Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samueli 12:13-23

2 Samueli 12:13-23 Biblia Habari Njema (BHN)

Basi, Daudi akamwambia Nathani, “Nimetenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu.” Nathani akamwambia, “Mwenyezi-Mungu amekusamehe dhambi yako, nawe hutakufa. Hata hivyo, kwa kuwa kwa tendo lako umemdharau kabisa Mwenyezi-Mungu, mtoto wako atakufa.” Kisha Nathani akarudi nyumbani kwake. Mwenyezi-Mungu alimpiga mtoto ambaye Bathsheba mkewe Uria alimzalia Daudi, naye akawa mgonjwa. Daudi alimwomba Mungu mtoto apate nafuu. Alikwenda chumbani kwake, na usiku kucha akalala sakafuni. Wazee waliokuwa wanamwangalia katika jumba hilo walimfuata na kumsihi aamke, lakini yeye alikataa, na hakula chakula chochote pamoja nao. Juma moja baadaye, mtoto huyo akafa. Watumishi wa Daudi waliogopa kumwambia kuwa mtoto amekufa, kwani walifikiri, “Mtoto huyo alipokuwa hai, tulizungumza naye, lakini hakutusikiliza. Sasa, tutamwambiaje kuwa mtoto wake amekufa? Huenda akajidhuru.” Daudi alipowaona watumishi wake wananongonezana, akagundua kuwa mtoto wake amekufa. Hivyo, akawauliza, “Je, mtoto amekufa?” Nao wakamjibu, “Naam! Amekufa.” Kisha, Daudi aliinuka kutoka sakafuni, akaoga, akajipaka mafuta na kubadilisha mavazi yake. Halafu akaenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kuabudu. Kisha akarudi nyumbani na alipotaka chakula, akapewa, naye akala. Ndipo watumishi wake wakamwuliza, “Ni jambo gani hili ulilofanya? Mtoto alipokuwa hai, wewe ulifunga na kumlilia. Lakini alipokufa, umeinuka, ukala chakula.” Daudi akawajibu, “Ni kweli mtoto alipokuwa hai, nilifunga na kulia. Nilifanya hivyo kwani nilifikiri, ‘Nani anajua? Huenda Mwenyezi-Mungu akanirehemu ili mtoto aishi’. Lakini sasa amekufa, ya nini nifunge? Je, mimi naweza kumrudisha duniani? Siku moja, nitakwenda huko alikokwenda, lakini yeye hawezi kurudi kwangu.”

2 Samueli 12:13-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia BWANA dhambi. Nathani akamwambia Daudi, BWANA naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa. Lakini, kwa kuwa kwa tendo hili umewapa adui za BWANA nafasi kubwa ya kukufuru, mtoto atakayezaliwa kwako hakika atakufa. Naye Nathani akaondoka kwenda nyumbani kwake. Basi BWANA akampiga yule mtoto ambaye mkewe Uria alimzalia Daudi naye akawa mgonjwa sana. Basi Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto; Daudi akafunga, akaingia, akalala chini usiku kucha. Nao wazee wa nyumba yake wakaondoka, wakasimama karibu naye, ili wamwinue kutoka chini; lakini hakukubali, wala hakula chakula pamoja nao. Ikawa siku ya saba, yule mtoto akafa. Nao watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia ya kuwa mtoto amekufa, maana, walisema, Angalieni, yule mtoto alipokuwa angali hai, tulisema naye, asitusikilize sauti zetu; si atajidhuru, tukimwambia ya kuwa mtoto amekufa? Lakini alipoona ya kuwa watumishi wake wananong'onezana, Daudi alitambua ya kuwa mtoto amekufa; basi Daudi akawauliza watumishi wake, Je! Mtoto amekufa? Nao wakasema, Amekufa. Ndipo Daudi akainuka pale chini akaoga, akajipaka mafuta, akabadili mavazi yake; akaingia nyumbani mwa BWANA, akasali; kisha akaenda nyumbani kwake, na alipotaka wakamwandalia chakula, naye akala. Watumishi wake wakamwambia, Ni jambo gani hili ulilolitenda? Ulifunga na kulia kwa ajili ya mtoto, alipokuwa hai; lakini mtoto alipokuwa amekufa, uliinuka ukala chakula. Akasema, Mtoto alipokuwa hai, nilifunga, nikalia; kwa maana nilisema, Ni nani ajuaye kama BWANA atanihurumia, mtoto apate kuishi? Lakini sasa amekufa nifungie nini? Je! Naweza kumrudisha tena? Mimi nitakwenda kwake lakini yeye hatanirudia mimi.

