Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 27:1-12

Matendo 27:1-12 SRUV

Basi ilipoamriwa tuabiri hadi Italia, wakamtia Paulo na wafungwa wengine katika mikono ya ofisa mmoja, jina lake Yulio, wa kikosi cha Augusto. Tukapanda katika merikebu ya Adramitio iliyokuwa tayari kusafiri mpaka miji ya pwani za Asia, tukatweka; Aristarko, Mmakedonia wa Thesalonike, akiwa pamoja nasi. Siku iliyofuata tukawasili Sidoni; Yulio akamfadhili sana Paulo akampa ruhusa kwenda kwa rafiki zake, apate kutunzwa. Kutoka huko tukiwa baharini, tukasafiri chini ya Kipro ili kujikinga upepo, kwa maana upepo ulikuwa unatukabili. Tulipopita bahari ya upande wa Kilikia na Pamfilia, tukafika Mira, mji wa Likia. Na huko yule ofisa akakuta merikebu ya Aleksandria, tayari kusafiri kwenda Italia, akatupandisha humo. Tukasafiri polepole kwa muda wa siku nyingi, tukafika mpaka Nido kwa shida; na kwa sababu upepo ulikuwa ukituzuia tukapita chini ya Krete, tukaikabili Salmone. Tukaipita kwa shida, pwani kwa pwani, tukafika mahali paitwapo Bandari Nzuri. Karibu na hapo pana mji uitwao Lasea. Na wakati mwingi ulipokwisha kupita, na safari ikiwa ina hatari sasa, kwa sababu siku za kufunga zilikuwa zimekwisha kupita, Paulo akawaonya, akawaambia, Wanaume, naona kwamba safari hii itakuwa na madhara na hasara nyingi, si ya shehena na merikebu tu, ila na ya maisha yetu pia. Lakini yule ofisa akawasikiliza nahodha na mwenye merikebu zaidi ya yale aliyoyasema Paulo. Na kwa sababu bandari ile ilikuwa haifai kukaa wakati wa baridi, wengi wao wakatoa shauri la kutweka kutoka huko ili wapate kufika Foinike, kama ikiwezekana, na kukaa huko wakati wa baridi; nayo ni bandari ya Krete, inaelekea kaskazini mashariki na kusini mashariki.

Soma Matendo 27

Video ya Matendo 27:1-12