Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 27:1-12

Matendo 27:1-12 NEN

Ilipoamuliwa kwamba tungesafiri kwa njia ya bahari kwenda Italia, Paulo na wafungwa wengine wakakabidhiwa kwa kiongozi mmoja wa askari aliyeitwa Juliasi, aliyekuwa wa Kikosi cha Walinzi wa Kaisari. Tulipanda meli iliyotoka Adramitio, iliyokuwa inakaribia kusafiri kwenda kwenye bandari zilizopo pwani ya Asia, tukaanza safari yetu tukiwa pamoja na Aristarko, Mmakedonia kutoka Thesalonike. Kesho yake tukatia nanga Sidoni, naye Juliasi akamfanyia wema Paulo, akamruhusu aende kwa rafiki zake ili wamtimizie mahitaji yake. Kutoka huko tukaingia baharini tena na tukapita upande wa chini wa kisiwa cha Kipro kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho. Baada ya sisi kuvuka bahari iliyoko upande wa Kilikia na Pamfilia, tukafika Mira huko Likia. Huko yule kiongozi wa askari akapata meli ya Iskanderia ikielekea Italia, akatupandisha humo. Tukasafiri polepole kwa siku nyingi na kwa shida, hatimaye tukafika karibu na Nido. Kwa kuwa upepo wa mbisho ulituzuia tusiweze kushika mwelekeo tuliokusudia, tukapita chini ya Krete mkabala na Salmone. Tukaambaa na pwani kwa shida, tukafika sehemu iitwayo Bandari Nzuri, karibu na mji wa Lasea. Muda mwingi ulikuwa umepotea na kusafiri baharini kulikuwa hatari kwa sababu wakati huu ulikuwa baada ya siku za kufunga. Hivyo Paulo akawaonya akasema, “Mabwana, naona kuwa hii safari ni yenye maafa na ya kuleta hasara kubwa kwa meli na shehena, pia kwa maisha yetu.” Lakini badala ya yule kiongozi wa askari kusikiliza yale Paulo aliyosema, akafuata zaidi ushauri wa nahodha na mwenye meli. Kwa kuwa ile bandari ilikuwa haifai kukaa wakati wa majira ya baridi, wengi wakashauri kwamba tuendelee na safari wakitarajia kufika Foinike na kukaa huko kwa majira ya baridi. Hii ilikuwa bandari iliyoko katika kisiwa cha Krete ikikabili upande wa kusini-magharibi na kaskazini-magharibi.

Video ya Matendo 27:1-12