Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu la Sheria 9:1-29

Kumbukumbu la Sheria 9:1-29 Biblia Habari Njema (BHN)

“Sikilizeni enyi Waisraeli! Hivi leo mmekaribia kuvuka mto Yordani, kwenda kumiliki nchi ya mataifa makubwa na yenye nguvu kuliko nyinyi. Miji yao ni mikubwa na ina kuta zifikazo mawinguni. Watu wenyewe ni warefu na wenye nguvu; ni Waanaki ambao kama mjuavyo na kama mlivyosikia watu husema juu yao ‘Nani awezaye kuwakabili?’ Jueni leo hii kwamba anayewatangulia kama moto uteketezao miti ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Yeye atawaangamiza hao na kuwashinda mbele yenu; kwa hiyo mtawafukuza na kuwaangamiza mara moja, kama Mwenyezi-Mungu alivyowaahidi. “Baada ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kuwafukuza watu hao mbele yenu, msiseme moyoni mwenu kuwa, ‘Ni kwa sababu ya uadilifu wetu Mwenyezi-Mungu ametuleta tuimiliki nchi hii,’ ambapo Mwenyezi-Mungu amewafukuza watu hawa mbele yenu kwa sababu wao ni waovu. Mnaweza kuimiliki nchi yao si kwa sababu nyinyi ni watu wema au wenye mioyo safi; bali Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawafukuza watu hao mbele yenu kwa sababu ni waovu na anataka kuliweka imara lile neno alilowaapia babu zenu, Abrahamu, Isaka na Yakobo. Basi, jueni ya kuwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawapeni nchi hii nzuri mwimiliki si kwa sababu mnastahili kuimiliki, maana nyinyi ni watu wakaidi. “Kumbukeni na msisahau jinsi mlivyomkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kule jangwani. Tangu siku ile mlipotoka nchi ya Misri mpaka siku mlipofika mahali hapa, nyinyi mmekuwa mkimwasi Mwenyezi-Mungu. Hata huko mlimani Horebu, mlimkasirisha Mwenyezi-Mungu, naye alikasirika sana, kiasi cha kutaka kuwaangamiza. Nilipopanda mlimani kupokea vibao vya mawe ambavyo viliandikwa agano ambalo Mwenyezi-Mungu alifanya nanyi, nilikaa huko siku arubaini, usiku na mchana; sikula wala kunywa chochote. Kisha Mwenyezi-Mungu alinipa vibao viwili vya mawe vilivyoandikwa kwa kidole chake Mungu; vilikuwa vimeandikwa maneno yote ambayo Mwenyezi-Mungu aliwaambieni mlimani kutoka kwenye moto siku ya mkutano. Naam, baada ya siku hizo arubaini, usiku na mchana, Mwenyezi-Mungu alinipa vibao hivyo viwili vya mawe ambavyo viliandikwa agano. “Basi, Mwenyezi-Mungu aliniambia, ‘Ondoka, ushuke chini ya mlima upesi, kwa kuwa watu wako uliowatoa Misri wamepotoka. Wameiacha upesi njia niliyowaamuru wafuate na wamejifanyia sanamu ya kusubu’. “Kadhalika, Mwenyezi-Mungu aliniambia, ‘Nimewaona watu hawa, ni watu wakaidi sana; niache niwaangamize, nilifutilie mbali jina lao duniani; nami nitakufanya wewe kuwa taifa lenye nguvu na kubwa kuliko wao.’ “Basi, niligeuka, nikashuka kutoka mlimani, nikiwa nimebeba vile vibao viwili vya mawe, nao moto ulikuwa unawaka mlimani. Nilitazama, nikaona kwamba tayari mmekwisha kutenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; mlikwisha jitengenezea sanamu ya ndama ya kusubu; bila kukawia mlikwisha iacha njia ya Mwenyezi-Mungu ambayo aliwaamuru. Hivyo, nilivishika vile vibao viwili nikavitupa chini, nikavivunja mbele yenu. Kisha nikalala chini kifudifudi mbele ya Mwenyezi-Mungu, kama hapo awali, kwa muda wa siku arubaini usiku na mchana; sikula chakula wala kunywa maji, kwa sababu ya dhambi mliyokuwa mmetenda kwa kufanya maovu mbele yake Mwenyezi-Mungu kwa kumkasirisha. Niliogopa kwamba hasira na ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu dhidi yenu, ingewaangamiza; lakini Mwenyezi-Mungu alinisikiliza pia wakati huo. Hali kadhalika, Mwenyezi-Mungu alikuwa amemkasirikia sana Aroni, kiasi cha kumwangamiza; hivyo, nikamwombea Aroni wakati huohuo. Kile kitu kiovu, yaani yule ndama mliyejitengenezea, nilikichukua, nikakiteketeza motoni, nikakipondaponda na kukisagasaga, kikawa mavumbi laini; halafu nikayatupa hayo mavumbi kwenye kijito kilichotiririka chini ya mlima huo. “Pia mlimkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, huko Tabera, Masa na Kibroth-hataava. Na Mwenyezi-Mungu alipowatuma kutoka Kadesh-barnea akisema, ‘Nendeni mkaimiliki nchi ambayo nimewapatia,’ mlimwasi; hamkusadiki wala hamkutii yale aliyowaambia. Nyinyi mmekuwa waasi dhidi ya Mwenyezi-Mungu tangu siku nilipowajua. “Kwa hiyo, nililala kifudifudi mbele ya Mwenyezi-Mungu siku hizo arubaini, usiku na mchana, kwa sababu Mwenyezi-Mungu alikuwa amesema atawaangamiza. Nilimwomba Mwenyezi-Mungu, nikisema. ‘Ee Mwenyezi-Mungu, usiwaangamize watu wako na urithi wako, watu uliowakomboa na kuwatoa katika nchi ya Misri kwa uwezo na nguvu yako kubwa. Wakumbuke watumishi wako, Abrahamu, Isaka na Yakobo, wala usiujali ukaidi, uovu na dhambi za watu hawa. Watu wa kule ulikotutoa wasije wakasema, Mwenyezi-Mungu aliwatoa ili awaue jangwani kwa sababu hakuweza kuwaingiza katika nchi aliyowaahidi na kwa sababu aliwachukia. Maana, hawa ni watu wako na urithi wako; watu ambao uliwatoa kutoka Misri kwa nguvu na uwezo wako mkuu.’

Kumbukumbu la Sheria 9:1-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Sikiza, Ee Israeli; hivi leo unataka kuvuka Yordani uingie kwa kuwamiliki mataifa yaliyo makubwa, na yenye nguvu kukupita, miji mikubwa iliyojengewa kuta hadi mbinguni, watu wakubwa, warefu, wana wa Waanaki, uwajuao, uliokuwa ukisikia wakitajwa hivi, Ni nani awezaye kusimama mbele ya wana wa Anaki? Basi jua siku hii ya leo kuwa BWANA, Mungu wako, ndiye atanguliaye kuvuka mbele yako kama moto uteketezao; atawaangamiza, tena atawaangusha mbele yako; ndivyo utakapowafukuza na kuwapoteza upesi, kama alivyokuambia BWANA. Usiseme moyoni mwako, BWANA, Mungu wako, atakapokwisha kuwasukumia nje mbele yako, ukasema, Ni kwa haki yangu alivyonitia BWANA niimiliki nchi hii; kwani ni kwa ajili ya uovu wa mataifa haya BWANA anawafukuza nje mbele yako. Si kwa haki yako, wala kwa unyofu wa moyo wako, hivi uingiavyo kuimiliki nchi yao; lakini ni kwa uovu wa mataifa haya BWANA, Mungu wako, awafukuza nje mbele yako; tena apate kuliweka imara hilo neno BWANA alilowaapia baba zako Abrahamu, na Isaka, na Yakobo. Basi jua ya kuwa BWANA, Mungu wako, hakupi nchi hii nzuri uimiliki kwa ajili ya haki yako, kwa maana u taifa lenye shingo ngumu. Kumbuka, usisahau ulivyomtia BWANA, Mungu wako, kasirani jangwani; tangu