2 Samweli 17:1-14
2 Samweli 17:1-14 NENO
Ahithofeli akamwambia Absalomu, “Nipe ruhusa niwachague watu elfu kumi na mbili, nao waanze safari usiku huu huu kumfuatia Daudi. Nitamshambulia wakati akiwa amechoka na ni dhaifu. Nitampiga na hofu, na kisha watu wote walio pamoja naye watakimbia. Nitampiga mfalme peke yake na kuwarudisha watu wote kwako. Kifo cha mtu yule unayemtafuta kitamaanisha kurudi kwa wote, hakuna hata mtu mmoja atakayeumizwa.” Mpango huu ulionekana mzuri kwa Absalomu na kwa wazee wote wa Israeli. Lakini Absalomu akasema, “Pia mwiteni Hushai, Mwarki, ili tuweze kusikia anachokisema.” Hushai alipokuja, Absalomu akasema, “Ahithofeli ametoa ushauri huu. Je, tufanye anavyosema? Kama sivyo, tupe maoni yako.” Hushai akamjibu Absalomu, “Ushauri alioutoa Ahithofeli haufai kwa wakati huu. Unamfahamu baba yako na watu wake, ni wapiganaji hodari, nao ni wakali kama dubu aliyepokonywa watoto wake. Zaidi ya hayo, baba yako ni mpiganaji jasiri, usiku hatalala pamoja na vikosi. Hata sasa, amefichwa ndani ya pango au mahali pengine. Kama atatangulia kushambulia vikosi vyako, yeyote asikiaye habari hii atasema, ‘Kuna machinjo makubwa miongoni mwa vikosi vinavyomfuata Absalomu.’ Basi hata yule askari hodari kuliko wengine wote, ambaye moyo wake ni kama wa simba, atayeyuka kwa hofu, kwa maana Israeli yote wanajua kwamba baba yako ni mpiganaji na kwamba wale walio pamoja naye ni watu hodari. “Kwa hiyo nakushauri: Israeli wote na wakusanyike kwako, kuanzia Dani hadi Beer-Sheba, wakiwa wengi kama mchanga wa ufuo wa bahari; wakusanyike kwako, nawe ukiwaongoza vitani. Ndipo tutakapomshambulia popote atakapoonekana, nasi tutamwangukia kama umande unavyoshuka juu ya ardhi. Yeye mwenyewe na watu wake hakuna atakayeachwa hai. Kama atakimbilia katika mji wowote, basi Israeli wote watazungushia mji ule kamba, nasi tutauburuta mji huo hadi bondeni, wala isionekane hata changarawe ya huo mji.” Absalomu na wanaume wote wa Israeli wakasema, “Ushauri wa Hushai, Mwarki, ni mwema kuliko ule wa Ahithofeli.” Kwa maana Mwenyezi Mungu alikuwa amekusudia kupinga ushauri mwema wa Ahithofeli, ili kuleta maafa kwa Absalomu.