Ezekieli 14:1-11
Ezekieli 14:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku moja baadhi ya wazee wa Israeli walinitembelea kutaka shauri. Basi neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Wewe mtu, watu hawa wamekubali mioyo yao itawaliwe na sanamu za miungu; miungu hiyo inawaelekeza kutenda dhambi. Je, nitakubali kuulizwa nao shauri? Basi, sema nao uwaambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Mtu yeyote miongoni mwa Waisraeli anayekubali sanamu za miungu zimtawale moyoni, na kuiruhusu miungu hiyo kumwelekeza kutenda dhambi, kisha akaja kumwomba shauri nabii, atapata jibu kutoka kwangu ambalo litazifaa hata sanamu zake nyingi za miungu. Nitaigusa mioyo ya Waisraeli ili wanirudie, kwani wamejitenga mbali nami kwa kuabudu sanamu zao za miungu. “Basi, waambie Waisraeli kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Tubuni, na kuacha kuziabudu sanamu zenu za miungu. Acheni kufanya machukizo. Wakati wowote mmojawapo wa Waisraeli au mgeni yeyote akaaye katika Israeli, anapojitenga nami na kuanza kuziabudu sanamu za miungu kwa bidii na dhambi hiyo ikawa kizuizi kati yangu naye, halafu akamwendea nabii ili kujua matakwa yangu, basi, mimi Mwenyezi-Mungu mwenyewe, nitamjibu mtu huyo. Nitapambana naye. Nitamfanya kuwa ishara na kielelezo; nitamwondoa kabisa kutoka taifa langu. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. Na ikiwa nabii huyo atadanganyika akasema kitu, basi mimi Mwenyezi-Mungu nimempotosha. Nami nitanyosha mkono wangu kumwondoa nabii huyo kutoka kwa watu wangu wa Israeli. Nitamwadhibu huyo nabii pamoja na huyo mtu aliyekuja kumwuliza matakwa yangu; wote watapata adhabu ileile, ili watu wa Israeli wasiniache tena na kujichafua wenyewe kwa kutenda dhambi; ili wawe watu wangu nami niwe Mungu wao. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Ezekieli 14:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo baadhi ya wazee wa Israeli wakanijia, wakaketi mbele yangu. Ndipo neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, watu hawa wametwaa vinyago vyao na kuvitia mioyoni mwao, nao wameweka kwazo la uovu wao mbele ya nyuso zao. Je! Nitakubali kuombwa ushauri na wao? Basi sema nao, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Kila mtu wa nyumba ya Israeli atwaaye vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake, na kumwendea nabii; mimi, BWANA, nitamjibu neno lake kulingana na wingi wa sanamu zake; ili niwakamate nyumba ya Israeli kwa mioyo yao wenyewe, kwa sababu wamefarakana nami kwa vinyago vyao. Kwa sababu hiyo uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Rudini ninyi, mkageuke na kuviacha vinyago vyenu; mkageuze nyuso zenu zisielekee machukizo yenu yote. Kwa maana kila mtu wa nyumba ya Israeli, au wa wageni wakaao katika Israeli, ajitengaye nami, na kuvitwaa vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake, kisha kumwendea nabii, na kuniuliza neno kwa ajili ya nafsi yake; mimi, BWANA, nitamjibu, mimi mwenyewe; nami nitaukaza uso wangu juu ya mtu yule, na kumfanya kuwa ajabu, awe ishara na mithali, nami nitamkatilia mbali, asiwe kati ya watu wangu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Na nabii akidanganyika, na kusema neno, mimi, BWANA, nimemdanganya nabii yule, nami nitaunyosha mkono wangu juu yake, na kumwangamiza, asiwe kati ya watu wangu Israeli. Nao watauchukua uovu wao; uovu wa nabii utakuwa sawasawa na uovu wake yule amwendeaye aulize neno; ili nyumba ya Israeli wasipotee mbali nami, wala wasijitie unajisi tena kwa makosa yao yote; bali wawe watu wangu, nami niwe Mungu wao, asema Bwana MUNGU.