siku uliyotoka nchi ya Misri hadi mlipofika mahali hapa, mmekuwa na uasi juu ya BWANA Tena mlimkasirisha BWANA katika Horebu, BWANA akakasirika hadi akataka kuwaangamiza. Na hapo nilipokwea mlimani kwenda kuzipokea mbao za mawe, nazo ni mbao za agano BWANA alilofanya nanyi, ndipo nikakaa mle mlimani siku arubaini usiku na mchana; sikula chakula wala kunywa maji. BWANA akanipa vile vimbao viwili vya mawe vilivyoandikwa kwa kidole cha Mungu; na juu yake yameandikwa maneno mfano wa yote aliyosema nanyi BWANA mle mlimani kutoka kati ya moto siku ya mkutano. Ikawa mwisho wa siku arubaini usiku na mchana, BWANA alinipa zile mbao mbili za mawe, nazo ni mbao za agano. BWANA akaniambia, Ondoka huko, shuka upesi; kwa kuwa watu wako uliowatoa Misri wamejiharibu; wamekengeuka mara katika njia niliyowaamuru; wamejifanyia sanamu ya kusubu. Tena BWANA akasema nami zaidi, akaniambia, Nimeliona taifa hili; na tazama, ni taifa lenye shingo ngumu; niache, nipate kuwaangamiza, na kulifuta jina lao chini ya mbingu; nami nitakufanya wewe uwe taifa kubwa lenye nguvu kuliko wao. Basi nikageuka nikashuka mle mlimani, mlima ukawaka moto; na vile zile mbao mbili za agano zilikuwa katika mikono yangu miwili. Nikaangalia, na tazama, mlikuwa mmefanya dhambi juu ya BWANA, Mungu wenu; mmefanya ndama ya ng'ombe ya kusubu; mmepotoka punde katika njia aliyowaamuru BWANA. Nikazishika zile mbao mbili, nikazitupa kutoka katika mikono yangu miwili, nikazivunja mbele ya macho yenu. Nikaanguka chini mbele za BWANA siku arubaini usiku na mchana, kama pale kwanza; sikula chakula wala kunywa maji; kwa sababu ya makosa yenu yote mliyofanya, kwa kufanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, kwa kumkasirisha. Kwa kuwa niliogopa hasira na makamio aliyowakasirikia BWANA kutaka kuwaangamiza. Lakini BWANA alinisikiza wakati huo nao. BWANA akamkasirikia sana Haruni akataka kumwangamiza; nikamwombea Haruni naye wakati huo. Kisha nikaitwaa ile dhambi yenu, huyo ndama mliyemfanya, nikamteketeza kwa moto, nikamponda, nikamsaga tikitiki, hata akawa laini kama vumbi; nikalitupa vumbi lake katika kijito kilichoshuka kutoka mlimani. Tena huko Tabera, na Masa, na Kibroth-hataava mlimtia BWANA hasira. Na wakati alipowatuma BWANA kutoka Kadesh-barnea, akiwaambia, Kweeni mkaimiliki nchi niliyowapa; ndipo mkaasi juu ya maagizo ya BWANA, Mungu wenu, hamkumsadiki wala hamkusikiza sauti yake. Mmekuwa na uasi juu ya BWANA tokea siku nilipowajua ninyi. Ndipo nikaanguka chini mbele za BWANA siku zile arubaini usiku na mchana nilizokuwa nimeanguka chini; kwa kuwa BWANA alisema atawaangamiza. Nikamwomba BWANA, nikasema, Ee Bwana Mungu, usiwaangamize watu wako, urithi wako, uliowakomboa kwa ukuu wako, uliowatoa Misri kwa mkono wa nguvu. Wakumbuke watumishi wako, Abrahamu, na Isaka, na Yakobo; usiangalie ukaidi wa watu hawa, wala uovu wao, wala dhambi yao; isije nchi uliyotutoa ikasema, Ni kwa sababu BWANA hakuweza kuwaleta katika nchi aliyowahidi, tena ni kwa kuwa aliwachukia, aliwatoa nje ili kuwaua jangwani. Nao ni watu wako, urithi wako, uliowatoa kwa nguvu zako kuu na mkono wako ulionyoka.

