Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 6:1-27

Kutoka 6:1-27 Biblia Habari Njema (BHN)

Lakini Mwenyezi-Mungu akamjibu Mose, “Sasa utaona jinsi nitakavyomtenda Farao; maana kwa nguvu atalazimika kuwaacha watu wangu watoke. Naam, kwa nguvu atawafukuza waondoke nchini mwake.” Mungu akamwambia Mose, “Mimi ni Mwenyezi-Mungu. Nilimtokea Abrahamu, Isaka na Yakobo nikijulikana kama Mungu Mwenye Nguvu, ingawa kwa jina langu, Mwenyezi-Mungu, sikuwajulisha. Tena nilifanya agano nao kwamba nitawapa nchi ya Kanaani ambako waliishi kama wageni. Zaidi ya hayo, nimesikia kilio cha Waisraeli ambao wamelazimishwa kufanya kazi za kitumwa na Wamisri, nikalikumbuka agano langu. Kwa hiyo, waambie Waisraeli hivi, ‘Mimi ni Mwenyezi-Mungu! Mimi nitawatoa katika nira mlizowekewa na Wamisri. Nitawaokoeni utumwani mwenu. Nitaunyosha mkono wangu wenye nguvu na kuwaadhibu vikali Wamisri na kuwakomboa nyinyi. Nitawafanyeni kuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu. Nyinyi mtatambua kuwa mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, niliyewatoa katika nira za Wamisri. Nami nitawapeleka katika nchi ile niliyoapa kumpa Abrahamu, Isaka na Yakobo. Nitawapeni nchi hiyo iwe yenu. Mimi ni Mwenyezi-Mungu.’” Mose akawaeleza Waisraeli maneno hayo. Lakini wao hawakumsikiliza kwa sababu walikuwa wamekufa moyo kutokana na utumwa mkali. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao, mfalme wa Misri, umwambie awaache Waisraeli waondoke nchini mwake.” Lakini Mose akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Tazama, Waisraeli hawanisikilizi mimi, sembuse Farao! Tena mimi ni mtu asiye na ufasaha wa kuongea!” Lakini Mwenyezi-Mungu akaongea na Mose na Aroni, akawaagiza waende kwa Farao, mfalme wa Misri, na kuwatoa Waisraeli nchini Misri. Hii ndiyo orodha ya wakuu wa jamaa za Waisraeli, Wana wa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Israeli: Henoki, Palu, Hesroni na Karmi. Hao walikuwa mababu wa jamaa za Reubeni. Wana wa Simeoni walikuwa: Yemueli, Yamini, Ohadi, Yakini, Sohari na Shauli; huyu wa mwisho alikuwa mtoto wa mwanamke wa Kikanaani. Hao walikuwa mababu wa jamaa za Simeoni. Sasa yafuata majina ya wana wa Lawi na wazawa wao: Gershoni, Kohathi na Merari. Lawi aliishi miaka 137. Wana wa Gershoni walikuwa: Libni na Shimei; jamaa zao zilitajwa kwa majina yao. Wana wa Kohathi walikuwa: Amramu, Ishari, Hebroni na Uzieli. Kohathi aliishi miaka 133. Wana wa Merari walikuwa: Mahli na Mushi. Hao ndio mababu wa jamaa za Walawi. Amramu alimwoa Yokebedi, shangazi yake, naye akamzalia Aroni na Mose. Amramu aliishi miaka 137. Na watoto wa kiume wa Ishari walikuwa: Kora, Nefegi na Zikri. Watoto wa kiume wa Uzieli walikuwa: Mishaeli, Elsafani na Sithri. Aroni alimwoa Elisheba, binti yake Aminadabu, dada yake Nashoni; naye akamzalia Nadabu, Abihu, Eleazari na Ithamari. Nao watoto wa kiume wa Kora walikuwa: Asiri, Elkana na Abiasafu, ambao walikuwa mababu wa jamaa za Kora. Eleazari, mwana wa Aroni, alimwoa mmoja wa binti za Putieli, naye akamzalia Finehasi. Hawa ndio waliokuwa wakuu wa jamaa za Lawi. Aroni na Mose ndio walioambiwa na Mwenyezi-Mungu, “Watoeni watu wa Israeli kutoka nchi ya Misri, vikundi kwa vikundi.” Ndio haohao Mose na Aroni walioongea na Farao, mfalme wa Misri, juu ya kuwatoa Waisraeli nchini Misri.

