Kutoka 4:18-31
Kutoka 4:18-31 SRUV
Basi Musa akaenda na kurejea kwa Yethro mkwewe, na kumwambia, Nipe ruhusa niende, nakusihi, niwarudie hao ndugu zangu walioko Misri, nipate kuwaona kwamba wako hai hata sasa. Yethro akamwambia Musa, Haya, nenda kwa amani. BWANA akamwambia Musa huko Midiani, Haya, nenda, rudi Misri; kwa kuwa wale watu wote walioutaka uhai wako wamekwisha kufa. Basi Musa akamchukua mkewe na wanawe, na kuwapandisha juu ya punda, naye akarudi mpaka nchi ya Misri; na Musa akaichukua ile fimbo ya Mungu mkononi mwake. BWANA akamwambia Musa, Hapo utakaporudi Misri, angalia ukazifanye mbele ya Farao zile ajabu zote nilizozitia mkononi mwako; lakini nitaufanya mgumu moyo wake, naye hatawapa ruhusa hao watu waende zao. Nawe umwambie Farao, BWANA asema hivi, Israeli ni mwanangu mimi, mzaliwa wa kwanza wangu; nami nimekuambia, Mpe mwanangu ruhusa aende, ili apate kunitumikia, nawe umekataa kumpa ruhusa aende; angalia basi, mimi nitamwua mwanao, mzaliwa wa kwanza wako. Ndipo walipokuwa njiani mahali pa kulala, BWANA akakutana naye, akataka kumwua. Ndipo Sipora akashika jiwe gumu lenye makali na kulikata govi ya zunga la mwanawe, na kulibwaga miguuni pa Musa akasema. Hakika wewe ni bwana arusi wa damu kwangu. Basi akamwacha. Ndipo huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri. BWANA akamwambia Haruni, Nenda jangwani uonane na Musa. Naye akaenda, akamkuta katika mlima wa Mungu, akambusu. Musa akamwambia Haruni hayo maneno yote ya BWANA ambayo alimtuma aende nayo, na ishara hizo zote alizomwagiza. Musa na Haruni wakaenda, wakawakusanya wazee wote wa watu wa Israeli. Haruni akawaambia maneno yote BWANA aliyonena na Musa akazifanya zile ishara mbele ya watu. Watu wakaamini, na waliposikia ya kuwa BWANA amewajia wana wa Israeli, na ya kuwa ameyaona mateso yao, wakainamisha vichwa vyao wakasujudu.