Kumbukumbu la Sheria 9:1-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Sikiza, Ee Israeli; hivi leo unataka kuvuka Yordani uingie kwa kuwamiliki mataifa yaliyo makubwa, na yenye nguvu kukupita wewe, miji mikubwa iliyojengewa kuta hata mbinguni, watu wakubwa, warefu, wana wa Waanaki, uwajuao, uliokuwa ukisikia wakitajwa hivi, Ni nani awezaye kusimama mbele ya wana wa Anaki? Basi jua siku hii ya leo kuwa BWANA, Mungu wako, ndiye atanguliaye kuvuka mbele yako kama moto uteketezao; atawaangamiza, tena atawaangusha mbele yako; ndivyo utakavyowafukuza na kuwapoteza upesi, kama alivyokuambia BWANA. Usiseme moyoni mwako, BWANA, Mungu wako, atakapokwisha kuwasukumia nje mbele yako, ukasema, Ni kwa haki yangu alivyonitia BWANA niimiliki nchi hii; kwani ni kwa ajili ya uovu wa mataifa haya BWANA awafukuza nje mbele yako. Si kwa haki yako, wala kwa unyofu wa moyo wako, hivi uingiavyo kuimiliki nchi yao; lakini ni kwa uovu wa mataifa haya BWANA, Mungu wako, awafukuza nje mbele yako; tena apate kuliweka imara hilo neno BWANA alilowaapia baba zako Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo. Basi jua ya kuwa BWANA, Mungu wako, hakupi nchi hii nzuri uimiliki kwa ajili ya haki yako, kwa maana u taifa lenye shingo ngumu. Kumbuka, usisahau ulivyomtia BWANA, Mungu wako, kasirani jangwani; tangu siku uliyotoka nchi ya Misri hata mlipofika mahali hapa, mmekuwa na uasi juu ya BWANA Tena mlimkasirisha BWANA katika Horebu, BWANA akakasirika nanyi hata akataka kuwaangamiza. Na hapo nilipokwea mlimani kwenda kuzipokea mbao za mawe, nazo ni mbao za agano BWANA alilofanya nanyi, ndipo nikakaa mle mlimani siku arobaini usiku na mchana; sikula chakula wala kunywa maji. BWANA akanipa zile mbao mbili za mawe zimeandikwa kwa kidole cha Mungu; na juu yake yameandikwa maneno mfano wa yote aliyosema nanyi BWANA mle mlimani toka kati ya moto siku ya mkutano. Ikawa mwisho wa siku arobaini usiku na mchana, BWANA alinipa zile mbao mbili za mawe, nazo ni mbao za agano. BWANA akaniambia, Ondoka huko, shuka upesi; kwa kuwa watu wako uliowatoa Misri wamejiharibu; wamekengeuka mara katika njia niliyowaamuru; wamejifanyia sanamu ya kusubu. Tena BWANA akasema nami zaidi, akaniambia, Nimeliona taifa hili; na tazama, ni taifa lenye shingo ngumu; niache, nipate kuwaangamiza, na kulifuta jina lao chini ya mbingu; nami nitakufanya wewe uwe taifa kubwa lenye nguvu kuwapita wao. Basi nikageuka nikashuka mle mlimani, mlima ukawaka moto; na zile mbao mbili za agano zilikuwa katika mikono yangu miwili. Nikaangalia, na tazama, mlikuwa mmefanya dhambi juu ya BWANA, Mungu wenu; mmefanya ndama ya ng’ombe ya kusubu; mmekengeuka upesi katika njia aliyowaamuru BWANA. Nikazishika zile mbao mbili, nikazitupa kutoka katika mikono yangu miwili, nikazivunja mbele ya macho yenu. Nikaanguka nchi mbele za BWANA siku arobaini usiku na mchana, kama pale kwanza; sikula chakula wala kunywa maji; kwa sababu ya makosa yenu yote mliyokosa, kwa kufanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, kwa kumkasirisha. Kwa kuwa niliogopa hasira na makamio aliyowakasirikia BWANA kutaka kuwaangamiza. Lakini BWANA alinisikiza wakati huo nao. BWANA akamkasirikia sana Haruni akataka kumwangamiza; nikamwombea Haruni naye wakati huo. Kisha nikaitwaa ile dhambi yenu, huyo ndama mliyemfanya, nikamteketeza kwa moto, nikamponda, nikamsaga tikitiki, hata akawa laini kama vumbi; nikalitupa vumbi lake katika kijito kilichoshuka kutoka mlimani. Tena huko Tabera, na Masa, na Kibroth-hataava mlimtia BWANA hasira. Na wakati alipowatuma BWANA kutoka Kadesh-barnea, akiwaambia, Kweeni mkaimiliki nchi niliyowapa; ndipo mkaasi juu ya maagizo ya BWANA, Mungu wenu, hamkumsadiki wala hamkusikiza sauti yake. Mmekuwa na uasi juu ya BWANA tokea siku nilipowajua ninyi. Ndipo nikaanguka nchi mbele za BWANA siku zile arobaini usiku na mchana nilizokuwa nimeanguka nchi; kwa kuwa BWANA alisema atawaangamiza. Nikamwomba BWANA, nikasema, Ee Bwana Mungu, usiwaangamize watu wako, urithi wako, uliowakomboa kwa ukuu wako, uliowatoa Misri kwa mkono wa nguvu. Wakumbuke watumwa wako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; usiangalie upotofu wa watu hawa, wala uovu wao, wala dhambi yao; isije nchi uliyotutoa ikasema, Ni kwa sababu BWANA hakuweza kuwaleta katika nchi aliyowapa ahadi, tena ni kwa kuwa aliwachukia, alivyowatoa nje ili kuwaua jangwani. Nao ni watu wako, urithi wako, uliowatoa kwa nguvu zako kuu na mkono wako ulionyoka.

Kumbukumbu la Sheria 9:1-29 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Sikiliza, ee Israeli. Sasa mnakaribia kuvuka Yordani mwingie na kuwafukuza mataifa makubwa na yenye nguvu kuliko ninyi pamoja na miji mikubwa yenye kuta zilizofika juu angani. Watu ni wenye nguvu na warefu, ni wana wa Waanaki! Mnafahamu habari zao na mmesikia inavyosemekana: “Ni nani awezaye kusimama dhidi ya Waanaki?” Kuweni na hakika leo kwamba BWANA Mungu wenu ndiye atakayetangulia kuvuka mbele yenu kama moto uteketezao. Atawaangamiza; atawatiisha mbele yenu. Nanyi mtawafukuza na kuwaangamiza mara moja, kama BWANA alivyowaahidi. Baada ya BWANA Mungu wenu kuwafukuza mbele yenu, msiseme mioyoni mwenu, “BWANA ametuleta hapa kuimiliki nchi hii kwa sababu ya haki yetu.” La, ni kwa sababu ya uovu wa mataifa haya ndiyo BWANA anawafukuza mbele yenu. Si kwa sababu ya haki yenu wala uadilifu wenu kwamba mtaimiliki nchi yao; lakini kwa sababu ya uovu wa mataifa haya, BWANA Mungu wenu atawafukuza mbele yenu, ili kutimiza lile alilowaapia baba zenu Abrahamu, Isaki na Yakobo. Basi mjue, si kwa sababu ya haki yenu BWANA Mungu wenu anawapa nchi hii nzuri kuimiliki, kwa kuwa ninyi ni taifa lenye shingo ngumu. Kumbukeni hili, kamwe msisahau jinsi mlivyomkasirisha BWANA Mungu wenu kwa hasira huko jangwani. Tangu siku mlipotoka Misri mpaka mlipofika hapa, mmekuwa waasi dhidi ya BWANA. Kule Horebu mliamsha ghadhabu ya BWANA, kwa hiyo alikasirika vya kutosha hata akataka