Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 10:1-33

Matendo 10:1-33 SRUV

Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, jemadari wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima. Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamkodolea macho, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu. Sasa basi, tuma watu Yafa, ukamwite Simoni, aitwaye Petro. Yeye ni mgeni wa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi, ambaye nyumba yake iko pwani, atakuambia yakupasayo kutenda. Na yule malaika aliyesema naye akiisha kuondoka, Kornelio akawaita watumishi wake wawili wa nyumbani, na askari mmoja, mtu mtauwa kati ya wale waliomhudumia daima; na alipokwisha kuwaeleza mambo yote akawatuma kwenda Yafa. Hata siku ya pili, walipokuwa wakisafiri na kuukaribia mji, Petro alipanda juu darini, kwenda kuomba, yapata saa sita ya mchana; akaumwa na njaa sana, akataka kula; lakini walipokuwa wakiandaa, roho yake ikazimia, akaona mbingu zimefunuka, na chombo kikishuka kama nguo kubwa, inateremshwa kwa pembe zake nne hadi chini; ambayo ndani yake walikuwamo aina zote za wanyama wenye miguu minne, na hao watambaao, na ndege wa angani. Kisha sauti ikamjia, kusema, Inuka, Petro, uchinje ule. Lakini Petro akasema, La, hasha! Bwana, kwa maana sijawahi kula kitu kilicho kichafu au najisi. Sauti ikamjia mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi. Jambo hili likatendeka mara tatu; kisha kile chombo kikapokewa tena mbinguni. Wakati Petro alipokuwa akisumbuka ndani ya nafsi yake, juu ya maana ya maono hayo aliyoyaona, wale watu waliotumwa na Kornelio, wakatokeza. Walikuwa kukiulizia nyumba ya Simoni, wakiwa wamesimama mbele ya lango, wakaita; wakauliza kama Simoni aitwaye Petro anakaa humo. Na Petro alikuwa akiyafikiri yale maono. Roho akamwambia, Wako watu watatu wanakutafuta. Basi inuka ushuke ufuatane nao, usione tashwishi, kwa maana ni mimi niliyewatuma. Petro akawashukia wale watu, akanena, Mimi ndiye mnayemtafuta. Mmekuja kwa sababu gani? Wakasema, Kornelio jemadari, mtu mwenye haki, mchaji wa Mungu, aliye na sifa njema kwa taifa lote la Wayahudi, alionywa na malaika mtakatifu kutuma watu kwako, uende nyumbani kwake, ili asikilize kile utakachosema. Akawakaribisha wawe wageni wake. Hata siku ya pili, Petro akaondoka akatoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu waliokaa Yafa wakafuatana naye. Kesho yake wakaingia Kaisaria. Na Kornelio alikuwa akiwangojea, akiwa amekusanya jamaa zake na rafiki zake. Petro alipokuwa akiingia Kornelio akatoka amlaki akamwangukia miguuni mwake, akamsujudia. Lakini Petro akamwinua, akasema, Simama, mimi nami ni mwanadamu. Na katika kusema naye akaingia ndani, akaona watu wengi wamekusanyika. Akawaambia, Ninyi mnajua ya kuwa si halali kwa mtu aliye Myahudi ashirikiane na mtu wa taifa lingine wala kumtembelea, lakini Mungu amenionya, nisimwite mtu yeyote mchafu wala najisi. Kwa sababu hiyo nilikuja nilipoitwa, nisikatae; basi nawauliza, ni neno gani mliloniitia? Kornelio akasema, Siku tatu zilizopita, katika saa ii hii, yaani saa tisa, nilikuwa nikisali nyumbani mwangu; nikamwona mtu amesimama mbele yangu, akiwa amevaa nguo zinazong'aa, akasema, Kornelio, kuomba kwako kumesikiwa, na sadaka zako zinakumbukwa mbele za Mungu. Basi, tuma watu kwenda Yafa, ukamwite Simoni aitwaye Petro, anakaa katika nyumba ya Simoni, mtengenezaji wa ngozi, karibu na pwani; naye akija atasema nawe. Mara nikatuma watu kwako, nawe umefanya vyema kuja. Basi sasa sisi sote tupo hapa mbele za Mungu, tupate kuyasikiliza maneno yote uliyoamriwa na Bwana.

Soma Matendo 10

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Matendo 10:1-33

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha