Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 30:17-38

Kutoka 30:17-38 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

BWANA akanena na Musa, na kumwambia Fanya na birika la shaba, na tako lake la shaba, ili kuogea; nawe utaliweka kati ya hema ya kukutania na madhabahu, nawe utalitia maji. Na Haruni na wanawe wataosha mikono yao na miguu yao humo; hapo waingiapo ndani ya hema ya kukutania; watajiosha majini, ili wasife; au hapo watakapoikaribia madhabahu ili watumike, kumteketezea BWANA sadaka ya moto; basi wataosha mikono yao na miguu yao ili kwamba wasife; na neno hili litakuwa amri kwao milele, kwake yeye na kwa wazao wake katika vizazi vyao vyote. Kisha BWANA akasema na Musa, na kumwambia, Jitwalie manukato yaliyo bora, manemane mbichi shekeli mia tano, na mdalasini wenye harufu nzuri nusu ya kiasi hicho, yaani, shekeli mia mbili na hamsini, na kane shekeli mia mbili na hamsini, na kida shekeli mia tano, kwa kuiandama shekeli ya mahali patakatifu, na mafuta ya zeituni kiasi cha vibaba vitano; nawe utayafanya mafuta ya kutiwa matakatifu, marhamu iliyochanganywa kwa kazi ya ustadi ya mtengezaji manukato; yatakuwa ni mafuta matakatifu ya kutiwa. Nawe utaipaka hema ya kukutania kwa mafuta hayo, na hilo sanduku la ushuhuda, na hiyo meza, na vyombo vyake vyote, na kinara cha taa, na vyombo vyake, na madhabahu ya kufukizia uvumba, na madhabahu ya kuteketezea sadaka, pamoja na vyombo vyake vyote, na birika, na tako lake. Nawe utavitakasa vitu hivyo, ili viwe vitakatifu sana; tena kila kivigusacho vyombo vile kitakuwa kitakatifu. Nawe utawatia mafuta Haruni na wanawe, na kuwatakasa, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani. Nawe utanena na wana wa Israeli na kuwaambia, Haya yatakuwa ni mafuta matakatifu ya kutiwa kwa ajili yangu mimi katika vizazi vyenu vyote. Hayatamiminwa katika kiwiliwili cha binadamu, wala msifanye mengine mfano wa haya kama yalivyoungwa kwa viungo vyake; ni matakatifu, na kwenu ninyi yatakuwa matakatifu. Mtu awaye yote atakayechanganya mafuta mfano wa haya, au mtu awaye yote atakayetia mafuta haya juu ya mgeni, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake. BWANA akamwambia Musa, Jitwalie manukato mazuri, yaani, natafi, na shekelethi, na kelbena; viungo vya manukato vizuri pamoja na ubani safi; vitu hivyo vyote na viwe vya kipimo kimoja; nawe utafanya uvumba wa vitu hivyo, manukato ya kazi ya ustadi wa mtengenazaji manukato, yatakuwa yamekolea, safi, matakatifu; nawe baadhi yake utayaponda sana, na kuyaweka mbele ya ushuhuda ndani ya hema ya kukutania, hapo nitakapokutana nawe; nayo yatakuwa kwenu matakatifu sana. Na uvumba utakaofanya, hamtajifanyia uvumba wenye viungo sawasawa na uvumba huo; utakuwa kwenu mtakatifu kwa ajili ya BWANA. Mtu ye yote atakayefanya mfano wa huo, ili kuunusa, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake.

Shirikisha
Soma Kutoka 30

Kutoka 30:17-38 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Utatengeneza birika la shaba la kutawadhia lenye tako la shaba, uliweke katikati ya hema la mkutano na madhabahu, na kutia maji ndani yake. Aroni na wanawe watatumia maji hayo kunawia mikono na miguu, kabla ya kuingia kwenye hema la mkutano au kukaribia madhabahu ili kunitolea tambiko mimi Mwenyezi-Mungu, tambiko zitolewazo kwa moto; watafanya hivyo wasije wakafa. Ni lazima wanawe mikono na miguu yao wasije wakafa. Hii itakuwa ni kanuni kwao daima, tangu Aroni na uzao wake, vizazi hata vizazi.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Utachukua viungo bora kabisa kama vifuatavyo: Manemane ya maji kilo sita, mdalasini wenye harufu nzuri kilo tatu, miwa yenye harufu nzuri kilo tatu, na aina nyingine ya mdalasini kilo 6 – vipimo hivyo vyote viwe kufuatana na vipimo vya hema takatifu; chukua pia lita 4 za mafuta. Kutokana na viungo hivyo utatengeneza mafuta matakatifu uyachanganye kama afanyavyo fundi wa manukato; hayo yatatumika kuweka vitu wakfu. Kisha utalimiminia mafuta hayo hema la mkutano, na sanduku la maamuzi; meza na vyombo vyake vyote; kinara cha taa na vyombo vyake, madhabahu ya kufukizia ubani, madhabahu ya sadaka za kuteketezwa na vyombo vyake vyote, birika na tako lake. Utaviweka wakfu, ili viwe vitakatifu kabisa. Chochote kitakachovigusa vifaa hivyo, kitakuwa kitakatifu. Kisha mpake mafuta Aroni na wanawe na kuwaweka wakfu ili wanitumikie kama makuhani. Waambie Waisraeli kwamba haya yatakuwa mafuta yangu matakatifu ya kupaka katika vizazi vyenu vyote. Mafuta haya kamwe yasimiminiwe mtu yeyote wa kawaida, wala yasitengenezwe mafuta mengine ya aina hii; haya ni mafuta matakatifu na ni lazima yawe daima matakatifu kwenu. Yeyote atakayetengeneza mafuta kama haya, au kumpaka mtu asiyestahili kupakwa mafuta haya, mtu huyo atatengwa mbali na watu wake.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Utachukua vipimo vinavyolingana vya viungo vitamu vifuatavyo: Utomvu wa natafi, utomvu wa shekelethi, utomvu wa kelbena na ubani safi. Utatumia vitu hivyo kutengenezea ubani kama utengenezwavyo na fundi manukato, utiwe chumvi upate kuwa safi na mtakatifu. Kisha utasagwa na kufanya unga laini, upate kutumiwa ndani ya hema la mkutano na kulipaka sanduku la agano, mahali nitakapokutana nawe; huo utakuwa ubani mtakatifu kabisa kwenu. Kamwe msifanye ubani wa mchanganyiko huo kwa matumizi yenu wenyewe kwani ubani huo utakuwa mtakatifu mbele yangu. Yeyote atakayejitengenezea ubani wa aina hiyo na kuutumia kama manukato yake binafsi, atatengwa mbali na watu wake.”

Shirikisha
Soma Kutoka 30

Kutoka 30:17-38 Swahili Revised Union Version (SRUV)

BWANA akanena na Musa, na kumwambia Fanya na birika la shaba, na kitako chake cha shaba, ili kuogea; nawe utaliweka kati ya hema ya kukutania na madhabahu, nawe utalitia maji. Na Haruni na wanawe wataosha mikono yao na miguu yao humo; hapo waingiapo ndani ya hema ya kukutania; watajiosha majini, ili wasife; au hapo watakapoikaribia madhabahu ili watumike, kumteketezea BWANA sadaka ya moto; basi wataosha mikono yao na miguu yao ili kwamba wasife; na neno hili litakuwa amri kwao milele, kwake yeye na kwa wazao wake katika vizazi vyao vyote. Kisha BWANA akasema na Musa, na kumwambia, Jitwalie manukato yaliyo bora, manemane mbichi shekeli mia tano, na mdalasini wenye harufu nzuri nusu ya kiasi hicho, yaani, shekeli mia mbili na hamsini, na miwa shekeli mia mbili na hamsini, na kida shekeli mia tano, kwa kuiandama shekeli ya mahali patakatifu, na mafuta ya zeituni kiasi cha vibaba vitano; nawe utayafanya mafuta ya kutiwa matakatifu, marhamu iliyochanganywa kwa kazi ya ustadi ya mtengezaji manukato; yatakuwa ni mafuta matakatifu ya kutiwa. Nawe utaipaka hema ya kukutania kwa mafuta hayo, na hilo sanduku la ushuhuda, na hiyo meza, vyombo vyake vyote, kinara cha taa, vyombo vyake na madhabahu ya kufukizia uvumba, na madhabahu ya kuteketezea sadaka, pamoja na vyombo vyake vyote, na birika, na kitako chake. Nawe utavitakasa vitu hivyo, ili viwe vitakatifu sana; tena kila kivigusacho vyombo vile kitakuwa kitakatifu. Nawe utawatia mafuta Haruni na wanawe, kuwaweka wakfu, ili wanitumikie wakiwa makuhani. Nawe utanena na wana wa Israeli na kuwaambia, Haya yatakuwa ni mafuta matakatifu ya kutiwa kwa ajili yangu mimi katika vizazi vyenu vyote. Hayatamiminwa katika kiwiliwili cha binadamu, wala msifanye mengine mfano wa haya kama yalivyoungwa kwa viungo vyake; ni matakatifu, na kwenu ninyi yatakuwa matakatifu. Mtu yeyote atakayechanganya mafuta mfano wa haya, au mtu yeyote atakayetia mafuta haya juu ya mgeni, mtu huyo atatengwa mbali na watu wake. BWANA akamwambia Musa, Jitwalie manukato mazuri, yaani, natafi, na shekelethi, na kelbena; viungo vya manukato vizuri pamoja na ubani safi; vitu hivyo vyote na viwe vya kipimo kimoja; nawe utafanya uvumba wa vitu hivyo, manukato ya kazi ya ustadi wa mtengenezaji manukato, yatakuwa yamekolea, safi, matakatifu; nawe baadhi yake utayaponda sana, na kuyaweka mbele ya ushuhuda ndani ya hema ya kukutania, hapo nitakapokutana nawe; nayo yatakuwa kwenu matakatifu sana. Na uvumba utakaofanya, hamtajifanyia uvumba wenye viungo sawasawa na uvumba huo; utakuwa kwenu mtakatifu kwa ajili ya BWANA. Mtu yeyote atakayefanya mfano wa huo, ili kuunusa, mtu huyo atatengwa mbali na watu wake.

