2 Wafalme 10:1-14
2 Wafalme 10:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Ahabu alikuwa na wana sabini katika Samaria. Yehu akaandika barua, akazipeleka Samaria kwa wakuu wa Yezreeli, yaani, wazee na hao walezi wa wana wa Ahabu, kusema, Barua hii mara ikiwawasilia, kwa kuwa mna wana wa bwana wenu pamoja nanyi, tena kwenu kuna magari na farasi, na mji wenye boma, na silaha; basi mtazameni yeye aliye mwema na hodari miongoni mwa wana wa bwana wenu, mkamweke kitini mwa babaye, mkaipiganie nyumba ya bwana wenu. Lakini wao wakaogopa mno, wakasema, Tazama, wafalme wawili hawakusimama mbele yake; tupateje sisi kusimama? Kisha yeye aliyekuwa juu ya nyumba, na yeye aliyekuwa juu ya mji, na wazee, na walezi, wakatuma ujumbe kwa Yehu, wakisema, Sisi tu watumwa wako, kila neno utakalotuambia, tutalifanya; hatutamfanya mtu awaye yote kuwa mfalme; ufanye yaliyo mema machoni pako. Ndipo akawaandikia barua ya pili, kusema, Mkiwa upande wangu, na sauti yangu mkiisikia, vitwaeni vichwa vyao hao watu, wana wa bwana wenu, mkanijie kama wakati huu kesho hapa Yezreeli. Na hao wana wa mfalme, watu sabini, walikuwako kwa wakuu wa mji waliowalea. Ikawa, barua ilipowawasilia, waliwatwaa hao wana wa mfalme, wakawaua, watu sabini, wakatia vichwa vyao katika makapu, wakampelekea huko Yezreeli. Akaja mjumbe, akamwambia, akasema, Wamevileta vile vichwa vya wana wa mfalme. Akasema, Viwekeni chungu mbili penye maingilio ya lango hata asubuhi. Ikawa asubuhi, akatoka, akasimama, akawaambia watu wote, Ninyi ni wenye haki; tazameni, mimi nalifanya fitina juu ya bwana wangu, nikamwua; ila ni nani aliyewapiga hawa wote? Jueni basi ya kwamba halianguki chini lo lote la neno la BWANA, alilolinena BWANA juu ya nyumba ya Ahabu; kwa maana BWANA ameyafanya hayo aliyoyanena kwa kinywa cha mtumishi wake Eliya. Hivyo Yehu akawapiga wote waliosalia wa nyumba ya Ahabu katika Yezreeli, na hao wakuu wake wote, na rafiki zake, na makuhani wake, hata hakumwachia aliyesalia hata mmoja. Akaondoka, akashika njia akaenda Samaria. Hata njiani karibu na nyumba ya kukatia manyoya kondoo, ya wachungaji. Yehu akakutana na ndugu za Ahazia mfalme wa Yuda, akawauliza, Ni nani ninyi? Wakamjibu, Sisi tu ndugu zake Ahazia; tunashuka kuwasalimu wana wa mfalme na wana wa malkia. Akasema, Wakamateni wa hai. Wakawakamata wa hai, wakawaua penye birika ya nyumba ya kukatia manyoya kondoo, watu arobaini na wawili; wala hakumsaza mtu wao awaye yote.