Shirikisha
Soma Kutoka 6

Kutoka 6:1-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)

BWANA akamwambia Musa, Sasa utaona nitakavyomtenda Farao; maana kwa mkono hodari atawapa ruhusa kwenda zao, na kwa mkono hodari atawafukuza katika nchi yake. Kisha Mungu akasema na Musa, akamwambia, Mimi ni BWANA; nami nilimtokea Abrahamu, na Isaka, na Yakobo, kama Mungu Mwenyezi, bali kwa jina langu YEHOVA sikujulikana kwao. Tena nimelithibitisha agano langu nao, la kuwapa nchi ya Kanaani; nchi ya waliyokaa kama wageni. Na zaidi ya hayo, nimesikia kuugua kwao wana wa Israeli, ambao Wamisri wanawatumikisha, nami nimelikumbuka agano langu. Basi waambie wana wa Israeli, Mimi ni BWANA nami nitawatoa ninyi mtoke chini ya ukandamizaji wa Wamisri, nami nitawaokoa kutoka utumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyoshwa, na kwa hukumu kubwa; nami nitawatwaeni kuwa watu wangu, nitakuwa Mungu kwenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ni YEHOVA, Mungu wenu, niwakomboaye mtoke chini ya mizigo ya Wamisri. Nami nitawaleta hata nchi ile ambayo niliinua mkono wangu, niwape Abrahamu, na Isaka, na Yakobo; nitawapa iwe urithi wenu; Mimi ni YEHOVA. Musa akawaambia wana wa Israeli maneno haya; lakini hawakumsikiliza Musa kwa ajili ya uchungu wa moyo, na kwa ajili ya utumwa mgumu. BWANA akasema na Musa, akamwambia, Ingia ndani, ukaseme na Farao, mfalme wa Misri, ili awape ruhusa wana wa Israeli watoke nchi yake. Musa akanena mbele za BWANA, akasema, Tazama, hao wana wa Israeli hawakunisikiza mimi; basi huyo Farao atanisikizaje, mimi niliye na midomo isiyo tohara? BWANA akanena na Musa na Haruni, akawaagiza wawaendee wana wa Israeli, na Farao, mfalme wa Misri, ili awatoe hao wana wa Israeli katika nchi ya Misri. Hawa ndio vichwa vya nyumba za baba zao: wana wa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Israeli; ni Hanoki, na Palu, na Hesroni, na Karmi; hao ni jamaa za Reubeni. Na wana wa Simeoni; ni Yemueli, na Yamini, na Ohadi, na Yakini, na Sohari, na Shauli mwana wa mwanamke wa Kikanaani; hao ni jamaa za Simeoni. Na haya ndiyo majina ya wana wa Lawi, kulingana na vizazi vyao; Gershoni, na Kohathi, na Merari; na miaka ya maisha yake Lawi ilikuwa ni miaka mia moja na thelathini na saba. Wana wa Gershoni; ni Libni, na Shimei, kulingana na jamaa zao. Na wana wa Kohathi; ni Amramu, na Ishari, na Hebroni, na Uzieli; na miaka ya maisha ya huyo Kohathi ilikuwa ni miaka mia moja na thelathini na mitatu. Na wana wa Merari; ni Mali, na Mushi. Hizi ni jamaa za hao Walawi kulingana na vizazi vyao. Huyo Amramu akamwoa Yokebedi shangazi yake; naye akamzalia Haruni, na Musa; na miaka ya maisha yake Amramu ilikuwa ni miaka mia moja na thelathini na saba. Na wana wa Ishari; ni Kora, na Nefegi, na Zikri. Na wana wa Uzieli; ni Mishaeli, na Elisafani, na Sithri. Haruni akamwoa Elisheba, binti ya Aminadabu, dada yake Nashoni; naye akamzalia Nadabu, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari. Na wana wa Kora; ni Asiri, na Elkana, na Abiasafu; hizo ni jamaa za hao Wakora. Na Eleazari mwana wa Haruni akamwoa mmoja miongoni mwa binti za Putieli; naye akamzalia Finehasi. Hawa ndio vichwa vya nyumba za baba wa Walawi kulingana na jamaa zao. Hawa ni Haruni yeye yule, na Musa yeye yule, BWANA aliowaambia, akisema, Watoeni wana wa Israeli watoke nchi ya Misri sawasawa na majeshi yao. Ni hao walionena na Farao mfalme wa Misri ili wawatoe wana wa Israeli watoke Misri; hao ni Musa yeye yule, na Haruni yeye yule.

