Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 16:1-9

2 Wafalme 16:1-9 NEN

Katika mwaka wa kumi na saba wa utawala wa Peka mwana wa Remalia, Ahazi mwana wa Yothamu mfalme wa Yuda alianza kutawala. Ahazi alikuwa na miaka ishirini alipoanza kutawala, akatawala huko Yerusalemu kwa miaka kumi na sita. Tofauti na Daudi baba yake, hakufanya yaliyo mema machoni pa Bwana, Mungu wake. Akaenenda katika njia za wafalme wa Israeli, na hata akamtoa mwanawe kafara katika moto, akifuata njia za machukizo za mataifa ambayo BWANA alikuwa ameyafukuza mbele ya Waisraeli. Akatoa kafara na kufukiza uvumba katika mahali pa juu pa kuabudia miungu, juu ya vilima, na chini ya kila mti uliotanda. Kisha Resini mfalme wa Aramu na Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli wakaondoka kwenda kupigana dhidi ya Yerusalemu na kumzunguka Ahazi kwa jeshi, lakini hawakuweza kumshinda. Wakati ule, Resini mfalme wa Aramu akaurudisha Elathi kwa Aramu kwa kuwafukuza watu wa Yuda. Kisha Waedomu wakahamia Elathi, nao wanaishi huko mpaka leo. Ahazi akatuma wajumbe kumwambia Tiglath-Pileseri mfalme wa Ashuru kwamba, “Mimi ni mtumishi na mtumwa wako. Njoo na uniokoe kutoka mkononi mwa mfalme wa Aramu na wa mfalme wa Israeli, ambao wananishambulia.” Naye Ahazi akachukua fedha na dhahabu zilizopatikana ndani ya Hekalu la BWANA na katika hazina ya jumba la mfalme, na kuzituma kama zawadi kwa mfalme wa Ashuru. Mfalme wa Ashuru akamwitikia kwa kushambulia Dameski na kuiteka. Akawahamishia wenyeji wake huko Kiri, na kumuua Resini.