Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 27:1-12

Matendo 27:1-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ilipoamuliwa kwamba tungesafiri kwa njia ya bahari kwenda Italia, Paulo na wafungwa wengine wakakabidhiwa kwa kiongozi mmoja wa askari aliyeitwa Juliasi, aliyekuwa wa Kikosi cha Walinzi wa Kaisari. Tulipanda meli iliyotoka Adramitio, iliyokuwa inakaribia kusafiri kwenda kwenye bandari zilizopo pwani ya Asia, tukaanza safari yetu tukiwa pamoja na Aristarko, Mmakedonia kutoka Thesalonike. Kesho yake tukatia nanga Sidoni, naye Juliasi akamfanyia wema Paulo, akamruhusu aende kwa rafiki zake ili wamtimizie mahitaji yake. Kutoka huko tukaingia baharini tena na tukapita upande wa chini wa kisiwa cha Kipro kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho. Baada ya sisi kuvuka bahari iliyoko upande wa Kilikia na Pamfilia, tukafika Mira huko Likia. Huko yule kiongozi wa askari akapata meli ya Iskanderia ikielekea Italia, akatupandisha humo. Tukasafiri polepole kwa siku nyingi na kwa shida, hatimaye tukafika karibu na Nido. Kwa kuwa upepo wa mbisho ulituzuia tusiweze kushika mwelekeo tuliokusudia, tukapita chini ya Krete mkabala na Salmone. Tukaambaa na pwani kwa shida, tukafika sehemu iitwayo Bandari Nzuri, karibu na mji wa Lasea. Muda mwingi ulikuwa umepotea na kusafiri baharini kulikuwa hatari kwa sababu wakati huu ulikuwa baada ya siku za kufunga. Hivyo Paulo akawaonya akasema, “Mabwana, naona kuwa hii safari ni yenye maafa na ya kuleta hasara kubwa kwa meli na shehena, pia kwa maisha yetu.” Lakini badala ya yule kiongozi wa askari kusikiliza yale Paulo aliyosema, akafuata zaidi ushauri wa nahodha na mwenye meli. Kwa kuwa ile bandari ilikuwa haifai kukaa wakati wa majira ya baridi, wengi wakashauri kwamba tuendelee na safari wakitarajia kufika Foinike na kukaa huko kwa majira ya baridi. Hii ilikuwa bandari iliyoko katika kisiwa cha Krete ikikabili upande wa kusini-magharibi na kaskazini-magharibi.

Shirikisha
Soma Matendo 27

Matendo 27:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

Walipokwisha amua tusafiri mpaka Italia, walimweka Paulo pamoja na wafungwa wengine chini ya ulinzi wa Yulio aliyekuwa ofisa wa jeshi katika kikosi kiitwacho “Kikosi cha Augusto.” Tulipanda meli ya Adiramito iliyokuwa inasafiri na kupitia bandari kadhaa za mkoa wa Asia, tukaanza safari. Aristarko, mwenyeji wa Makedonia kutoka Thesalonike, alikuwa pamoja nasi. Kesho yake tulitia nanga katika bandari ya Sidoni. Yulio alimtendea Paulo vizuri kwa kumruhusu awaone rafiki zake na kupata mahitaji yake. Kutoka huko tuliendelea na safari, lakini kwa kuwa upepo ulikuwa unavuma kwa kasi kutujia kwa mbele, tulipitia upande wa kisiwa cha Kupro ambapo upepo haukuwa mwingi. Halafu tulivuka bahari ya Kilikia na Pamfulia, tukatia nanga Mura, mji wa Lukia. Hapo yule ofisa alikuta meli moja ya Aleksandria iliyokuwa inakwenda Italia, na hivyo akatupandisha ndani. Kwa muda wa siku nyingi tulisafiri polepole, na kwa shida tulifika karibu na Nido. Kwa sababu upepo ulikuwa bado unatupinga, tuliendelea mbele moja kwa moja tukapitia upande wa Krete karibu na rasi Salmone ambapo upepo haukuwa mwingi. Tulipita kando yake polepole tukafika mahali paitwapo “Bandari Nzuri,” karibu na mji wa Lasea. Muda mrefu ulikuwa umepita, na hata siku ya kufunga ilikuwa imekwisha pita. Sasa ilikuwa hatari sana kusafiri kwa meli. Basi, Paulo aliwapa onyo: “Waheshimiwa, nahisi kwamba safari hii itakuwa ya shida na hasara nyingi si kwa shehena na meli tu, bali pia kwa maisha yetu.” Lakini yule ofisa alivutiwa zaidi na maoni ya nahodha na ya mwenye meli kuliko yale aliyosema Paulo. Kwa kuwa bandari hiyo haikuwa mahali pazuri pa kukaa wakati wa baridi, wengi walipendelea kuendelea na safari, ikiwezekana mpaka Foinike. Foinike ni bandari ya Krete inayoelekea kusini-magharibi na kaskazini-magharibi; na huko wangeweza kukaa wakati wa baridi.

Shirikisha
Soma Matendo 27

Matendo 27:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi ilipoamriwa tuabiri hadi Italia, wakamtia Paulo na wafungwa wengine katika mikono ya ofisa mmoja, jina lake Yulio, wa kikosi cha Augusto. Tukapanda katika merikebu ya Adramitio iliyokuwa tayari kusafiri mpaka miji ya pwani za Asia, tukatweka; Aristarko, Mmakedonia wa Thesalonike, akiwa pamoja nasi. Siku iliyofuata tukawasili Sidoni; Yulio akamfadhili sana Paulo akampa ruhusa kwenda kwa rafiki zake, apate kutunzwa. Kutoka huko tukiwa baharini, tukasafiri chini ya Kipro ili kujikinga upepo, kwa maana upepo ulikuwa unatukabili. Tulipopita bahari ya upande wa Kilikia na Pamfilia, tukafika Mira, mji wa Likia. Na huko yule ofisa akakuta merikebu ya Aleksandria, tayari kusafiri kwenda Italia, akatupandisha humo. Tukasafiri polepole kwa muda wa siku nyingi, tukafika mpaka Nido kwa shida; na kwa sababu upepo ulikuwa ukituzuia tukapita chini ya Krete, tukaikabili Salmone. Tukaipita kwa shida, pwani kwa pwani, tukafika mahali paitwapo Bandari Nzuri. Karibu na hapo pana mji uitwao Lasea. Na wakati mwingi ulipokwisha kupita, na safari ikiwa ina hatari sasa, kwa sababu siku za kufunga zilikuwa zimekwisha kupita, Paulo akawaonya, akawaambia, Wanaume, naona kwamba safari hii itakuwa na madhara na hasara nyingi, si ya shehena na merikebu tu, ila na ya maisha yetu pia. Lakini yule ofisa akawasikiliza nahodha na mwenye merikebu zaidi ya yale aliyoyasema Paulo. Na kwa sababu bandari ile ilikuwa haifai kukaa wakati wa baridi, wengi wao wakatoa shauri la kutweka kutoka huko ili wapate kufika Foinike, kama ikiwezekana, na kukaa huko wakati wa baridi; nayo ni bandari ya Krete, inaelekea kaskazini mashariki na kusini mashariki.

Shirikisha
Soma Matendo 27

Matendo 27:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi ilipoamriwa tuabiri hata Italia, wakamtia Paulo na wafungwa wengine katika mikono ya akida mmoja, jina lake Yulio, wa kikosi cha Augusto. Tukapanda katika merikebu ya Adramitio iliyokuwa tayari kusafiri mpaka miji ya pwani za Asia, tukatweka; Aristarko, Mmakedonia wa Thesalonike, akiwa pamoja nasi. Siku ya pili tukawasili Sidoni; Yulio akamfadhili sana Paulo akampa ruhusa kwenda kwa rafiki zake, apate kutunzwa. Kutoka huko tukatweka, tukasafiri chini ya Kipro ili kuukinga upepo, kwa maana pepo zilikuwa za mbisho. Tulipopita bahari ya upande wa Kilikia na Pamfilia, tukafika Mira, mji wa Likia. Na huko yule akida akakuta merikebu ya Iskanderia, tayari kusafiri kwenda Italia, akatupandisha humo. Tukasafiri polepole kwa muda wa siku nyingi, tukafika mpaka Nido kwa shida; na kwa sababu upepo ulikuwa ukituzuia tukapita chini ya Krete, tukaikabili Salmone. Tukaipita kwa shida, pwani kwa pwani, tukafika mahali paitwapo Bandari Nzuri. Karibu na hapo pana mji uitwao Lasea. Na wakati mwingi ulipokwisha kupita, na safari ikiwa ina hatari sasa, kwa sababu siku za kufunga zilikuwa zimekwisha kupita, Paulo akawaonya, akawaambia, Wanaume, naona kwamba safari hii itakuwa na madhara na hasara nyingi, si ya shehena na merikebu tu, ila na ya maisha yetu pia. Lakini yule akida akawasikiliza nahodha na mwenye merikebu zaidi ya yale aliyoyasema Paulo. Na kwa sababu bandari ile ilikuwa haifai kukaa wakati wa baridi, wengi wao wakatoa shauri la kutweka kutoka huko ili wapate kufika Foinike, kama ikiwezekana, na kukaa huko wakati wa baridi; nayo ni bandari ya Krete, inaelekea kaskazini-mashariki na kusini-mashariki.

Shirikisha
Soma Matendo 27