Waefeso 3:1-7
Waefeso 3:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Kutokana na hayo, mimi Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu kwa ajili yenu, namwomba Mungu. Bila shaka mmekwisha sikia kwamba Mungu, kwa neema yake, alinikabidhi kazi hii niifanye kwa faida yenu. Mimi nilijulishwa kwa njia ya ufunuo mpango wake uliofichika. (Nimeandika kwa ufupi juu ya jambo hili, nanyi mkiyasoma maneno yangu mtaweza kujua jinsi ninavyoielewa siri hiyo ya Kristo). Zamani watu hawakujulishwa siri hiyo; lakini sasa Mungu amewajulisha mitume na manabii wake watakatifu kwa njia ya Roho. Siri yenyewe ni hii: Kwa njia ya Injili watu wa mataifa mengine wanapata sehemu yao pamoja na Wayahudi katika zile baraka za Mungu; wao ni viungo vya mwili uleule, na wanashiriki ahadi ileile aliyofanya Mungu kwa njia ya Kristo Yesu. Mimi nimefanywa kuwa mtumishi wa Injili kwa neema ya pekee aliyonijalia Mungu kwa uwezo wake mkuu.
Waefeso 3:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa sababu hiyo mimi Paulo ni mfungwa wake Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi Mataifa; ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu; ya kwamba kwa kufunuliwa nilijulishwa siri hiyo, kama nilivyotangulia kuandika kwa maneno machache. Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake Kristo. Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii nyakati hizi katika Roho; ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili; Injili hiyo ambayo nilifanywa mhudumu wake, kwa kadiri ya kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa kadiri ya utendaji wa uweza wake.
Waefeso 3:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa sababu hiyo mimi Paulo ni mfungwa wake Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi Mataifa; ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu; ya kwamba kwa kufunuliwa nalijulishwa siri hiyo, kama nilivyotangulia kuandika kwa maneno machache. Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake Kristo. Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho; ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili; Injili hiyo ambayo nalifanywa mhudumu wake, kwa kadiri ya kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa kadiri ya utendaji wa uweza wake.
Waefeso 3:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kwa sababu hii, mimi Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi watu wa Mataifa: Kwa hakika mmekwisha kusikia kuhusu ile huduma ya neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu, yaani, ile siri iliodhihirishwa kwangu kwa njia ya ufunuo, kama nilivyotangulia kuandika kwa kifupi. Kwa kusoma haya, basi mtaweza kuelewa ufahamu wangu katika siri ya Kristo. Siri hii haikudhihirishwa kwa wanadamu katika vizazi vingine kama vile sasa ilivyodhihirishwa na Roho kwa mitume na manabii watakatifu wa Mungu. Siri hii ni kwamba, kwa njia ya Injili, watu wa Mataifa ni warithi pamoja na Israeli, viungo vya mwili mmoja na washiriki pamoja wa ahadi katika Kristo Yesu. Nimekuwa mtumishi wa Injili hii kwa kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa nguvu yake itendayo kazi.