2 Wafalme 10:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Katika mji wa Samaria kulikuwa na wana sabini wa Ahabu. Yehu akaandika barua na kuzituma kwa watawala wa mji, kwa viongozi na kwa walinzi wa wana wa Ahabu. Barua yenyewe ilisema hivi: “Kwa kuwa mnao miongoni mwenu wana wa mfalme, kadhalika mnao farasi na magari, silaha na miji ya ngome, mchagueni na kumtawaza mwenye uwezo zaidi kati ya wana wa mfalme; halafu mpige vita kwa ajili ya ukoo wa mfalme.” Watawala wa Samaria waliogopa sana na kusema, “Tunawezaje kumpiga Yehu hali mfalme Yoramu na mfalme Ahazia hawakuweza?” Kwa hiyo ofisa mkuu wa nyumba ya mfalme na ofisa mkuu wa mji, wakishirikiana na viongozi wengine na walinzi, wakampelekea Yehu ujumbe huu: “Sisi tu watumwa wako, na tuko tayari kufanya lolote unalosema. Lakini hatutamtawaza mtu yeyote kuwa mfalme; fanya unavyoona vyema.” Yehu akawaandikia barua nyingine akiwaambia: “Ikiwa kweli mko tayari kufuata maagizo yangu, leteni hapa Yezreeli vichwa vya wana wa bwana wenu; nivipate kesho wakati kama huu.” Wana sabini wa mfalme Ahabu waliishi kwa viongozi wa Samaria, ambao walikuwa walezi wao. Basi, barua ilipowafikia waliwachukua hao wana wa mfalme na kuwakata wote sabini. Waliweka vichwa vyao vikapuni na kumpelekea Yehu huko Yezreeli. Kisha mtumishi mmoja akamwendea na kusema, “Vichwa vya wana wa mfalme vimekwisha letwa.” Ndipo akaamuru, “Viwekwe chini katika mafungu mawili kwenye lango la mji; halafu viache vikae huko mpaka asubuhi.” Asubuhi yake akatoka, akasimama na kuwaambia watu wote, “Nyinyi ni waadilifu, angalia mimi nilikula njama dhidi ya bwana wangu na kumuua. Lakini ni nani aliyewaua hawa wote? Jueni ya kwamba maneno yote aliyosema Mwenyezi-Mungu kuhusu jamaa ya Ahabu yametimia. Mwenyezi-Mungu ameyafanya hayo aliyosema kwa njia ya mtumishi wake Elia.” Ndipo Yehu akaua jamaa yote ya Ahabu iliyokuwa inakaa Yezreeli, pamoja na maofisa wake na marafiki na makuhani wake; hakumwacha mtu yeyote. Baadaye Yehu aliondoka Yezreeli, akaelekea Samaria. Akiwa njiani mahali panapoitwa “Kambi ya Wachungaji,” alikutana na jamaa za marehemu Ahazia mfalme wa Yuda akawauliza, “Nyinyi ni kina nani?” Wakamjibu, “Sisi ni jamaa za Ahazia. Tumeteremka huku kuwatembelea wana wa mfalme na wana wa malkia.” Kisha akasema, “Wakamateni wakiwa hai.” Wakawakamata watu arubaini na wawili, wakawaulia karibu na kisima cha “Kambi ya Wachungaji.” Hakuna aliyebaki hata mmoja.
2 Wafalme 10:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Ahabu alikuwa na wana sabini katika Samaria. Yehu akaandika barua, akazipeleka Samaria kwa wakuu wa Yezreeli, yaani, wazee na hao walezi wa wana wa Ahabu, kusema, Barua hii mara ikiwawasilia, kwa kuwa mna wana wa bwana wenu pamoja nanyi, tena kwenu kuna magari na farasi, na mji wenye boma, na silaha; basi mtazameni yeye aliye mwema na hodari miongoni mwa wana wa bwana wenu, mkamweke kitini mwa babaye, mkaipiganie nyumba ya bwana wenu. Lakini wao wakaogopa mno, wakasema, Tazama, wafalme wawili hawakusimama mbele yake; tupateje sisi kusimama? Kisha yeye aliyekuwa juu ya nyumba, na yeye aliyekuwa juu ya mji, na wazee, na walezi, wakatuma ujumbe kwa Yehu, wakisema, Sisi tu watumwa wako, kila neno utakalotuambia, tutalifanya; hatutamfanya mtu awaye yote kuwa mfalme; ufanye yaliyo mema machoni pako. Ndipo akawaandikia barua ya pili, kusema, Mkiwa upande wangu, na sauti yangu mkiisikia, vitwaeni vichwa vyao hao watu, wana wa bwana wenu, mkanijie kama wakati huu kesho hapa Yezreeli. Na hao wana wa mfalme, watu sabini, walikuwako kwa wakuu wa mji waliowalea. Ikawa, barua ilipowawasilia, waliwatwaa hao wana wa mfalme, wakawaua, watu sabini, wakatia vichwa vyao katika makapu, wakampelekea huko Yezreeli. Akaja mjumbe, akamwambia, akasema, Wamevileta vile vichwa vya wana wa mfalme. Akasema, Viwekeni marundo mawili penye maingilio ya lango hata asubuhi. Ikawa asubuhi, akatoka, akasimama, akawaambia watu wote, Ninyi ni wenye haki; tazameni, mimi nalimfitinia bwana wangu, nikamwua; ila ni nani aliyewapiga hawa wote? Jueni basi ya kwamba halianguki chini lolote la neno la BWANA, alilolinena BWANA juu ya nyumba ya Ahabu; kwa maana BWANA ameyafanya hayo aliyoyanena kwa kinywa cha mtumishi wake Eliya. Hivyo Yehu akawaua wote waliosalia wa nyumba ya Ahabu katika Yezreeli, na hao wakuu wake wote, na rafiki zake, na makuhani wake, hata hakumwachia aliyesalia hata mmoja. Akaondoka, akashika njia akaenda Samaria. Hata njiani karibu na nyumba ya kukatia manyoya kondoo, ya wachungaji. Yehu akakutana na ndugu za Ahazia mfalme wa Yuda, akawauliza, Ni nani ninyi? Wakamjibu, Sisi tu ndugu zake Ahazia; tunashuka kuwasalimu wana wa mfalme na wana wa malkia. Akasema, Wakamateni wa hai. Wakawakamata wa hai, wakawaua penye birika ya nyumba ya kukatia manyoya kondoo, watu arubaini na wawili; wala hakumsaza mtu wao awaye yote.
