Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 12

12
Nathani amkemea Daudi
1Mwenyezi Mungu akamtuma Nathani kwa Daudi. Alipofika kwake akamwambia, “Katika mji mmoja kulikuwa na watu wawili; mmoja alikuwa tajiri na mwingine alikuwa maskini. 2Yule mtu tajiri alikuwa na idadi kubwa sana ya kondoo na ng’ombe, 3lakini yule maskini hakuwa na chochote ila kondoo jike mdogo aliyekuwa amemnunua. Akamtunza kondoo huyo, akakulia kwake pamoja na watoto wake. Kondoo huyo alishiriki chakula cha bwana wake na kunywea kikombe chake, hata pia huyo kondoo alilala mikononi mwa bwana wake. Kwake alikuwa kama binti yake.
4“Siku moja yule tajiri akafikiwa na mgeni, lakini huyo tajiri hakuchukua mmoja wa kondoo au ng’ombe wake mwenyewe amwandalie mgeni. Badala yake akachukua yule kondoo jike mdogo aliyekuwa mali ya yule maskini na kumwandalia yule mgeni wake.”
5Daudi akawakwa na hasira dhidi ya mtu huyo tajiri na kumwambia Nathani, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, mtu huyo aliyefanya hivyo anastahili kufa! 6Lazima alipe mara nne zaidi, kwa ajili ya kondoo huyo, kwa sababu amefanya jambo kama hilo na hakuwa na huruma.”
7Ndipo Nathani akamwambia Daudi, “Wewe ndiwe huyo mtu! Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Nilikupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli, nilikuokoa kutokana na mkono wa Sauli. 8Nilikupa nyumba ya bwana wako na wake za bwana wako mikononi mwako. Nikakupa nyumba yote ya Israeli na ya Yuda. Kama haya yote yalikuwa madogo sana, ningekupa hata zaidi. 9Kwa nini ulilidharau neno la Mwenyezi Mungu kwa kufanya lililo ovu machoni pake? Ulimuua Uria Mhiti kwa upanga, na kumchukua mke wake awe mkeo. Ulimuua kwa upanga wa Waamoni. 10Basi kwa hiyo, upanga hautaondoka nyumbani mwako kamwe, kwa sababu ulinidharau mimi na kumchukua mke wa Uria Mhiti kuwa mkeo.’
11“Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Kutoka kwa nyumba yako mwenyewe nitaleta maafa juu yako. Mbele ya macho yako mwenyewe nitatwaa wake zako na kumpa yeye aliye wa karibu nawe, naye atakutana kimwili na wake zako mchana mwangavu. 12Ulifanya kwa siri, lakini nitalifanya jambo hili wakati wa mchana mwangavu mbele ya Israeli yote.’ ”
13Ndipo Daudi akamjibu Nathani, “Nimefanya dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu.”
Nathani akamjibu, “Mwenyezi Mungu amekuondolea dhambi yako. Hutakufa. 14Lakini kwa sababu kwa kufanya hili umefanya adui za Mwenyezi Mungu kuonesha dharau kabisa, mwana atakayezaliwa kwako atakufa.”
15Baada ya Nathani kurudi nyumbani mwake, Mwenyezi Mungu akampiga yule mtoto ambaye mke wa Uria alikuwa amemzalia Daudi, akaugua. 16Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto. Akafunga na akaingia ndani ya nyumba yake akawa siku zote analala sakafuni usiku kucha. 17Wazee wa nyumbani mwake wakamwendea wakasimama karibu naye ili kumwamsha kutoka pale sakafuni, lakini akakataa, wala hakula chochote pamoja nao.
18Ilipotimia siku ya saba, yule mtoto akafa. Watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia kuwa mtoto amekufa, kwa maana walifikiri, “Mtoto alipokuwa angali hai, tulizungumza na Daudi lakini hakutusikiliza. Tutawezaje kumwambia kwamba mtoto amekufa? Anaweza kufanya kitu cha kujidhuru.”
19Daudi akaona kuwa watumishi wake wananong’onezana wenyewe, naye akatambua kuwa mtoto alikuwa amekufa. Akauliza “Je, ni kwamba huyo mtoto amekufa?”
Wakamjibu, “Ndiyo, mtoto amekufa.”
20Basi Daudi akainuka kutoka pale sakafuni. Baada ya kuoga, akajipaka mafuta na kubadilisha nguo zake kisha akaenda ndani ya nyumba ya Mwenyezi Mungu, akaabudu. Baada ya hapo akaenda nyumbani mwake, akaomba wamwandalie chakula, naye akala.
21Watumishi wake wakamuuliza, “Kwa nini unafanya hivi? Mtoto alipokuwa angali hai, ulifunga na kulia; lakini sasa mtoto amekufa, umeinuka na kula.”
22Akajibu, “Mtoto alipokuwa angali hai, nilifunga na kulia. Nilifikiri, ‘Nani ajuaye? Mwenyezi Mungu aweza kunirehemu ili kumwacha mtoto aishi.’ 23Lakini sasa kwa kuwa amekufa, kwa nini nifunge? Je, naweza kumrudisha tena? Mimi nitaenda kwake, lakini yeye hatanirudia mimi.”
24Ndipo Daudi akamfariji Bathsheba mkewe; akaingia kwake akakutana naye kimwili. Akazaa mwana, wakamwita jina Sulemani. Mwenyezi Mungu alimpenda Sulemani. 25Kwa kuwa Mwenyezi Mungu alimpenda, akatuma neno kwa Daudi kwa kinywa cha nabii Nathani kuwa mtoto aitwe Yedidia#12:25 maana yake Apendwaye na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
26Wakati huo Yoabu akapigana dhidi ya Raba jamii ya Waamoni na kuteka ngome ya kifalme. 27Kisha Yoabu akatuma wajumbe kwa Daudi, kusema, “Nimepigana dhidi ya Raba, nami nimetwaa chanzo chake cha maji. 28Sasa kusanya vikosi vilivyobaki na ukauzingire mji kwa jeshi na kuuteka. La sivyo, nitauteka mimi, nao utaitwa kwa jina langu.”
29Kwa hiyo Daudi akakusanya jeshi lote akaenda Raba, akaushambulia na kuuteka. 30Akachukua taji kutoka kwa kichwa cha mfalme wao, lililokuwa na uzito wa talanta moja ya dhahabu#12:30 Talanta moja ya dhahabu ni sawa na kilo 34., nalo lilizungushiwa vito vya thamani. Likawekwa juu ya kichwa cha Daudi. Alichukua nyara nyingi kutoka mjini huo. 31Akawatoa watu waliokuwa humo, akawaweka wafanye kazi kwa misumeno, sululu za chuma na mashoka, naye akawaweka kwenye kazi ya kutengeneza matofali. Akafanya hivi kwa miji yote ya Waamoni. Kisha Daudi na jeshi lake lote wakarudi Yerusalemu.

Iliyochaguliwa sasa

2 Samweli 12: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia