Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 30:17-38

Kutoka 30:17-38 NEN

Kisha BWANA akamwambia Mose, “Tengeneza sinia la shaba lenye kitako cha shaba kwa ajili ya kunawia. Liweke kati ya Hema la Kukutania na madhabahu, kisha uweke maji ndani yake. Aroni na wanawe watanawa mikono na miguu yao kwa maji yatokayo katika hilo sinia. Wakati wowote wanapoingia katika Hema la Kukutania, watanawa kwa maji ili kwamba wasije wakafa. Pia, wanapokaribia madhabahu ili kuhudumu kwa kuleta sadaka zilizotolewa kwa BWANA kwa moto, watanawa mikono na miguu yao ili kwamba wasije wakafa. Hii itakuwa ni amri ya kudumu kwa ajili ya Aroni na wazao wake kwa vizazi vijavyo.” Kisha BWANA akamwambia Mose, “Chukua vikolezi bora vifuatavyo: shekeli 500 za manemane ya maji, shekeli 250 za mdalasini wenye harufu nzuri, shekeli 250 za miwa yenye harufu nzuri, shekeli 500 za aina nyingine ya mdalasini, vyote kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, pia hini ya mafuta ya zeituni. Vitengeneze vikolezi hivi kuwa mafuta matakatifu ya upako yenye harufu nzuri, kazi ya mtengeneza manukato. Yatakuwa mafuta matakatifu ya upako. Kisha yatumie kupaka hilo Hema la Kukutania, Sanduku la Ushuhuda, meza na vifaa vyake vyote, kinara cha taa na vifaa vyake vyote, madhabahu ya kufukizia uvumba, madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote na sinia pamoja na kitako chake. Utaviweka wakfu ili viwe vitakatifu sana na kila kitakachoigusa kitakuwa kitakatifu. “Mtie Aroni na wanawe mafuta na uwaweke wakfu ili waweze kunitumikia katika kazi ya ukuhani. Waambie Waisraeli, ‘Haya yatakuwa mafuta matakatifu yangu ya upako kwa vizazi vijavyo. Usiyamimine juu ya miili ya wanadamu wala usitengeneze mafuta ya aina nyingine kwa utaratibu huu. Ni mafuta matakatifu na ni lazima myaone kuwa ni matakatifu. Mtu yeyote atakayetengeneza manukato kama hayo na yeyote atakayeyamimina juu ya mtu yeyote ambaye si kuhani atakatiliwa mbali na watu wake.’ ” Kisha BWANA akamwambia Mose, “Chukua vikolezi vyenye harufu nzuri vifuatavyo: natafi, shekelethi, kelbena na uvumba safi vyote vikiwa na vipimo sawa, pia tengeneza mchanganyiko wa uvumba wenye harufu nzuri, kazi ya mtengeneza manukato. Utiwe chumvi ili upate kuwa safi na mtakatifu. Saga baadhi yake kuwa unga na uweke mbele ya Sanduku la Ushuhuda ndani ya Hema la Kukutania, mahali ambapo nitakutana nawe. Itakuwa takatifu sana kwenu. Msitengeneze uvumba mwingine wowote wa namna hii kwa ajili yenu wenyewe; uoneni kuwa ni mtakatifu kwa BWANA. Yeyote atakayetengeneza uvumba kama huu ili kufurahia harufu yake nzuri lazima akatiliwe mbali na watu wake.”

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Kutoka 30:17-38