Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 9:10-23

1 Wafalme 9:10-23 SRUV

Ikawa miaka ishirini ilipopita, ambayo katika hiyo Sulemani alizijenga zile nyumba mbili, nyumba ya BWANA na nyumba yake mfalme, (basi Hiramu, mfalme wa Tiro, alikuwa amemletea Sulemani mierezi na miberoshi, na dhahabu, sawasawa na haja zake zote), ndipo mfalme Sulemani akampa Hiramu miji ishirini ya nchi ya Galilaya. Naye Hiramu akatoka Tiro kuitazama hiyo miji Sulemani aliyompa; wala hakupendezwa. Akasema, Miji gani hii uliyonipa, ndugu yangu? Akaiita nchi ya Kabuli, hata leo. Hiramu alikuwa amemletea mfalme talanta mia moja na ishirini za dhahabu. Na hii ndiyo sababu ya shokoa aliyoitoza mfalme Sulemani; ili kuijenga nyumba ya BWANA, na nyumba yake mwenyewe, na Milo, na ukuta wa Yerusalemu, na Hasori, na Megido, na Gezeri. Farao, mfalme wa Misri, alikuwa amepanda akautwaa Gezeri, na kuuteketeza kwa moto, akawaua Wakanaani waliokaa mjini, akampa zawadi binti yake, mkewe Sulemani. Naye Sulemani akaujenga Gezeri, na Beth-horoni wa chini, na Baalathi, na Tamari ulio nyikani, katika nchi; na miji yote ya hazina iliyokuwa yake Sulemani; na miji ya magari yake, na miji ya watu wake wapandao farasi, na kila alichopenda kujenga Sulemani huko Yerusalemu, na katika Lebanoni, na katika nchi yote ya mamlaka yake. Kwa habari ya watu wote waliosalia, Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi, na Wayebusi, wasiokuwa wa wana wa Israeli; watoto wao waliosalia baada yao katika nchi, ambao wana wa Israeli hawakuweza kuwaharibu kabisa, katika hao Sulemani akawatumikisha shokoa hata leo. Lakini kwa wana wa Israeli Sulemani hakumtumikisha mtu yeyote shokoa; ila wao walikuwa askari, watumishi wake, makamanda wake, maafisa wake, makamanda wa magari yake na wapanda farasi wake. Hao maofisa wakuu, waliokuwa juu ya kazi yake Sulemani, walikuwa mia tano na hamsini, waliowasimamia watu watendao kazi.