kuwaangamiza. Nilipopanda mlimani kupokea mbao za mawe, mbao za Agano lile BWANA alilofanya nanyi, nilikaa mlimani siku arobaini usiku na mchana, sikula mkate wala sikunywa maji. BWANA alinipa mbao mbili za mawe zilizoandikwa kwa kidole cha Mungu. Juu ya mbao hizo kulikuwepo amri zote ambazo BWANA aliwatangazia kule mlimani kwa njia ya moto, siku ya kusanyiko. Mwisho wa siku arobaini usiku na mchana, BWANA alinipa mbao mbili za mawe, mbao za Agano. Kisha BWANA akaniambia, “Shuka chini mara moja, kwa sababu watu wako ambao umewatoa katika nchi ya Misri wamepotoka. Wamegeukia mbali haraka kutoka lile nililowaagiza, wamejitengenezea sanamu ya kusubu.” Naye BWANA akaniambia, “Nimewaona watu hawa nao ni watu wenye shingo ngumu sana! Niache, ili nipate kuwaangamiza na kufuta jina lao kutoka chini ya mbingu. Nami nitakufanya kuwa taifa lenye nguvu zaidi na kuwa wengi kuliko wao.” Kwa hiyo niligeuka na kuteremka kutoka mlimani kwani mlima ulikuwa ukiwaka moto. Pia vibao vile viwili vya Agano vilikuwa mikononi mwangu. Nilipotazama, niliona kuwa mmefanya dhambi dhidi ya BWANA Mungu wenu; mmejifanyia sanamu ya kusubu katika umbo la ndama. Mmegeuka upesi kutoka njia ile BWANA aliyowaagiza. Kwa hiyo nilichukua vibao vile viwili nikavitupa na kuvipasua vipande vipande mbele ya macho yenu. Ndipo tena nikasujudu mbele za BWANA kwa siku arobaini usiku na mchana. Sikula mkate wala sikunywa maji, kwa sababu ya dhambi yote mliyoifanya, mkifanya lile lililo ovu mbele za BWANA na kumkasirisha. Niliogopa hasira na ghadhabu ya BWANA, kwa kuwa aliwakasirikia vya kutosha na kutaka kuwaangamiza. Lakini BWANA alinisikiliza tena. Bali yeye alimkasirikia Aroni kiasi cha kutaka kumwangamiza, nami wakati huo nilimwombea Aroni pia. Kisha nikachukua ile sanamu ya ndama mliyoitengeneza na kuichoma kwenye moto. Nikaiponda na kuisaga ikawa unga laini kama vumbi, nikatupa lile vumbi kwenye kijito kilichotiririka toka mlimani. Pia mlimkasirisha BWANA huko Tabera, Masa na Kibroth-Hataava. Vilevile wakati BWANA alipowatuma kutoka Kadesh-Barnea, alisema, “Kweeni, mkaimiliki nchi ambayo nimewapa.” Lakini mliasi dhidi ya agizo la BWANA Mungu wenu. Hamkumtegemea wala kumtii. Mmekuwa waasi dhidi ya BWANA tangu nilipowajua ninyi. Nilianguka kifudifudi mbele za BWANA kwa zile siku arobaini usiku na mchana kwa sababu BWANA alikuwa amesema angewaangamiza ninyi. Nilimwomba BWANA na kusema, “Ee BWANA Mwenyezi, usiangamize watu wako, urithi wako mwenyewe ule ulioukomboa kwa uweza wako mkuu na kuwatoa katika nchi ya Misri kwa mkono wenye nguvu. Wakumbuke watumishi wako Abrahamu, Isaki na Yakobo. Usiangalie ukaidi wa watu hawa, uovu wao wala dhambi yao. Watu wa nchi ile uliyotutoa sisi wasije wakasema, ‘Ni kwa sababu BWANA hakuweza kuwachukua mpaka nchi aliyokuwa amewaahidia, kwa sababu aliwachukia, akawaleta ili aje kuwaua jangwani.’ Bali wao ni watu wako, urithi wako ule ulioutoa Misri kwa uweza wako mkuu na kwa mkono wako ulionyooka.”