Ezekieli 14:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo baadhi ya wazee wa Israeli wakanijia, wakaketi mbele yangu. Ndipo neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, watu hawa wametwaa vinyago vyao na kuvitia mioyoni mwao, nao wameweka kwazo la uovu wao mbele ya nyuso zao. Je! Ni laiki yangu niulizwe na wao katika neno lo lote? Basi sema nao, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Kila mtu wa nyumba ya Israeli atwaaye vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake, na kumwendea nabii; mimi, BWANA, nitamjibu neno lake sawasawa na wingi wa sanamu zake; ili niwakamate nyumba ya Israeli kwa mioyo yao wenyewe, kwa sababu wamefarakana nami kwa vinyago vyao. Kwa sababu hiyo uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Rudini ninyi, mkageuke na kuviacha vinyago vyenu; mkageuze nyuso zenu zisielekee machukizo yenu yote. Kwa maana kila mtu wa nyumba ya Israeli, au wa wageni wakaao katika Israeli, ajitengaye nami, na kuvitwaa vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake, kisha kumwendea nabii, na kuniuliza neno kwa ajili ya nafsi yake; mimi, BWANA, nitamjibu, mimi mwenyewe; nami nitaukaza uso wangu juu ya mtu yule, na kumfanya kuwa ajabu, awe ishara na mithali, nami nitamkatilia mbali, asiwe kati ya watu wangu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Na nabii akidanganyika, na kusema neno, mimi, BWANA, nimemdanganya nabii yule, nami nitaunyosha mkono wangu juu yake, na kumwangamiza, asiwe kati ya watu wangu Israeli. Nao watauchukua uovu wao; uovu wa nabii utakuwa sawasawa na uovu wake yule amwendeaye aulize neno; ili nyumba ya Israeli wasipotee mbali nami, wala wasijitie unajisi tena kwa makosa yao yote; bali wawe watu wangu, nami niwe Mungu wao, asema Bwana MUNGU.
Ezekieli 14:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Baadhi ya wazee wa Israeli walinijia na kuketi mbele yangu. Ndipo neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, watu hawa wameweka sanamu katika mioyo yao na kuweka vitu viovu vya kukwaza mbele ya macho yao. Je, kweli niwaruhusu waniulize jambo lolote? Kwa hiyo sema nao uwaambie, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Wakati Mwisraeli yeyote anapoweka sanamu moyoni mwake na kuweka kitu kiovu cha kukwaza mbele ya macho yake na kisha akaenda kwa nabii, Mimi BWANA nitamjibu peke yangu sawasawa na ukubwa wa ibada yake ya sanamu. Nitafanya jambo hili ili kukamata tena mioyo ya watu wa Israeli, ambao wote wameniacha kwa ajili ya sanamu zao.’ “Kwa hiyo iambie nyumba ya Israeli, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Tubuni! Geukeni kutoka kwenye sanamu zenu na mkatae matendo yenu yote ya machukizo! “ ‘Mwisraeli yeyote au mgeni yeyote anayeishi katika Israeli anapojitenga nami na kujiwekea sanamu katika moyo wake na kwa hivyo kuweka kitu kiovu cha kukwaza mbele ya macho yake na kisha akamwendea nabii kuuliza shauri kwangu, mimi BWANA nitamjibu mwenyewe. Nitaukaza uso wangu dhidi ya mtu huyo na kumwadhibu na kumfanya ishara kwa watu. Nitamkatilia mbali kutoka watu wangu. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA. “ ‘Naye nabii kama atakuwa ameshawishika kutoa unabii, Mimi BWANA nitakuwa nimemshawishi nabii huyo, nami nitaunyoosha mkono wangu dhidi yake na kumwangamiza kutoka miongoni mwa watu wangu Israeli. Watachukua hatia yao, nabii atakuwa na hatia sawa na yule mtu aliyekuja kuuliza neno kwake. “ ‘Ndipo watu wa Israeli hawataniacha tena, wala kujitia unajisi tena kwa dhambi zao zote. Ndipo watakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wao, asema BWANA Mwenyezi.’ ”