Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 12:13-23

2 Samweli 12:13-23 SRUV

Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia BWANA dhambi. Nathani akamwambia Daudi, BWANA naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa. Lakini, kwa kuwa kwa tendo hili umewapa adui za BWANA nafasi kubwa ya kukufuru, mtoto atakayezaliwa kwako hakika atakufa. Naye Nathani akaondoka kwenda nyumbani kwake. Basi BWANA akampiga yule mtoto ambaye mkewe Uria alimzalia Daudi naye akawa mgonjwa sana. Basi Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto; Daudi akafunga, akaingia, akalala chini usiku kucha. Nao wazee wa nyumba yake wakaondoka, wakasimama karibu naye, ili wamwinue kutoka chini; lakini hakukubali, wala hakula chakula pamoja nao. Ikawa siku ya saba, yule mtoto akafa. Nao watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia ya kuwa mtoto amekufa, maana, walisema, Angalieni, yule mtoto alipokuwa angali hai, tulisema naye, asitusikilize sauti zetu; si atajidhuru, tukimwambia ya kuwa mtoto amekufa? Lakini alipoona ya kuwa watumishi wake wananong'onezana, Daudi alitambua ya kuwa mtoto amekufa; basi Daudi akawauliza watumishi wake, Je! Mtoto amekufa? Nao wakasema, Amekufa. Ndipo Daudi akainuka pale chini akaoga, akajipaka mafuta, akabadili mavazi yake; akaingia nyumbani mwa BWANA, akasali; kisha akaenda nyumbani kwake, na alipotaka wakamwandalia chakula, naye akala. Watumishi wake wakamwambia, Ni jambo gani hili ulilolitenda? Ulifunga na kulia kwa ajili ya mtoto, alipokuwa hai; lakini mtoto alipokuwa amekufa, uliinuka ukala chakula. Akasema, Mtoto alipokuwa hai, nilifunga, nikalia; kwa maana nilisema, Ni nani ajuaye kama BWANA atanihurumia, mtoto apate kuishi? Lakini sasa amekufa nifungie nini? Je! Naweza kumrudisha tena? Mimi nitakwenda kwake lakini yeye hatanirudia mimi.