Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 10:1-14

2 Wafalme 10:1-14 SRUV

Basi Ahabu alikuwa na wana sabini katika Samaria. Yehu akaandika barua, akazipeleka Samaria kwa wakuu wa Yezreeli, yaani, wazee na hao walezi wa wana wa Ahabu, kusema, Barua hii mara ikiwawasilia, kwa kuwa mna wana wa bwana wenu pamoja nanyi, tena kwenu kuna magari na farasi, na mji wenye boma, na silaha; basi mtazameni yeye aliye mwema na hodari miongoni mwa wana wa bwana wenu, mkamweke kitini mwa babaye, mkaipiganie nyumba ya bwana wenu. Lakini wao wakaogopa mno, wakasema, Tazama, wafalme wawili hawakusimama mbele yake; tupateje sisi kusimama? Kisha yeye aliyekuwa juu ya nyumba, na yeye aliyekuwa juu ya mji, na wazee, na walezi, wakatuma ujumbe kwa Yehu, wakisema, Sisi tu watumwa wako, kila neno utakalotuambia, tutalifanya; hatutamfanya mtu awaye yote kuwa mfalme; ufanye yaliyo mema machoni pako. Ndipo akawaandikia barua ya pili, kusema, Mkiwa upande wangu, na sauti yangu mkiisikia, vitwaeni vichwa vyao hao watu, wana wa bwana wenu, mkanijie kama wakati huu kesho hapa Yezreeli. Na hao wana wa mfalme, watu sabini, walikuwako kwa wakuu wa mji waliowalea. Ikawa, barua ilipowawasilia, waliwatwaa hao wana wa mfalme, wakawaua, watu sabini, wakatia vichwa vyao katika makapu, wakampelekea huko Yezreeli. Akaja mjumbe, akamwambia, akasema, Wamevileta vile vichwa vya wana wa mfalme. Akasema, Viwekeni marundo mawili penye maingilio ya lango hata asubuhi. Ikawa asubuhi, akatoka, akasimama, akawaambia watu wote, Ninyi ni wenye haki; tazameni, mimi nalimfitinia bwana wangu, nikamwua; ila ni nani aliyewapiga hawa wote? Jueni basi ya kwamba halianguki chini lolote la neno la BWANA, alilolinena BWANA juu ya nyumba ya Ahabu; kwa maana BWANA ameyafanya hayo aliyoyanena kwa kinywa cha mtumishi wake Eliya. Hivyo Yehu akawaua wote waliosalia wa nyumba ya Ahabu katika Yezreeli, na hao wakuu wake wote, na rafiki zake, na makuhani wake, hata hakumwachia aliyesalia hata mmoja. Akaondoka, akashika njia akaenda Samaria. Hata njiani karibu na nyumba ya kukatia manyoya kondoo, ya wachungaji. Yehu akakutana na ndugu za Ahazia mfalme wa Yuda, akawauliza, Ni nani ninyi? Wakamjibu, Sisi tu ndugu zake Ahazia; tunashuka kuwasalimu wana wa mfalme na wana wa malkia. Akasema, Wakamateni wa hai. Wakawakamata wa hai, wakawaua penye birika ya nyumba ya kukatia manyoya kondoo, watu arubaini na wawili; wala hakumsaza mtu wao awaye yote.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 2 Wafalme 10:1-14