Shirikisha
Soma Kutoka 6

Kutoka 6:1-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

BWANA akamwambia Musa, Sasa utaona nitakavyomtenda Farao; maana kwa mkono hodari atawapa ruhusa kwenda zao, na kwa mkono hodari atawafukuza katika nchi yake. Kisha Mungu akasema na Musa, akamwambia, Mimi ni YEHOVA; nami nilimtokea Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kama Mungu Mwenyezi, bali kwa jina langu YEHOVA sikujulikana kwao. Tena nimelithibitisha agano langu nao, la kuwapa nchi ya Kanaani; nchi ya kukaa kwao hali ya ugeni. Na zaidi ya hayo, nimesikia kuugua kwao wana wa Israeli, ambao Wamisri wanawatumikisha, nami nimelikumbuka agano langu. Basi waambie wana wa Israeli, Mimi ni YEHOVA, nami nitawatoa ninyi mtoke chini ya mizigo ya Wamisri, nami nitawaokoa na utumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyoshwa, na kwa hukumu kubwa; nami nitawatwaeni kuwa watu wangu, nitakuwa Mungu kwenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ni YEHOVA, Mungu wenu, niwatoaye mtoke chini ya mizigo ya Wamisri. Nami nitawaleta hata nchi ile ambayo naliinua mkono wangu, niwape Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; nitawapa iwe urithi wenu; Mimi ni YEHOVA. Musa akawaambia wana wa Israeli maneno haya; lakini hawakumsikiliza Musa kwa ajili ya uchungu wa moyo, na kwa ajili ya utumwa mgumu. BWANA akasema na Musa, akamwambia, Ingia ndani, ukaseme na Farao, mfalme wa Misri, ili awape ruhusa wana wa Israeli watoke nchi yake. Musa akanena mbele ya BWANA, akasema, Tazama, hao wana wa Israeli hawakunisikiza mimi; basi huyo Farao atanisikizaje, mimi niliye na midomo isiyo tohara? BWANA akanena na Musa na Haruni, akawaagiza wawaendee wana wa Israeli, na Farao, mfalme wa Misri, ili awatoe hao wana wa Israeli katika nchi ya Misri. Hawa ndio vichwa vya nyumba za baba zao: wana wa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Israeli; ni Hanoki, na Palu, na Hesroni, na Karmi; hao ni jamaa za Reubeni. Na wana wa Simeoni; ni Yemueli, na Yamini, na Ohadi, na Yakini, na Sohari, na Shauli mwana wa mwanamke wa Kikanaani; hao ni jamaa za Simeoni. Na haya ndiyo majina ya wana wa Lawi, sawasawa na vizazi vyao; Gershoni, na Kohathi, na Merari; na miaka ya maisha yake Lawi ilikuwa ni miaka mia na thelathini na saba. Wana wa Gershoni; ni Libni, na Shimei, sawasawa na jamaa zao. Na wana wa Kohathi; ni Amramu, na Ishari, na Hebroni, na Uzieli; na miaka ya maisha ya huyo Kohathi ilikuwa ni miaka mia na thelathini na mitatu. Na wana wa Merari; ni Mali, na Mushi. Hizi ni jamaa za hao Walawi sawasawa na vizazi vyao. Huyo Amramu akamwoa Yokebedi ndugu ya baba yake; naye akamzalia Haruni, na Musa; na miaka ya maisha yake Amramu ilikuwa ni miaka mia na thelathini na saba. Na wana wa Ishari; ni Kora, na Nefegi, na Zikri. Na wana wa Uzieli; ni Mishaeli, na Elisafani, na Sithri. Haruni akamwoa Elisheba, binti ya Aminadabu, umbu lake Nashoni; naye akamzalia Nadabu, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari. Na wana wa Kora; ni Asiri, na Elkana, na Abiasafu; hizo ni jamaa za hao Wakora. Na Eleazari mwana wa Haruni akamwoa mmoja miongoni mwa binti za Putieli; naye akamzalia Finehasi. Hawa ndio vichwa vya nyumba za mababa ya Walawi sawasawa na jamaa zao. Hawa ni Haruni ye yule, na Musa ye yule, BWANA aliowaambia, akisema, Watoeni wana wa Israeli watoke nchi ya Misri sawasawa na majeshi yao. Ni hao walionena na Farao mfalme wa Misri ili wawatoe wana wa Israeli watoke Misri; hao ni Musa ye yule, na Haruni ye yule.

