Kutoka 12
12
Kuadhimisha Pasaka ya kwanza
1 #
Law 23:5; Hes 9:1-5; 28:16; Kum 16:1-2 BWANA akanena na Musa na Haruni katika nchi ya Misri, akawaambia, 2#Kut 13:4; Kum 16:1 Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu; utakuwa ni mwezi wa kwanza wa mwaka kwenu. 3Waambieni mkutano wote, Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja; 4na ikiwa watu wa nyumba ni wachache kwa mwana-kondoo, basi yeye na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na watwae mwana-kondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu; kwa kadiri ya ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu kwa yule mwana-kondoo. 5#Law 22:19; Mal 1:8,14; Ebr 9:14; 1 Pet 1:19 Mwana-kondoo wenu atakuwa hana dosari, wa kiume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi. 6#Law 23:15; Hes 9:3; 26:18; Kum 16:1,6 Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni. 7Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kuitia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla. 8#Hes 9:11; 1 Kor 5:8 Watakula nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu; tena pamoja na mboga zenye uchungu. 9Msiile mbichi, wala ya kutokoswa majini, bali imeokwa motoni; kichwa chake pamoja na miguu yake, na nyama zake za ndani. 10#Kut 23:18 Wala msisaze kitu chake chochote hata asubuhi, bali kitu kitakachosalia hata asubuhi mtakichoma kwa moto. 11#Kum 16:5 Tena mtamla hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni Pasaka ya BWANA. 12#Kut 11:4,5; Amo 5:17; Hes 33:4 Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawaua wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi BWANA. 13#Ebr 11:28 Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lolote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri. 14#Kut 23:15; 34:18; Law 23:4,5,6-8; 2 Fal 23:21; Hes 28:17-25; Kum 16:3-8 Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa BWANA; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele 15#1 Kor 5:7; Mwa 17:14; Hes 9:13; 28:17; Kum 16:3 Mtakula mikate isiyochachwa muda wa siku saba; siku hiyo ya kwanza mtaondoa chachu yote isiwe katika nyumba zenu kabisa; kwa kuwa mtu yeyote atakayekula mkate uliochachwa tangu siku hiyo ya kwanza hata siku ya saba, nafsi hiyo atakatiliwa mbali na Israeli. 16Siku ya kwanza kutakuwa kwenu na kusanyiko takatifu, na siku ya saba kutakuwa kusanyiko takatifu; haitafanywa kazi yoyote katika siku hizo, isipokuwa kwa hiyo ambayo kila mtu hana budi kula, hiyo tu ifanyike kwenu. 17#Kut 13:3 Nanyi mtaitunza ile sikukuu ya mikate isiyochachwa; kwa kuwa katika siku iyo hiyo mimi nimeyatoa majeshi yenu katika nchi ya Misri; kwa hiyo mtaitunza siku hiyo katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele. 18#Law 23:5 Mwezi wa kwanza, siku ya mwezi kumi na nne, wakati wa jioni, mtakula mikate isiyochachwa, hata siku ya mwezi ishirini na moja jioni. 19#Kut 23:15; 34:18; Hes 9:13 Muda wa siku saba isionekane chachu katika nyumba zenu kabisa; kwa kuwa mtu yeyote atakayekula hiyo iliyotiwa chachu, nafsi hiyo atakatiliwa mbali na mkutano wa Israeli, akiwa mwenye kukaa kama mgeni, au akiwa mtu aliyezaliwa katika nchi. 20Msile kitu chochote kilichochachwa; mtakula mikate isiyochachwa katika makao yenu yote.
21 #
Hes 9:4; Yos 5:10; Ezr 6:20; Lk 22:7 Hapo ndipo Musa akawaita wazee wa Israeli, na kuwaambia, Nendeni, mkajitwalie wana-kondoo kama jamaa zenu zilivyo mkamchinje kondoo wa Pasaka. 22Nanyi twaeni tawi la hisopo, mkalichovye katika ile damu iliyo bakulini na kukipiga kizingiti cha juu, na miimo miwili ya mlango, kwa hiyo damu iliyo katika bakuli; tena mtu yeyote miongoni mwenu asitoke mlangoni mwa nyumba yake hata asubuhi. 23#Ebr 11:28; Eze 9:6; Ufu 7:3; 9:4; 2 Sam 24:16; 1 Kor 10:10 Kwa kuwa BWANA atapita ili awapige hao Wamisri; na hapo atakapoiona hiyo damu katika kizingiti cha juu, na katika ile miimo miwili, BWANA atapita juu ya mlango, wala hatamwacha mharibifu aingie nyumbani mwenu kuwapiga ninyi. 24Nanyi mtalitunza jambo hili kuwa ni amri kwako na kwa wanao milele. 25Itakuwa hapo mtakapoifikia hiyo nchi, BWANA atakayowapa, kama alivyoahidi, ndipo mtakapoushika utumishi huu. 26#Kut 13:8,14; Kum 32:7; Yos 4:6; Zab 78:6 Kisha itakuwa, hapo watoto wenu watakapowauliza, Ni nini maana yake utumishi huu kwenu? 27Ndipo mtawaambia, Ni dhabihu ya Pasaka ya BWANA, kwa kuwa alipita juu ya nyumba za wana wa Israeli huko Misri, hapo alipowapiga Wamisri, akaziokoa nyumba zetu. Hao watu wakainamisha vichwa na kusujudia. 28Basi wana wa Israeli wakaenda na kufanya mambo hayo; vile vile kama BWANA alivyowaamuru Musa na Haruni, ndivyo walivyofanya.
