

Ezekieli 14:1-11 SRUV

Ndipo baadhi ya wazee wa Israeli wakanijia, wakaketi mbele yangu. Ndipo neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, watu hawa wametwaa vinyago vyao na kuvitia mioyoni mwao, nao wameweka kwazo la uovu wao mbele ya nyuso zao. Je! Nitakubali kuombwa ushauri na wao? Basi sema nao, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Kila mtu wa nyumba ya Israeli atwaaye vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake, na kumwendea nabii; mimi, BWANA, nitamjibu neno lake kulingana na wingi wa sanamu zake; ili niwakamate nyumba ya Israeli kwa mioyo yao wenyewe, kwa sababu wamefarakana nami kwa vinyago vyao. Kwa sababu hiyo uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Rudini ninyi, mkageuke na kuviacha vinyago vyenu; mkageuze nyuso zenu zisielekee machukizo yenu yote. Kwa maana kila mtu wa nyumba ya Israeli, au wa wageni wakaao katika Israeli, ajitengaye nami, na kuvitwaa vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake, kisha kumwendea nabii, na kuniuliza neno kwa ajili ya nafsi yake; mimi, BWANA, nitamjibu, mimi mwenyewe; nami nitaukaza uso wangu juu ya mtu yule, na kumfanya kuwa ajabu, awe ishara na mithali, nami nitamkatilia mbali, asiwe kati ya watu wangu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Na nabii akidanganyika, na kusema neno, mimi, BWANA, nimemdanganya nabii yule, nami nitaunyosha mkono wangu juu yake, na kumwangamiza, asiwe kati ya watu wangu Israeli. Nao watauchukua uovu wao; uovu wa nabii utakuwa sawasawa na uovu wake yule amwendeaye aulize neno; ili nyumba ya Israeli wasipotee mbali nami, wala wasijitie unajisi tena kwa makosa yao yote; bali wawe watu wangu, nami niwe Mungu wao, asema Bwana MUNGU.