Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu la Torati 9:1-29

Kumbukumbu la Torati 9:1-29 SRUV

Sikiza, Ee Israeli; hivi leo unataka kuvuka Yordani uingie kwa kuwamiliki mataifa yaliyo makubwa, na yenye nguvu kukupita, miji mikubwa iliyojengewa kuta hadi mbinguni, watu wakubwa, warefu, wana wa Waanaki, uwajuao, uliokuwa ukisikia wakitajwa hivi, Ni nani awezaye kusimama mbele ya wana wa Anaki? Basi jua siku hii ya leo kuwa BWANA, Mungu wako, ndiye atanguliaye kuvuka mbele yako kama moto uteketezao; atawaangamiza, tena atawaangusha mbele yako; ndivyo utakapowafukuza na kuwapoteza upesi, kama alivyokuambia BWANA. Usiseme moyoni mwako, BWANA, Mungu wako, atakapokwisha kuwasukumia nje mbele yako, ukasema, Ni kwa haki yangu alivyonitia BWANA niimiliki nchi hii; kwani ni kwa ajili ya uovu wa mataifa haya BWANA anawafukuza nje mbele yako. Si kwa haki yako, wala kwa unyofu wa moyo wako, hivi uingiavyo kuimiliki nchi yao; lakini ni kwa uovu wa mataifa haya BWANA, Mungu wako, awafukuza nje mbele yako; tena apate kuliweka imara hilo neno BWANA alilowaapia baba zako Abrahamu, na Isaka, na Yakobo. Basi jua ya kuwa BWANA, Mungu wako, hakupi nchi hii nzuri uimiliki kwa ajili ya haki yako, kwa maana u taifa lenye shingo ngumu. Kumbuka, usisahau ulivyomtia BWANA, Mungu wako, kasirani jangwani; tangu siku uliyotoka nchi ya Misri hadi mlipofika mahali hapa, mmekuwa na uasi juu ya BWANA Tena mlimkasirisha BWANA katika Horebu, BWANA akakasirika hadi akataka kuwaangamiza. Na hapo nilipokwea mlimani kwenda kuzipokea mbao za mawe, nazo ni mbao za agano BWANA alilofanya nanyi, ndipo nikakaa mle mlimani siku arubaini usiku na mchana; sikula chakula wala kunywa maji. BWANA akanipa vile vimbao viwili vya mawe vilivyoandikwa kwa kidole cha Mungu; na juu yake yameandikwa maneno mfano wa yote aliyosema nanyi BWANA mle mlimani kutoka kati ya moto siku ya mkutano. Ikawa mwisho wa siku arubaini usiku na mchana, BWANA alinipa zile mbao mbili za mawe, nazo ni mbao za agano. BWANA akaniambia, Ondoka huko, shuka upesi; kwa kuwa watu wako uliowatoa Misri wamejiharibu; wamekengeuka mara katika njia niliyowaamuru; wamejifanyia sanamu ya kusubu. Tena BWANA akasema nami zaidi, akaniambia, Nimeliona taifa hili; na tazama, ni taifa lenye shingo ngumu; niache, nipate kuwaangamiza, na kulifuta jina lao chini ya mbingu; nami nitakufanya wewe uwe taifa kubwa lenye nguvu kuliko wao. Basi nikageuka nikashuka mle mlimani, mlima ukawaka moto; na vile zile mbao mbili za agano zilikuwa katika mikono yangu miwili. Nikaangalia, na tazama, mlikuwa mmefanya dhambi juu ya BWANA, Mungu wenu; mmefanya ndama ya ng'ombe ya kusubu; mmepotoka punde katika njia aliyowaamuru BWANA. Nikazishika zile mbao mbili, nikazitupa kutoka katika mikono yangu miwili, nikazivunja mbele ya macho yenu. Nikaanguka chini mbele za BWANA siku arubaini usiku na mchana, kama pale kwanza; sikula chakula wala kunywa maji; kwa sababu ya makosa yenu yote mliyofanya, kwa kufanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, kwa kumkasirisha. Kwa kuwa niliogopa hasira na makamio aliyowakasirikia BWANA kutaka kuwaangamiza. Lakini BWANA alinisikiza wakati huo nao. BWANA akamkasirikia sana Haruni akataka kumwangamiza; nikamwombea Haruni naye wakati huo. Kisha nikaitwaa ile dhambi yenu, huyo ndama mliyemfanya, nikamteketeza kwa moto, nikamponda, nikamsaga tikitiki, hata akawa laini kama vumbi; nikalitupa vumbi lake katika kijito kilichoshuka kutoka mlimani. Tena huko Tabera, na Masa, na Kibroth-hataava mlimtia BWANA hasira. Na wakati alipowatuma BWANA kutoka Kadesh-barnea, akiwaambia, Kweeni mkaimiliki nchi niliyowapa; ndipo mkaasi juu ya maagizo ya BWANA, Mungu wenu, hamkumsadiki wala hamkusikiza sauti yake. Mmekuwa na uasi juu ya BWANA tokea siku nilipowajua ninyi. Ndipo nikaanguka chini mbele za BWANA siku zile arubaini usiku na mchana nilizokuwa nimeanguka chini; kwa kuwa BWANA alisema atawaangamiza. Nikamwomba BWANA, nikasema, Ee Bwana Mungu, usiwaangamize watu wako, urithi wako, uliowakomboa kwa ukuu wako, uliowatoa Misri kwa mkono wa nguvu. Wakumbuke watumishi wako, Abrahamu, na Isaka, na Yakobo; usiangalie ukaidi wa watu hawa, wala uovu wao, wala dhambi yao; isije nchi uliyotutoa ikasema, Ni kwa sababu BWANA hakuweza kuwaleta katika nchi aliyowahidi, tena ni kwa kuwa aliwachukia, aliwatoa nje ili kuwaua jangwani. Nao ni watu wako, urithi wako, uliowatoa kwa nguvu zako kuu na mkono wako ulionyoka.

Video for Kumbukumbu la Torati 9:1-29