2 Samweli 17:1-14
2 Samweli 17:1-14 SRUV
Zaidi ya hayo Ahithofeli akamwambia Absalomu, Niache nichague watu elfu kumi na mbili, nami nitaondoka na kumfuatia Daudi usiku huu; nami nitamshambulia wakati atakaokuwa amechoka, na mikono yake imekuwa dhaifu, nami nitamtia hofu; na watu wote walio pamoja naye watakimbia; nami nitampiga mfalme peke yake; na hao watu wote nitawarejesha kwako; kama bibi arusi anavyorudi nyumbani kwa mumewe. Kurudi kwa yule mtu umtafutaye ni kana kurudi kwa wote; maana watu wote watakuwa katika amani. Shauri hili likawa jema machoni pa Absalomu, na machoni pa wazee wote wa Israeli. Ndipo Absalomu akasema, Basi, mwiteni Hushai, Mwarki, naye, tukasikie atakayosema yeye pia. Basi Hushai alipofika kwa Absalomu, Absalomu akamwambia, akasema, Ahithofeli amesema hivi; je! Tufanye kama alivyosema? Kama sivyo, sema maneno yako. Hushai akamwambia Absalomu, Ushauri huu alioutoa Ahithofeli si mwema wakati huu. Hushai akaendelea kusema, Unamjua baba yako na watu wake, ya kuwa ni watu mashujaa hawa, nao wana uchungu katika mioyo yao, kama dubu aliyenyang'anywa watoto wake nyikani; tena baba yako ni mtu wa vita, hatalala pamoja na watu wake. Angalia, amefichwa sasa katika shimo, au penginepo; kisha itakuwa, watakapoanguka baadhi yao mwanzo, kila mtu atakayesikia, atasema, Kuna mauaji katika watu wanaofuatana na Absalomu. Basi hata yeye aliye shujaa, mwenye moyo kama moyo wa simba, atayeyuka kabisa; maana Israeli wote wanajua ya kuwa baba yako ni shujaa, na ya kuwa watu wale walio pamoja naye ni mashujaa. Kwa hiyo shauri langu ni hili, Waisraeli wote toka Dani mpaka Beer-sheba wakusanyike kwako, kama mchanga wa bahari kwa wingi; na wewe uende vitani mwenyewe. Hivyo tutamfikia mahali popote atakapoonekana, na kumwangukia kama vile umande uangukavyo juu ya nchi; wala hatutaacha hata mmoja wao, yeye na watu wote walio pamoja naye. Tena, ikiwa amejitia katika mji wowote ule, basi Israeli wote wataleta kamba, na kuuendea mji ule, nasi tutaukokota mpaka mtoni, wala halitaonekana huko hata jiwe dogo moja la mawe yake. Naye Absalomu na watu wote wa Israeli wakasema, Ushauri wa Hushai, Mwarki, ni mwema kuliko ushauri wa Ahithofeli. Kwa maana BWANA alikuwa amekusudia kuuvunja ushauri mwema wa Ahithofeli, ili BWANA alete mabaya juu ya Absalomu.