Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 10:1-33

Matendo 10:1-33 NEN

Katika mji wa Kaisaria palikuwa na mtu jina lake Kornelio, ambaye alikuwa jemadari wa kile kilichojulikana kama kikosi cha Kiitalia. Yeye alikuwa mcha Mungu pamoja na wote wa nyumbani mwake. Aliwapa watu sadaka nyingi na kumwomba Mungu daima. Siku moja alasiri, yapata saa tisa, aliona maono waziwazi, malaika wa Mungu akimjia na kumwambia, “Kornelio!” Kornelio akamkazia macho kwa hofu akasema, “Kuna nini, Bwana?” Malaika akamwambia, “Sala zako na sadaka zako kwa maskini zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu. Sasa tuma watu waende Yafa wakamwite mtu mmoja jina lake Simoni aitwaye Petro. Yeye anaishi na Simoni mtengenezaji ngozi ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.” Yule malaika aliyekuwa akizungumza naye alipoondoka, Kornelio akawaita watumishi wake wawili pamoja na askari mmoja mcha Mungu aliyekuwa miongoni mwa wale waliomtumikia. Akawaambia mambo yote yaliyotukia, kisha akawatuma waende Yafa. Siku ya pili yake, walipokuwa wameukaribia mji, wakati wa adhuhuri, Petro alipanda juu ya nyumba kuomba. Alipokuwa akiomba akahisi njaa, akatamani kupata chakula. Lakini wakati walikuwa wakiandaa chakula, akalala usingizi mzito sana. Akaona mbingu zimefunguka na kitu kama nguo kubwa kikishushwa duniani kwa ncha zake nne. Ndani yake walikuwepo aina zote za wanyama wenye miguu minne, nao watambaao nchini, na ndege wa angani. Ndipo sauti ikamwambia “Petro, ondoka, uchinje na ule.” Petro akajibu, “La hasha Bwana! Sijawahi kamwe kula kitu chochote kilicho najisi.” Ile sauti ikasema naye mara ya pili, “Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.” Jambo hili lilitokea mara tatu na ghafula ile nguo ikarudishwa mbinguni. Wakati Petro akiwa bado anajiuliza kuhusu maana ya maono haya, wale watu waliokuwa wametumwa na Kornelio wakaipata nyumba ya Simoni mtengenezaji wa ngozi wakawa wamesimama mbele ya lango. Wakabisha hodi na kuuliza kama Simoni aliyeitwa Petro alikuwa anaishi hapo. Wakati Petro akiwa anafikiria juu ya yale maono, Roho Mtakatifu akamwambia, “Simoni, wako watu watatu wanaokutafuta. Inuka na ushuke, usisite kwenda nao kwa kuwa mimi nimewatuma.” Petro akashuka na kuwaambia wale watu waliokuwa wametumwa kutoka kwa Kornelio, “Mimi ndiye mnayenitafuta. Mmekuja kwa sababu gani?” Wale watu wakamjibu, “Tumetumwa na Kornelio yule jemadari. Yeye ni mtu mwema anayemcha Mungu, na anaheshimiwa na Wayahudi wote. Yeye ameagizwa na malaika mtakatifu akukaribishe nyumbani kwake, ili asikilize maneno utakayomwambia.” Basi Petro akawakaribisha wakafuatana naye ndani, akawapa pa kulala. Kesho yake akaondoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu kutoka Yafa wakafuatana naye. Siku iliyofuata wakawasili Kaisaria. Kornelio alikuwa akiwangoja pamoja na jamaa yake na marafiki zake wa karibu. Petro alipokuwa akiingia ndani, Kornelio alikuja kumlaki, akaanguka miguuni pake kwa heshima. Lakini Petro akamwinua akamwambia, “Simama, mimi ni mwanadamu tu.” Petro alipokuwa akizungumza naye akaingia ndani na kukuta watu wengi wamekusanyika. Akawaambia, “Mnajua kabisa kwamba ni kinyume cha sheria yetu Myahudi kuchangamana na mtu wa Mataifa au kumtembelea. Lakini Mungu amenionyesha kwamba nisimwite mtu yeyote kuwa najisi au asiye safi. Ndiyo sababu ulipotuma niitwe nilikuja bila kupinga lolote. Basi sasa naomba unieleze kwa nini umeniita?” Kornelio akajibu, “Siku nne zilizopita, nilikuwa nyumbani nikisali saa kama hii, saa tisa alasiri. Ghafula mtu aliyevaa nguo zilizongʼaa akasimama mbele yangu, akasema, ‘Kornelio, maombi yako yamesikiwa na sadaka zako kwa maskini zimekumbukwa mbele za Mungu. Basi tuma watu waende Yafa wakaulize mtu mmoja Simoni aitwaye Petro, yeye ni mgeni katika nyumba ya Simoni mtengenezaji ngozi, ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.’ Nilituma watu kwako mara moja, nawe umefanya vyema kuja. Basi sasa sisi sote tuko hapa mbele za Mungu kuyasikiliza yote ambayo Bwana amekuamuru kutuambia.”

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Matendo 10:1-33

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha