Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 16:1-9

2 Wafalme 16:1-9 SRUV

Katika mwaka wa kumi na saba wa Peka mwana wa Remalia Ahazi mwana wa Yothamu mfalme wa Yuda alianza kutawala. Alikuwa na umri wa miaka ishirini alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na sita katika Yerusalemu; wala hakufanya mema machoni pa BWANA Mungu wake, kama Daudi babaye. Lakini aliiendea njia ya wafalme wa Israeli, hata akampitisha mwanawe motoni, sawasawa na machukizo ya mataifa BWANA aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli. Kisha akatoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti mbichi. Hapo ndipo akakwea Resini mfalme wa Shamu pamoja na Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli juu ya Yerusalemu ili wapigane; wakamhusuru Ahazi, ila hawakuweza kumshinda. Wakati huo Resini mfalme wa Shamu akawarudishia Washami Elathi, akawafukuza Wayahudi kutoka Elathi; nao Washami wakaja Elathi, wakakaa humo hata leo. Basi Ahazi akatuma wajumbe kwa Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru, akasema, Mimi ni mtumishi, tena mwana wako; kwea, ukaniokoe mkononi mwa mfalme wa Shamu, na mkononi mwa mfalme wa Israeli, walioniinukia. Ahazi akatwaa fedha na dhahabu iliyoonekana katika nyumba ya BWANA, na katika hazina za nyumba ya mfalme, akazipeleka kwa mfalme wa Ashuru kuwa zawadi. Na huyo mfalme wa Ashuru akamsikia; mfalme wa Ashuru akapanda juu ya Dameski, akautwaa, akawahamisha watu wake mateka mpaka Kiri, akamwua Resini.