Baa la kumi: Kufa kwa wazaliwa wote wa kwanza wa Misri
29 #
Kut 4:22-23; Hes 8:17; 33:4; Zab 78:51; 105:36; Isa 37:36 Hata ikawa, usiku wa manane BWANA akawaua wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, tangu mzaliwa wa kwanza wa Farao aliyeketi katika kiti chake cha enzi, hadi mzaliwa wa kwanza wa mtu aliyefungwa katika nyumba ya wafungwa; na wazaliwa wa kwanza wote wa wanyama. 30#Mwa 11:6; Mit 21:13; Eze 7:27; Yak 2:13 Farao akaondoka usiku, yeye na watumishi wake wote, na Wamisri wote; pakawa na kilio kikuu katika Misri; maana hapakuwa na nyumba hata moja asimokufa mtu. 31#Kut 10:9 Akawaita Musa na Haruni usiku, akasema, Ondokeni tokeni katika watu wangu, ninyi na wana wa Israeli; nendeni, kamtumikieni BWANA kama mlivyosema. 32#Mwa 27:34 Twaeni kondoo zenu na ng'ombe zenu kama mlivyosema, nendeni zenu, mkanibariki mimi pia.
Kutoka: Waisraeli watoka Ramesesi hadi Sukothi
33 #
Kut 11:8; Zab 105:38; Mwa 20:3 Wamisri nao wakawahimiza watu, kuwatoa katika nchi kwa haraka, maana walisema, Tumekwisha kufa sote. 34Watu wakauchukua unga wa mikate yao kabla haijatiwa chachu, na vyombo vyao vya kukandia wakavitia ndani ya nguo zao mabegani. 35#Kut 3:21-22; 11:2 Wana wa Israeli wakafanya kama Musa alivyowaagiza; wakataka kwa Wamisri vyombo vya fedha na vyombo vya dhahabu, na mavazi. 36#Mwa 15:14; Kut 3:22 BWANA akawajalia kupendelewa na Wamisri hata wakawapa kila walichokitaka. Nao wakawateka Wamisri nyara.
37 #
Hes 33:3,5; Mwa 47:11; 12:2; 46:3; Kut 38:26; Hes 1:46; 11:21 Wana wa Israeli wakasafiri kutoka Ramesesi mpaka Sukothi, walipata hesabu yao kama watu elfu mia sita wanaume waliokwenda kwa miguu, bila kuhesabu watoto. 38Na kundi kubwa la watu waliochangamana mno wakakwea pamoja nao; na kondoo na ng'ombe, wanyama wengi sana. 39#Kut 6:1; 11:1 Nao wakaoka mikate isiyochachwa ya ule unga waliouchukua walipotoka Misri, maana, haukutiwa chachu, kwa sababu walitolewa watoke Misri, wasiweze kukawia, nao walikuwa hawajajifanyia tayari chakula. 40#Mwa 15:13; Gal 3:17; Mdo 7:6 Muda ambao wana wa Israeli walikaa Misri, ulikuwa ni miaka mia nne na thelathini. 41#Kut 7:4 Ilikuwa mwisho wa miaka hiyo mia nne na thelathini, ilikuwa siku ile ile, majeshi yote ya BWANA yalitoka nchi ya Misri. 42Ni usiku wa kuangaliwa sana mbele za BWANA kwa sababu ya kuwatoa katika nchi ya Misri; huu ndio usiku wa BWANA, ambao wapasa kuangaliwa sana na wana wa Israeli wote katika vizazi vyao.
Maelezo juu ya Pasaka
43 #
Hes 9:14
BWANA akawaambia Musa na Haruni, Amri ya Pasaka ni hii; mtu mgeni asimle; 44#Mwa 17:12,13 lakini mtumishi wa mtu awaye yote aliyenunuliwa kwa fedha, ukiisha kumtahiri, ndipo hapo atamla Pasaka. 45#Law 22:10 Akaaye kwenu kama mgeni, na mtumishi aliyeajiriwa, wasimle Pasaka. 46#Hes 9:12; Yn 19:33,36; Zab 34:20 Na aliwe ndani ya nyumba moja; usiichukue nje ya nyumba nyama yake yoyote; wala msivunje mfupa wake uwao wote. 47Na wafanye jambo hili mkutano wa Israeli wote. 48Na mgeni atakapoketi pamoja nawe, na kupenda kumfanyia BWANA Pasaka, wanaume wake wote watahiriwe, ndipo hapo akaribie na kufanya Pasaka; naye atakuwa mfano mmoja na mtu aliyezaliwa katika nchi; lakini mtu yeyote asiyetahiriwa asimle. 49#Hes 9:14; 15:15; Gal 3:28 Sheria ni hiyo moja kwa mtu aliyezaliwa kwenu, na kwa mgeni akaaye kati yenu ugenini. 50Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli wote; kama BWANA alivyowaagiza Musa na Haruni, ndivyo walivyofanya. 51#Mdo 7:36 Ilikuwa siku ile ile moja, BWANA akawatoa wana wa Israeli katika nchi ya Misri kwa majeshi yao.
Iliyochaguliwa sasa
Kutoka 12: SRUV
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.