Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 30:17-38

Kutoka 30:17-38 SRUV

BWANA akanena na Musa, na kumwambia Fanya na birika la shaba, na kitako chake cha shaba, ili kuogea; nawe utaliweka kati ya hema ya kukutania na madhabahu, nawe utalitia maji. Na Haruni na wanawe wataosha mikono yao na miguu yao humo; hapo waingiapo ndani ya hema ya kukutania; watajiosha majini, ili wasife; au hapo watakapoikaribia madhabahu ili watumike, kumteketezea BWANA sadaka ya moto; basi wataosha mikono yao na miguu yao ili kwamba wasife; na neno hili litakuwa amri kwao milele, kwake yeye na kwa wazao wake katika vizazi vyao vyote. Kisha BWANA akasema na Musa, na kumwambia, Jitwalie manukato yaliyo bora, manemane mbichi shekeli mia tano, na mdalasini wenye harufu nzuri nusu ya kiasi hicho, yaani, shekeli mia mbili na hamsini, na miwa shekeli mia mbili na hamsini, na kida shekeli mia tano, kwa kuiandama shekeli ya mahali patakatifu, na mafuta ya zeituni kiasi cha vibaba vitano; nawe utayafanya mafuta ya kutiwa matakatifu, marhamu iliyochanganywa kwa kazi ya ustadi ya mtengezaji manukato; yatakuwa ni mafuta matakatifu ya kutiwa. Nawe utaipaka hema ya kukutania kwa mafuta hayo, na hilo sanduku la ushuhuda, na hiyo meza, vyombo vyake vyote, kinara cha taa, vyombo vyake na madhabahu ya kufukizia uvumba, na madhabahu ya kuteketezea sadaka, pamoja na vyombo vyake vyote, na birika, na kitako chake. Nawe utavitakasa vitu hivyo, ili viwe vitakatifu sana; tena kila kivigusacho vyombo vile kitakuwa kitakatifu. Nawe utawatia mafuta Haruni na wanawe, kuwaweka wakfu, ili wanitumikie wakiwa makuhani. Nawe utanena na wana wa Israeli na kuwaambia, Haya yatakuwa ni mafuta matakatifu ya kutiwa kwa ajili yangu mimi katika vizazi vyenu vyote. Hayatamiminwa katika kiwiliwili cha binadamu, wala msifanye mengine mfano wa haya kama yalivyoungwa kwa viungo vyake; ni matakatifu, na kwenu ninyi yatakuwa matakatifu. Mtu yeyote atakayechanganya mafuta mfano wa haya, au mtu yeyote atakayetia mafuta haya juu ya mgeni, mtu huyo atatengwa mbali na watu wake. BWANA akamwambia Musa, Jitwalie manukato mazuri, yaani, natafi, na shekelethi, na kelbena; viungo vya manukato vizuri pamoja na ubani safi; vitu hivyo vyote na viwe vya kipimo kimoja; nawe utafanya uvumba wa vitu hivyo, manukato ya kazi ya ustadi wa mtengenezaji manukato, yatakuwa yamekolea, safi, matakatifu; nawe baadhi yake utayaponda sana, na kuyaweka mbele ya ushuhuda ndani ya hema ya kukutania, hapo nitakapokutana nawe; nayo yatakuwa kwenu matakatifu sana. Na uvumba utakaofanya, hamtajifanyia uvumba wenye viungo sawasawa na uvumba huo; utakuwa kwenu mtakatifu kwa ajili ya BWANA. Mtu yeyote atakayefanya mfano wa huo, ili kuunusa, mtu huyo atatengwa mbali na watu wake.

Soma Kutoka 30

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Kutoka 30:17-38