Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 9:10-23

1 Wafalme 9:10-23 NENO

Miaka ishirini ilipopita, muda ambao Sulemani alijenga majengo haya mawili, yaani Hekalu la BWANA na jumba la kifalme, Mfalme Sulemani akampa Hiramu mfalme wa Tiro miji ishirini katika Galilaya, kwa sababu Hiramu alikuwa amempatia mierezi na misunobari yote na dhahabu yote kama alivyohitaji. Lakini Hiramu alipotoka Tiro kwenda kuiona ile miji ambayo Sulemani alikuwa amempa, hakupendezwa nayo. Hiramu akauliza, “Hii ni miji ya namna gani uliyonipa, ndugu yangu?” Naye akaiita nchi ya Kabul, jina lililoko hadi leo. Basi Hiramu alikuwa amempelekea mfalme talanta mia moja na ishirini za dhahabu. Haya ni maelezo kuhusu kazi za kulazimishwa ambazo Mfalme Sulemani aliwafanyiza watu ili kulijenga Hekalu la BWANA, na jumba lake la kifalme, na Milo, ukuta wa Yerusalemu, Hazori, Megido na Gezeri. (Farao mfalme wa Misri alikuwa ameushambulia na kuuteka mji wa Gezeri. Alikuwa ameuchoma moto. Akawaua Wakanaani waliokuwa wakikaa humo na kisha kuutoa kwa binti yake, yaani mkewe Sulemani, kama zawadi ya arusi. Sulemani akaujenga tena Gezeri.) Akajenga Beth-Horoni ya Chini, akajenga Baalathi na Tamari kwenye jangwa katika eneo la nchi yake. Vilevile, alijenga miji ya ghala na ya magari yake ya vita na kwa ajili ya farasi wake na wapanda farasi: alijenga kila alichotaka katika Yerusalemu, katika Lebanoni, na katika eneo lote alilotawala. Watu wote waliosalia miongoni mwa Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi, na Wayebusi (watu wasiokuwa Waisraeli), yaani, wazao wao waliobakia katika nchi, ambao Waisraeli hawakuwaangamiza kabisa, Sulemani akawalazimisha kuwa shokoa, kama ilivyo hadi leo. Lakini Sulemani hakumfanya Mwisraeli yeyote kuwa mtumwa; hao ndio walikuwa wapiganaji wake, viongozi wa serikali yake, maafisa wake, wakuu wake wa jeshi, majemadari wa magari yake ya vita, na wapanda farasi wake. Pia walikuwa maafisa wakuu wasimamizi wa miradi ya Sulemani: maafisa mia tano na hamsini waliwasimamia watu waliofanya kazi.