2 Wafalme 10:1-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wakati huu katika Samaria walikuwepo wana sabini wa nyumba ya Ahabu. Kwa hiyo Yehu akaandika barua na kuzituma Samaria: kwa maafisa wa Yezreeli, kwa wazee, na kwa walezi wa watoto wa Ahabu. Akasema, “Mara tu barua hii itakapokufikia, kwa kuwa wana wa bwana wako wapo pamoja nawe, nawe una magari ya vita na farasi, mji wenye ngome na silaha, mchague mwenye uwezo zaidi kati ya wana wa bwana wako, na umweke juu ya kiti cha enzi cha baba yake. Kisha upigane kwa ajili ya nyumba ya bwana wako.” Lakini wakaogopa sana na kusema, “Ikiwa wafalme wawili hawakuweza kupambana na Yehu, sisi tutawezaje?” Basi msimamizi wa jumba la mfalme, mtawala wa mji, na wazee na walezi wakatuma ujumbe huu kwa Yehu: “Sisi tu watumishi wako, na tutafanya kila kitu utakachosema. Hatutamteuwa mtu yeyote kuwa mfalme. Wewe fanya uonalo kuwa ni bora.” Kisha Yehu akawaandikia barua ya pili, akisema, “Ikiwa ninyi mko upande wangu na mtanitii mimi, twaeni vichwa vya wana wa bwana wenu, na mnijie huku Yezreeli kesho wakati kama huu.” Wakati huo wana sabini wa mfalme walikuwa wakiishi pamoja na viongozi wa mji wa Samaria, waliokuwa wakiwalea. Hiyo barua ilipowafikia, watu hawa wakawachukua wale wana sabini wa mfalme na kuwachinja wote. Wakaweka vichwa vyao ndani ya makapu na kumpelekea Yehu huko Yezreeli. Mjumbe alipofika, akamwambia Yehu, “Wameleta vichwa vya wana wa mfalme.” Ndipo Yehu akaagiza, “Viwekeni malundo mawili katika ingilio la lango la mji mpaka asubuhi.” Asubuhi yake, Yehu akatoka nje. Akasimama mbele ya watu wote na akasema, “Hamna hatia. Ni mimi niliyefanya shauri baya dhidi ya bwana wangu na kumuua, lakini ni nani aliyewaua wote hawa? Fahamuni basi kwamba, hakuna neno ambalo BWANA amesema dhidi ya nyumba ya Ahabu ambalo halitatimia. BWANA amefanya lile aliloahidi kupitia mtumishi wake Eliya.” Hivyo Yehu akaua kila mtu huko Yezreeli aliyekuwa amebaki wa nyumba ya Ahabu, ikiwa ni pamoja na wakuu wake, rafiki zake wa karibu, na makuhani wake. Hakuacha yeyote anusurike. Kisha Yehu akaondoka kuelekea Samaria. Alipokuwa njiani karibu na nyumba ya kukatia manyoya ya kondoo, yaani, Beth-Ekedi ya wachunga kondoo, Yehu akakutana na watu wa jamaa ya Ahazia mfalme wa Yuda, akauliza, “Ninyi ni nani?” Wao wakasema, “Sisi ni jamaa ya Ahazia, nasi tumeshuka kuwasalimu jamaa ya mfalme na ya mama malkia.” Yehu akaagiza, “Wakamateni wakiwa hai!” Kwa hiyo wakawachukua wakiwa hai, watu arobaini na wawili, na kuwachinja kando ya kisima cha Beth-Ekedi. Hakuacha yeyote anusurike.