Kutoka 4:18-31
Kutoka 4:18-31 NEN
Kisha Mose akarudi kwa Yethro mkwewe akamwambia, “Niruhusu nirudi kwa watu wangu Misri kuona kama yuko hata mmoja wao ambaye bado anaishi.” Yethro akamwambia, “Nenda, nami nakutakia mema.” Basi BWANA alikuwa amemwambia Mose huko Midiani, “Rudi Misri kwa maana watu wote waliotaka kukuua wamekufa.” Basi Mose akamchukua mkewe na wanawe, akawapandisha juu ya punda na kuanza safari kurudi Misri. Naye akaichukua ile fimbo ya Mungu mkononi mwake. BWANA akamwambia Mose, “Utakaporudi Misri, hakikisha kwamba utafanya mbele ya Farao maajabu yote niliyokupa uwezo wa kuyafanya. Lakini nitafanya moyo wake kuwa mgumu ili kwamba asiwaruhusu watu waende. Kisha mwambie Farao, ‘Hili ndilo asemalo BWANA: Israeli ni mwanangu mzaliwa wa kwanza, nami nilikuambia, “Ruhusu mwanangu aondoke, ili aweze kuniabudu mimi.” Lakini ukakataa kumruhusu kwenda, basi nitaua mwana wako mzaliwa wa kwanza.’ ” Mose alipokuwa mahali pa kulala wageni akiwa njiani kurudi Misri, BWANA akakutana naye, akataka kumuua. Lakini Sipora akachukua jiwe gumu, akakata govi la mwanawe na kugusa nalo miguu ya Mose. Sipora akasema, “Hakika wewe ni bwana arusi wa damu kwangu.” Sipora alipomwita Mose, “Bwana arusi wa damu,” alikuwa anamaanisha ile tohara. Baada ya hayo BWANA akamwacha. BWANA akamwambia Aroni, “Nenda jangwani ukamlaki Mose.” Basi akakutana na Mose kwenye mlima wa Mungu, akambusu. Kisha Mose akamwambia Aroni kila kitu BWANA alichomtuma kusema, vilevile habari za ishara na maajabu alizokuwa amemwamuru kufanya. Mose na Aroni wakawakusanya wazee wote wa Waisraeli, naye Aroni akawaambia kila kitu BWANA alichokuwa amemwambia Mose. Pia akafanya ishara mbele ya watu, nao wakaamini. Nao waliposikia kuwa BWANA anajishughulisha nao, na kwamba ameona mateso yao, walisujudu na kuabudu.