2 Samueli 12:13-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia BWANA dhambi. Nathani akamwambia Daudi, BWANA naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa. Lakini, kwa kuwa kwa tendo hili umewapa adui za BWANA nafasi kubwa ya kukufuru, mtoto atakayezaliwa kwako hakika yake atakufa. Naye Nathani akaondoka kwenda nyumbani kwake. Basi BWANA akampiga yule mtoto ambaye mkewe Uria alimzalia Daudi naye akawa hawezi sana. Basi Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto; Daudi akafunga, akaingia, akalala usiku kucha chini. Nao wazee wa nyumba yake wakaondoka, wakasimama karibu naye, ili wamwinue katika nchi; lakini hakukubali, wala hakula chakula pamoja nao. Ikawa siku ya saba, yule mtoto akafa. Nao watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia ya kuwa mtoto amekufa, maana, walisema, Angalieni, yule mtoto alipokuwa angali hai, tulisema naye, asitusikilize sauti zetu; basi hatazidi kujisumbua, tukimwambia ya kuwa mtoto amekufa? Lakini alipoona ya kuwa watumishi wake wananong’onezana, Daudi alitambua ya kuwa mtoto amekufa; basi Daudi akawauliza watumishi wake, Je! Mtoto amekufa? Nao wakasema, Amekufa. Ndipo Daudi akainuka pale chini akaoga, akajipaka mafuta, akabadili mavazi yake; akaingia nyumbani mwa BWANA, akasali; kisha akaenda nyumbani kwake, na alipotaka wakamwandalia chakula, naye akala. Watumishi wake wakamwambia, Ni neno gani hili ulilolitenda? Ulifunga na kulia kwa ajili ya mtoto, alipokuwa hai; lakini mtoto alipokuwa amekufa, uliinuka ukala chakula. Akasema, Mtoto alipokuwa hai, nalifunga, nikalia; kwa maana nalisema, Ni nani ajuaye kwamba BWANA atanihurumia, mtoto apate kuishi? Lakini sasa amekufa nifungie nini? Je! Naweza kumrudisha tena? Mimi nitakwenda kwake lakini yeye hatanirudia mimi.

2 Samueli 12:13-23 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Ndipo Daudi akamjibu Nathani, “Nimefanya dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu.” Nathani akamjibu, “Mwenyezi Mungu amekuondolea dhambi yako. Hutakufa. Lakini kwa sababu kwa kufanya hili umefanya adui za Mwenyezi Mungu kuonesha dharau kabisa, mwana atakayezaliwa kwako atakufa.” Baada ya Nathani kurudi nyumbani mwake, Mwenyezi Mungu akampiga yule mtoto ambaye mke wa Uria alikuwa amemzalia Daudi, akaugua. Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto. Akafunga na akaingia ndani ya nyumba yake akawa siku zote analala sakafuni usiku kucha. Wazee wa nyumbani mwake wakamwendea wakasimama karibu naye ili kumwamsha kutoka pale sakafuni, lakini akakataa, wala hakula chochote pamoja nao. Ilipotimia siku ya saba, yule mtoto akafa. Watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia kuwa mtoto amekufa, kwa maana walifikiri, “Mtoto alipokuwa angali hai, tulizungumza na Daudi lakini hakutusikiliza. Tutawezaje kumwambia kwamba mtoto amekufa? Anaweza kufanya kitu cha kujidhuru.” Daudi akaona kuwa watumishi wake wananong’onezana wenyewe, naye akatambua kuwa mtoto alikuwa amekufa. Akauliza “Je, ni kwamba huyo mtoto amekufa?” Wakamjibu, “Ndiyo, mtoto amekufa.” Basi Daudi akainuka kutoka pale sakafuni. Baada ya kuoga, akajipaka mafuta na kubadilisha nguo zake kisha akaenda ndani ya nyumba ya Mwenyezi Mungu, akaabudu. Baada ya hapo akaenda nyumbani mwake, akaomba wamwandalie chakula, naye akala. Watumishi wake wakamuuliza, “Kwa nini unafanya hivi? Mtoto alipokuwa angali hai, ulifunga na kulia; lakini sasa mtoto amekufa, umeinuka na kula.” Akajibu, “Mtoto alipokuwa angali hai, nilifunga na kulia. Nilifikiri, ‘Nani ajuaye? Mwenyezi Mungu aweza kunirehemu ili kumwacha mtoto aishi.’ Lakini sasa kwa kuwa amekufa, kwa nini nifunge? Je, naweza kumrudisha tena? Mimi nitaenda kwake, lakini yeye hatanirudia mimi.”