Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 6:1-27

Kutoka 6:1-27 SRUV

BWANA akamwambia Musa, Sasa utaona nitakavyomtenda Farao; maana kwa mkono hodari atawapa ruhusa kwenda zao, na kwa mkono hodari atawafukuza katika nchi yake. Kisha Mungu akasema na Musa, akamwambia, Mimi ni BWANA; nami nilimtokea Abrahamu, na Isaka, na Yakobo, kama Mungu Mwenyezi, bali kwa jina langu YEHOVA sikujulikana kwao. Tena nimelithibitisha agano langu nao, la kuwapa nchi ya Kanaani; nchi ya waliyokaa kama wageni. Na zaidi ya hayo, nimesikia kuugua kwao wana wa Israeli, ambao Wamisri wanawatumikisha, nami nimelikumbuka agano langu. Basi waambie wana wa Israeli, Mimi ni BWANA nami nitawatoa ninyi mtoke chini ya ukandamizaji wa Wamisri, nami nitawaokoa kutoka utumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyoshwa, na kwa hukumu kubwa; nami nitawatwaeni kuwa watu wangu, nitakuwa Mungu kwenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ni YEHOVA, Mungu wenu, niwakomboaye mtoke chini ya mizigo ya Wamisri. Nami nitawaleta hata nchi ile ambayo niliinua mkono wangu, niwape Abrahamu, na Isaka, na Yakobo; nitawapa iwe urithi wenu; Mimi ni YEHOVA. Musa akawaambia wana wa Israeli maneno haya; lakini hawakumsikiliza Musa kwa ajili ya uchungu wa moyo, na kwa ajili ya utumwa mgumu. BWANA akasema na Musa, akamwambia, Ingia ndani, ukaseme na Farao, mfalme wa Misri, ili awape ruhusa wana wa Israeli watoke nchi yake. Musa akanena mbele za BWANA, akasema, Tazama, hao wana wa Israeli hawakunisikiza mimi; basi huyo Farao atanisikizaje, mimi niliye na midomo isiyo tohara? BWANA akanena na Musa na Haruni, akawaagiza wawaendee wana wa Israeli, na Farao, mfalme wa Misri, ili awatoe hao wana wa Israeli katika nchi ya Misri. Hawa ndio vichwa vya nyumba za baba zao: wana wa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Israeli; ni Hanoki, na Palu, na Hesroni, na Karmi; hao ni jamaa za Reubeni. Na wana wa Simeoni; ni Yemueli, na Yamini, na Ohadi, na Yakini, na Sohari, na Shauli mwana wa mwanamke wa Kikanaani; hao ni jamaa za Simeoni. Na haya ndiyo majina ya wana wa Lawi, kulingana na vizazi vyao; Gershoni, na Kohathi, na Merari; na miaka ya maisha yake Lawi ilikuwa ni miaka mia moja na thelathini na saba. Wana wa Gershoni; ni Libni, na Shimei, kulingana na jamaa zao. Na wana wa Kohathi; ni Amramu, na Ishari, na Hebroni, na Uzieli; na miaka ya maisha ya huyo Kohathi ilikuwa ni miaka mia moja na thelathini na mitatu. Na wana wa Merari; ni Mali, na Mushi. Hizi ni jamaa za hao Walawi kulingana na vizazi vyao. Huyo Amramu akamwoa Yokebedi shangazi yake; naye akamzalia Haruni, na Musa; na miaka ya maisha yake Amramu ilikuwa ni miaka mia moja na thelathini na saba. Na wana wa Ishari; ni Kora, na Nefegi, na Zikri. Na wana wa Uzieli; ni Mishaeli, na Elisafani, na Sithri. Haruni akamwoa Elisheba, binti ya Aminadabu, dada yake Nashoni; naye akamzalia Nadabu, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari. Na wana wa Kora; ni Asiri, na Elkana, na Abiasafu; hizo ni jamaa za hao Wakora. Na Eleazari mwana wa Haruni akamwoa mmoja miongoni mwa binti za Putieli; naye akamzalia Finehasi. Hawa ndio vichwa vya nyumba za baba wa Walawi kulingana na jamaa zao. Hawa ni Haruni yeye yule, na Musa yeye yule, BWANA aliowaambia, akisema, Watoeni wana wa Israeli watoke nchi ya Misri sawasawa na majeshi yao. Ni hao walionena na Farao mfalme wa Misri ili wawatoe wana wa Israeli watoke Misri; hao ni Musa yeye yule, na Haruni yeye yule.

Soma Kutoka 6

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Kutoka 6:1-27