Waefeso 3:1-7
Waefeso 3:1-7 SRUV
Kwa sababu hiyo mimi Paulo ni mfungwa wake Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi Mataifa; ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu; ya kwamba kwa kufunuliwa nilijulishwa siri hiyo, kama nilivyotangulia kuandika kwa maneno machache. Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake Kristo. Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii nyakati hizi katika Roho; ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili; Injili hiyo ambayo nilifanywa mhudumu wake, kwa kadiri ya kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa kadiri ya utendaji wa uweza wake.