Shirikisha
Soma Kutoka 6

Kutoka 6:1-27 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kisha BWANA akamwambia Mose, “Sasa utaona kitu nitakachomfanyia Farao: Kwa sababu ya mkono wangu wenye nguvu atawaachia watu waende; kwa sababu ya mkono wangu wenye nguvu atawafukuza waondoke nchini mwake.” Pia Mungu akamwambia Mose, “Mimi ndimi BWANA. Nilimtokea Abrahamu, Isaki na Yakobo kama Mungu Mwenyezi, ingawa sikuwajulisha Jina langu, Yehova, Mimi mwenyewe sikujitambulisha kwao. Pia niliweka Agano langu nao kuwapa nchi ya Kanaani, ambako waliishi kama wageni. Zaidi ya hayo, nimesikia kilio cha huzuni cha Waisraeli ambao Wamisri wamewatia utumwani, nami nimelikumbuka Agano langu. “Kwa hiyo, waambie Waisraeli: ‘Mimi ndimi BWANA, nami nitawatoa mtoke katika kongwa la Wamisri. Nitawaweka huru mtoke kuwa watumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyooshwa pamoja na matendo makuu ya hukumu. Nitawatwaa mwe watu wangu mwenyewe, nami nitakuwa Mungu wenu. Ndipo mtajua kuwa mimi ndimi BWANA Mungu wenu, niliyewatoa chini ya kongwa la Wamisri. Nami nitawaleta mpaka nchi niliyoapa kwa mkono ulioinuliwa kumpa Abrahamu, Isaki na Yakobo. Nitawapa iwe milki yenu. Mimi ndimi BWANA.’ ” Mose akawaarifu Waisraeli jambo hili, lakini hawakumsikiliza kwa sababu ya maumivu makuu ya moyoni na utumwa wa kikatili. Ndipo BWANA akamwambia Mose, “Nenda, mwambie Farao mfalme wa Misri awaachie Waisraeli waondoke nchini mwake.” Lakini Mose akamwambia BWANA, “Ikiwa Waisraeli hawatanisikiliza, kwa nini yeye Farao anisikilize mimi, ambaye huzungumza kwa kigugumizi?” Ndipo BWANA akanena na Mose na Aroni kuhusu Waisraeli na Farao mfalme wa Misri, naye akawaamuru wawatoe Waisraeli kutoka Misri. Hawa walikuwa wakuu wa jamaa zao: Wana wa Reubeni mzaliwa wa kwanza wa kiume wa Israeli walikuwa Hanoki, Palu, Hesroni na Karmi. Hawa walikuwa ndio koo za Reubeni. Wana wa Simeoni walikuwa Yemueli, Yamini, Ohadi, Yakini, Sohari na Shauli mwana wa mwanamke Mkanaani. Hawa walikuwa ndio koo za Simeoni. Haya ndiyo majina ya wana wa Lawi kufuatana na orodha zao: Gershoni, Kohathi na Merari. Lawi aliishi miaka 137. Wana wa Gershoni kwa koo, walikuwa Libni na Shimei. Wana wa Kohathi walikuwa Amramu, Ishari, Hebroni na Uzieli. Kohathi aliishi miaka 133. Wana wa Merari walikuwa Mahli na Mushi. Hizi ndizo zilizokuwa koo za Lawi kufuatana na orodha zao. Amramu akamwoa Yokebedi, shangazi yake, ambaye alimzalia Aroni na Mose. Amramu aliishi miaka 137. Wana wa Ishari walikuwa Kora, Nefegi na Zikri. Wana wa Uzieli walikuwa Mishaeli, Elisafani na Sithri. Aroni akamwoa Elisheba binti wa Aminadabu ndugu yake Nashoni, naye akamzalia Nadabu, Abihu, Eleazari na Ithamari. Wana wa Kora walikuwa Asiri, Elikana na Abiasafu. Hawa walikuwa ndio koo za Kora. Eleazari mwana wa Aroni akamwoa mmoja wa binti za Putieli, naye akamzalia Finehasi. Hawa walikuwa ndio wakuu wa jamaa za Walawi, ukoo kwa ukoo. Hawa walikuwa Aroni na Mose wale wale ambao BWANA aliwaambia, “Watoeni Waisraeli katika nchi ya Misri kwa vikosi vyao.” Ndio hao hao waliozungumza na Farao mfalme wa Misri kuhusu kuwatoa Waisraeli Misri. Ilikuwa ni huyo Mose na huyo Aroni.

Shirikisha
Soma Kutoka 6