Ezekieli 14:1-11
Ezekieli 14:1-11 NEN
Baadhi ya wazee wa Israeli walinijia na kuketi mbele yangu. Ndipo neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, watu hawa wameweka sanamu katika mioyo yao na kuweka vitu viovu vya kukwaza mbele ya macho yao. Je, kweli niwaruhusu waniulize jambo lolote? Kwa hiyo sema nao uwaambie, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Wakati Mwisraeli yeyote anapoweka sanamu moyoni mwake na kuweka kitu kiovu cha kukwaza mbele ya macho yake na kisha akaenda kwa nabii, Mimi BWANA nitamjibu peke yangu sawasawa na ukubwa wa ibada yake ya sanamu. Nitafanya jambo hili ili kukamata tena mioyo ya watu wa Israeli, ambao wote wameniacha kwa ajili ya sanamu zao.’ “Kwa hiyo iambie nyumba ya Israeli, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Tubuni! Geukeni kutoka kwenye sanamu zenu na mkatae matendo yenu yote ya machukizo! “ ‘Mwisraeli yeyote au mgeni yeyote anayeishi katika Israeli anapojitenga nami na kujiwekea sanamu katika moyo wake na kwa hivyo kuweka kitu kiovu cha kukwaza mbele ya macho yake na kisha akamwendea nabii kuuliza shauri kwangu, mimi BWANA nitamjibu mwenyewe. Nitaukaza uso wangu dhidi ya mtu huyo na kumwadhibu na kumfanya ishara kwa watu. Nitamkatilia mbali kutoka watu wangu. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA. “ ‘Naye nabii kama atakuwa ameshawishika kutoa unabii, Mimi BWANA nitakuwa nimemshawishi nabii huyo, nami nitaunyoosha mkono wangu dhidi yake na kumwangamiza kutoka miongoni mwa watu wangu Israeli. Watachukua hatia yao, nabii atakuwa na hatia sawa na yule mtu aliyekuja kuuliza neno kwake. “ ‘Ndipo watu wa Israeli hawataniacha tena, wala kujitia unajisi tena kwa dhambi zao zote. Ndipo watakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wao, asema BWANA Mwenyezi.’ ”