Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 1:1-10

1 Wafalme 1:1-10 SRUV

Mfalme Daudi alikuwa mzee, mkongwe katika siku zake, nao wakamfunika nguo, lakini asipate joto. Kwa hiyo watumishi wake wakamwambia, Bwana wangu mfalme na atafutiwe kijana mwanamwali; naye asimame mbele ya mfalme, amtunze; alale kifuani mwako, ili bwana wangu mfalme apate joto Basi wakatafuta msichana mzuri katika nchi yote ya Israeli, wakamwona Abishagi, Mshunami, wakamleta kwa mfalme. Naye msichana huyo alikuwa mzuri sana; akamtunza mfalme, akamtumikia; lakini mfalme hakumjua. Ndipo Adonia mwana wa Hagithi akatakabari, akasema, Mimi nitakuwa mfalme. Akajiwekea tayari magari na wapanda farasi, na watu hamsini wapige mbio mbele yake. Tena baba yake hakumchukiza wakati wowote kwa kusema, Mbona umefanya hivi? Kisha, alikuwa mtu mzuri sana; naye alizaliwa baada ya Absalomu. Akashauriana na Yoabu, mwana wa Seruya, na Abiathari, kuhani; nao wakamsaidia Adonia, wakamfuata. Ila Sadoki, kuhani, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Nathani, nabii, na Shimei, na Rei, na mashujaa wa Daudi, hao hawakuwa pamoja na Adonia. Adonia akatoa sadaka ya kondoo, ng'ombe na ndama wanono, karibu na jiwe la Zohelethi, lililo karibu na chemchemi Enrogeli; akawaita ndugu zake wote, wana wa mfalme, na watu wote wa Yuda, watumishi wa mfalme; ila nabii Nathani, Benaya, walinzi wa mfalme na Sulemani ndugu yake hakuwaalika.