Shirikisha
Soma Kutoka 30

Kutoka 30:17-38 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kisha BWANA akamwambia Mose, “Tengeneza sinia la shaba lenye kitako cha shaba kwa ajili ya kunawia. Liweke kati ya Hema la Kukutania na madhabahu, kisha uweke maji ndani yake. Aroni na wanawe watanawa mikono na miguu yao kwa maji yatokayo katika hilo sinia. Wakati wowote wanapoingia katika Hema la Kukutania, watanawa kwa maji ili kwamba wasije wakafa. Pia, wanapokaribia madhabahu ili kuhudumu kwa kuleta sadaka zilizotolewa kwa BWANA kwa moto, watanawa mikono na miguu yao ili kwamba wasije wakafa. Hii itakuwa ni amri ya kudumu kwa ajili ya Aroni na wazao wake kwa vizazi vijavyo.” Kisha BWANA akamwambia Mose, “Chukua vikolezi bora vifuatavyo: shekeli 500 za manemane ya maji, shekeli 250 za mdalasini wenye harufu nzuri, shekeli 250 za miwa yenye harufu nzuri, shekeli 500 za aina nyingine ya mdalasini, vyote kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, pia hini ya mafuta ya zeituni. Vitengeneze vikolezi hivi kuwa mafuta matakatifu ya upako yenye harufu nzuri, kazi ya mtengeneza manukato. Yatakuwa mafuta matakatifu ya upako. Kisha yatumie kupaka hilo Hema la Kukutania, Sanduku la Ushuhuda, meza na vifaa vyake vyote, kinara cha taa na vifaa vyake vyote, madhabahu ya kufukizia uvumba, madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote na sinia pamoja na kitako chake. Utaviweka wakfu ili viwe vitakatifu sana na kila kitakachoigusa kitakuwa kitakatifu. “Mtie Aroni na wanawe mafuta na uwaweke wakfu ili waweze kunitumikia katika kazi ya ukuhani. Waambie Waisraeli, ‘Haya yatakuwa mafuta matakatifu yangu ya upako kwa vizazi vijavyo. Usiyamimine juu ya miili ya wanadamu wala usitengeneze mafuta ya aina nyingine kwa utaratibu huu. Ni mafuta matakatifu na ni lazima myaone kuwa ni matakatifu. Mtu yeyote atakayetengeneza manukato kama hayo na yeyote atakayeyamimina juu ya mtu yeyote ambaye si kuhani atakatiliwa mbali na watu wake.’ ” Kisha BWANA akamwambia Mose, “Chukua vikolezi vyenye harufu nzuri vifuatavyo: natafi, shekelethi, kelbena na uvumba safi vyote vikiwa na vipimo sawa, pia tengeneza mchanganyiko wa uvumba wenye harufu nzuri, kazi ya mtengeneza manukato. Utiwe chumvi ili upate kuwa safi na mtakatifu. Saga baadhi yake kuwa unga na uweke mbele ya Sanduku la Ushuhuda ndani ya Hema la Kukutania, mahali ambapo nitakutana nawe. Itakuwa takatifu sana kwenu. Msitengeneze uvumba mwingine wowote wa namna hii kwa ajili yenu wenyewe; uoneni kuwa ni mtakatifu kwa BWANA. Yeyote atakayetengeneza uvumba kama huu ili kufurahia harufu yake nzuri lazima akatiliwe mbali na watu wake.”

Shirikisha
Soma Kutoka 30